Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.

Kufananishwa na mnyama sio jambo la heshima sana, sawa na mtu kukufananisha na ng’ombe. Yaani akili yako ipo kama ya ng’ombe, pamoja na ng’ombe kuwa na nyama tamu na maziwa mazuri, bado haiwezi kuwa heshima mtu kufananishwa na ng’ombe.

Binadamu tunazo akili za kuweza kufikiri mema na mabaya, tofauti na mnyama yeyote yule chini ya jua. Pamoja na kuwa na akili ya kujua mema na mabaya, bado tunafanya vitu kama wanyama wasio na akili.

Unakataa vipi huwezi kufanana na mnyama wakati unaabudu sanamu isiyoweza kusema chochote wala haina uhai wowote. Unaamini vipi kitu cha uongo, tena cha kuchonga na mfua vyuma/dhahabu.

Utaachaje kufananishwa na mnyama, upo kanisani lakini bado unaenda kwa miungu mingine kutafuta msaada. Na bado unamwomba Mungu huyu huyu akutendee mambo makuu katika maisha yako.

Utaachaje kufananishwa akili yako na mnyama, na wakati unaishi na mwanaume asiye wako na unajua ameoa mke wake. Unazini na mke wa mtu, na unajua ameolewa, unaishi na binti wa shule ndani kwako, huku kwao wanajua yupo shule.

Tumekuwa na mioyo migumu sana, hatutaki kusikia,wala hatuki kubadilika kwa yale tunayoamini ni sawa kuyafanya. Lakini si sawa kuyaishi kama wakristo, kwa sababu tu ya kutokuwa na maarifa sahihi, tunakuwa tunayaishi.

Neno la Mungu linamfananisha mtu asiye na maarifa ni kama mnyama, mnyama hawezi kujiongoza mwenyewe, mnyama hawezi kufanya maamzi yake kama anavyoweza kufanya mtu.

Imekuwa rahisi kuamini kila roho ambazo zingine sio zinazotoka kwa Mungu, hata mtu umwambie hapo sio sawa, ataona kama vile unamwonea wivu. Hii ni kwa sababu ufahamu wake umekosa maarifa sahihi ndani yake kutoka kwa Mungu.

Tusiwe kama mnyama, tujaza maarifa ya Neno la Mungu, yatatusaidia katika maisha yetu ya kiroho. Huenda tulipo tunajiona tupo sahihi, tunaona hivyo kwa sababu ya kukosa maarifa sahihi, ila ukweli tulipo sio mahali sahihi kabisa.

Usahihi wake tutaanza kujua pale tukapojua iliyo kweli, na kweli yenyewe inapatikana ndani ya Neno la Mungu. Hakuna namna unaweza kukwepa maarifa haya yatokanayo na maandiko matakatifu.

Zipo elimu zingine za kidunia sio sahihi, kukosa kwako maarifa ya Neno la Mungu, unaweza kuyaona ni sahihi, kwa sababu hujui Maandiko Matakatifu yanavyosema juu ya hayo unayoyaamini na kuyafanya.

Wakati mwingine unayakataa maarifa sahihi kwa sababu umejaza elimu potofu ndani yako. Inakuwa ngumu kuelewa kwa sababu moyo wako umetiwa ganzi na elimu isiyo sahihi.

Tukatae kwa pamoja kuwa kama wanyama, hakuna jehanamu ya ng’ombe wala mbuzi, ipo jehanamu yetu sisi wanadamu.

Rejea: Kila mtu amekuwa kama mnyama, hana maarifa; Kila mfua dhahabu amefedheheshwa na sanamu yake ya kuchonga; Maana sanamu yake ya kuyeyuka ni uongo, Wala hamna pumzi ndani yake. YER. 51:17 SUV

Nimekupitisha kwenye andiko hilo uweze kuona, huenda ulianza kufikiri hakuna mstari wa namna hiyo. Andiko linaposema kila mtu amekuwa kama mnyama, halikuwa kundi dogo la watu wala haikuwa mtu mmoja, walikuwa watu wengi.

Usikokotwe kama mnyama, hebu amua mwenyewe kuchota maarifa ndani ya Neno la Mungu. Hapa sharti uokoke kwanza na uruhusu Roho Mtakatifu awe ndani yako, maana unaweza kusoma na usielewe chochote.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

+255759808081.