Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, kama umeamka huna furaha kutokana na hali unayopitia, hebu mfurahie Mungu na mshukuru kukupa nafasi nyingine tena ukiwa hai.

Tunakutana na changamoto nyingi sana katika maisha yetu, tena zingine ni ngumu haswa kulinganisha na jinsi tunavyoziona kwenye fahamu zetu.

Tunapokuwa na changamoto, kila mmoja ana namna ya kukabiliana nazo, wengine wakishapatwa na changamoto ngumu, anapoteza kabisa hali yake fulani nzuri aliyokuwa nayo. Kinachomfanya apoteze huo uzuri ni kule kuwaza kwake sana.

Lipo kundi la wachanga wa kiroho wao nao wana namna ya kuzibeba changamoto, lakini asilimia kubwa huwa zinawaondoa kwenye malengo yao. Na wakati mwingine huwa wanamezwa moja kwa moja na changamoto hizo.

Kuna kundi la waliokomaa kiroho nao wana namna ya kukabiliana na changamoto ngumu, wanajua mahali sahihi pa kutiwa nguvu katika yale wanayopitia. Na wanaona ni shule kwao kwa yale wanayopitia, utawaona uhusiano wao na Mungu ukizidi kuimarika zaidi.

Lipo jambo ambalo wengi huwa tunalitumia, huenda kwa kujua ama pasipo kujua chochote. Uvivu umekuwa ukisumbua wengi sana hasa kwenye mambo ya kiMungu, hasa katika kusoma neno la Mungu.

Wengi wanatumia mwavuli wa changamoto kufichia uvivu wao, akishakutana na kachangamoto kidogo kwake inakuwa furaha sana. Maana amepata kitu cha kusingizia kwanini hakufanya lile alilopaswa kulifanya.

Kweli zipo changamoto zinaweza kutupata na kutukwamisha baadhi ya mambo yetu, ila wengi wetu huwa tunazibeba kulea uvivu tulionao. Jifikirie mwenyewe siku umepanga jambo fulani kulifanya, ukitaka kulifanya unajisikia ka uvivu, ili kujipa moyo unaangalia changamoto gani inayokukabili wakati huo, ukishaipata tu unajiingiza humo kujifichia.

Tunafanya hivyo sana kwenye Neno la Mungu, wengi wanashindwa kuendelea kusoma Neno la Mungu kwa sababu ya uvivu wao wenyewe. Wanachofanya ili wasionekane ni uvivu ndio umewafanya waache kusoma, wanatafuta changamoto yeyote inayowakabili wanaingia humo.

Atakuwa hivyo siku zote, atakachoendelea kukifanya ni kuendelea kuingiza uvivu wake kwenye changamoto tofauti tofauti anazokutana nazo mbele kwa mbele.

Kujiondoa kwenye tabia hii ya uvivu, ni kuamua kufanya hata pale unapokuwa hujisikii vizuri, hii itakupa nafasi ya kuendelea kuonekana imara siku hadi siku. Mbinu hii unaweza kuitumia hata kwenye shughuli zako zingine unazozifanya kila siku.

Siku umeamka unaona una nafasi ya kusoma Neno la Mungu alafu uvivu unakuambia usisome, uvivu unaenda mbali zaidi kwa kukuambia ona changamoto hii ilivyo ngumu kwako. Ukiona hivyo wewe jaribu kutuliza mawazo yako kisha soma biblia yako, hata kama huoni sana unachokifanya wakati huo ni bora zaidi kuliko kuacha.

Changamoto zipo na zitaendelea kuwepo siku zote, inatoka hii leo, inaingia nyingine kesho, mchezo huu unaenda nao mwaka mzima. Ukijidekeza sana utajikuta unakwama kila mwaka kwenye mpango wako wa kusoma Neno la Mungu kila siku.

Leo tumezungumzia sana kuhusu UVIVU unavyoturudisha nyuma kwa kutumia changamoto zetu kujifichia humo, kwa kuwa umejifunza na umejua adui yako ni uvivu na sio changamoto unazokutana nazo. Basi ni vyema ukajipanga katika hilo.

Shika sana hili, popote utakapokuwa, kama una nafasi ya kusoma Neno la Mungu, hata kama nafasi ni ndogo sana ilimradi ipo. Nakusihi sana usome Neno la Mungu, utaona ukisogea hatua moja kwenda nyingine kubwa zaidi.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

WhatsApp 0759808081