Nakusalimu katika jina lililo kuu la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai sasa na hata milele.
Nyakati ambazo tulitakiwa kuonyesha ukomavu wetu wa kiroho, ndio wakati ambao tunakimbia. Hata ule ujasiri wa kusema kwa watu unakuwa haupo, maana sisi wenyewe hatuonyeshi ule ukomavu wetu kama wakristo.
Mtu alikuwa mtu wa ibada, humkosi kwenye vipindi kanisani, humkosi akijitoa kwa mambo mbalimbali, acha aguswe na tatizo fulani. Ile bidii yake inaonekana kuondoka kabisa, sio kwamba hawezi kuonyesha tena ile bidii yake, ile hamu ndani yake imetoweka kabisa.
Mtu anayempenda Mungu wakati wa raha tu, huyo mtu anakosea sana, kwa sababu hapa duniani hakuna raha ya moja kwa moja. Utaumizwa moyo wako na mambo mbalimbali katika maisha yako, hupaswi Kurudi nyuma, utapoteza vile vitu ulivyokuwa unavipenda sana, hupaswi kurudi nyuma.
Wakati mwingine unaona umelemewa sana na mzigo mzito, hadi unaanza kuona imani yako imeshuka huku ukiwa na maumivu makali moyoni mwako. Bado hupaswi kuonyesha kuchoshwa na mambo ya Mungu, ile bidii yako inakuwa pale pale hata kama umelala kitandani.
Hupaswi kusinyaa moyo wako na kuanza kuonyesha umenyanyua mikono ishara ya hutaki tena kuendelea na safari uliyoanza nayo kwa juhudi kubwa. Badala yake unapaswa kujua hayo ni ya muda tu, kama bado una uwezo wa kufanya kile kilikuwa kinamletea Mungu sifa na utukufu, fanya. Tena fanya zaidi kwa muda unaokuwa nao, hata kama sio ule muda wako wa kawaida, onyesha bado Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako.
Sio unaguswa kidogo na kachangamoto, unaacha na kusoma Neno la Mungu, inamaanisha ulikuwa husomi ipasavyo. Mtu anayesoma Neno la Mungu vizuri na kulitafakari kila wakati, hawezi kurudishwa nyuma na mambo madogo madogo.
Matatizo/changamoto zinatusaidia kujijua tumefikia hatua gani katika ukuaji wetu wa kiroho, yapo mambo magumu kweli yatakujia. Hapo ndipo mahali pako sahihi kujua/kufahamu umesogea hatua fulani kiroho ama bado umedumaa pale pale kiroho.
Hatuwezi kusema kwa maneno matupu tumekomaa kiroho pasipo kuona matendo ya kututhibitishia kweli tumekomaa. Nasema hivi huwezi kusema nilivipigana vita sana wakati huo umetoroka hivyo vita, watu hawatakuelewa, utaeleweka pale utakapovivumilia hivyo vita hadi mwisho wakachukua ushindi.
Sasa wewe ndugu yangu, mtu anakukwaza kidogo unaacha kusoma Neno la Mungu wiki, kwa madai kwamba akili yako haipo sawa. Huo ni uchanga wa kiroho wala hakuna kitu kingine hapo, unamweka mtu moyoni wa nini na wakati unapaswa kumsamehe, na kumwachilia kabisa moyoni mwako?
Haijalishi inakuja nini mbele yako, iambie kabisa sijaacha kusoma Neno la Mungu, hapa napumzika tu kidogo, kesho naanza tena kusoma neno la Mungu. Hakuna kukubali kirahisi hivyo, kwanza utakubalije kirahisi wakati hukuokoka kirahisi? Ulihangaika kujiondoa kwenye kifungo cha dhambi, Yesu Kristo akakusaidia, leo shetani anataka kukurudisha unamkubalia kirahisi hivyo! Shauri yako.
Jipime mwenyewe na jiambie kabisa, katika changamoto hii ngumu, nataka kumfurahisha Mungu wangu aliye hai kuwa alinikoa kwa gharama kubwa sana. Sio umeokoka alafu umelegeaa…ukitikiswa kidogo na kachangamoto/katatizo unapeperushwa nako moja kwa moja, ni aibu mbaya.
Natamani kusikia hivi kwako, napita kwenye wakati mgumu, lakini siwezi kurudi nyuma katika usomaji wangu wa Neno la Mungu. Maana najua Neno la Mungu ni chakula changu cha kiroho, bila Neno la Mungu maisha yangu bado hajawa salama. Haya yawe maneno ya mkristo yeyote yule mwenye safari ya kwenda mbinguni.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
WhatsApp 0759808081.