Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.
Haijalishi itapita miaka mingapi huko mbele, Neno lake litabakia AMINA, haijalishi vipindi vingapi vitapita ikiwa Neno lake limesema. Hakuna kitu kitaweza kuzuia hilo jambo lisiweze kutokea kwako au kwangu.
Tunachokosea ni kutokujua Neno lake, laiti tungelijua na kulishika mioyoni mwetu, tungekuwa na ujasiri mkubwa sana mbele za Mungu. Tungekuwa na uhakika wa kufanya kazi ya Bwana sawaswa na mapenzi yake, kwa maana upo ujasiri kwa tunachofanya.
Mioyo yetu inasinyaa haraka kwa sababu ya kukosa msingi wa Neno lake, tunakuwa na msingi imara zaidi wa dini zetu kuliko Neno lake. Msingi wa dini zetu, unatutaka tuishi kama mapokeo ya dini zetu zinavyotaka, ambapo wakati mwingine zinakuwa kinyume na Neno lake.
Kuomba kwetu ili kusiweze kuzuiliwa na yaweze kujibiwa yale tumwombayo, tunapaswa kuomba sawa sawa na Neno lake, nje na hapo tunakuwa tunaomba maombi ambayo yanakuwa kelele mbele zake. Maana hatujui itupasavyo kuomba sawa sawa na Neno lake.
Tunaweza kukaa utumwani bila sisi kujua kama tumeshawekwa huru siku nyingi kwa kukosa tu neno lake, ama tunaweza kuendelea kukaa kifungo cha magereza kwa kutojua neno lake. Tungejua tungeweza kutoka hilo gereza la mateso, maana ipo kanuni ambayo ingetuwezesha kutupa kibali cha kutoka mahali pale.
Unapaswa kuelewa haya vizuri, kinachoangaliwa na yeye ni neno lake tu, kama neno lake linasema utamiliki uwe na uhakika ni kweli. Kama alisema utakuwa huru kweli kweli, uwe na uhakika na uhuru huo upo ukiudai kupitia Neno lake.
Haijalishi utakaa utumwani miaka mingapi, alafu ukaja ukajua Neno lake linasemaje kuhusu kukaa huko utumwani, itakuwa ni rahisi kwako kujua ule muda uliopangwa ukae utumwani utakuwa umeshaisha kwa mjibu wa Neno lake.
Siri hii aliijua Daniel kutokana na tabia yake ya kusoma vitabu, akajua ahadi ya Bwana iliyoshusha kupitia nabii wake Yeremia. Alijuaje hili? Nimesema kwa kuvisoma vitabu, tena sio kimoja ni vingi sana, kwa mjibu wa maandiko matakatifu.
Rejea: katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini. Danieli 9:2 SUV.
Sijui kama umeona kitu hapo kwenye mstari huo juu, Daniel aligundua vitu vingi kutokana na tabia yake ya kusoma vitabu, ambavyo vilivyokuwa na ahadi mbalimbali za Mungu.
Kupitia hili andiko uhakika upo kupishana na baraka za Mungu kwa kutojua neno lake, maana anachoangalia yeye kwetu ni Neno lake ndipo aweze kulitimiza. Na ili alitimiza kwako ni mpaka ulijue kwanza ndipo uweze kumdai kwa kuomba.
Zipo nyakati nyingine ngumu tunapita, kwa sababu ya kukosa Neno lake, tunakuwa tunafikiri ni sahihi kuendelea kupita nyakati zile. Kumbe Mungu alitegemea tumwombe sawasawa na Neno lake ili aweze kutuvusha kwenye ugumu ule; wakati mwingine tunaweza kujiona Mungu ametuacha kumbe ilinenwa utakuja wakati kama huo mgumu, na maelekezo yakawepo tulipaswa kufanyaje tukikutwa na wakati kama huo.
Ngoja nikupitishe kwenye andiko hili ili uone kweli haya ninayokuambia, huenda bado unakataa kuhusu hili Mungu kuangalia Neno lake ndipo aweze kulitimiza kwetu wanadamu.
Rejea: Ndipo Bwana akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize. Yeremia 1:12 SUV.
Mimi sijui una mpango gani hadi sasa wa kusoma Neno la Mungu, tumeona Daniel alikuwa msoma vitabu ndipo akagundua vitu. Tunasoma tena kuwa Mungu anaangalia Neno lake ndipo aweze kulitimiza kwetu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
WhatsApp 0759808081