Ndugu katika Kristo, nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.

Kupumzika au kujipa likizo ni nzuri sana, maana inakupa nafasi ya kujitafakari na kujikagua maisha yako na utendaji wako. Pia inakupa nafasi ya kukusanya nguvu zingine za kuja kuanza kwa namna ya tofauti na isiyo ile ya mazoea.

Kupumzika/likizo inaamsha kiu mpya ya kufanya zaidi, kwa sababu ya kukaa nje ya lile jambo bila kulifanya. Wengi waliotumia vizuri mapumziko yao ya likizo, walikuja na kasi ya tofauti kabisa katika kazi zao.

Ndio maana tunaona shule zinakuwa na awamu kadhaa za mapumziko ndani ya mwaka mmoja, hii inampa nafasi mwalimu na mwanafunzi kuwa nje ya kile alichokuwa anafanya kila siku. Kutokana na mazingira yetu na malezi yetu, badala ya kupumzika unaona wanafunzi wengi wanaendelea na tuition.

Ile dhana ya kupumzika kabisa unaona haipo, kutokana labda na mzazi kuona mtoto wake anakuwa bize sana na michezo na kusahau kabisa mambo ya shule. Na kuanza kuingiza vitu tofauti kabisa asivyovitaka mzazi wake.

Pamoja na kupumzika kote kwa mwezi mzima, ipo tarehe maalum iliyopangwa kurudi shule kuendelea na masomo. Uwe bado unatamani kuendelea na likizo, hilo ni juu yako, ila tarehe iliyopangwa ikifika tu masomo yanaanza/yanaendelea. Inakulazimu sasa kusitisha mambo yako mengine ili kuanza masomo ya pamoja na wenzako, usipoanza pamoja na wenzako maana yake unaachwa nyuma licha ya kuonekana mtoro.

Nataka kukuambia nini hapa, nataka kukuambia hili, mambo mengi tunajifunza ukubwani, hatukuwa na msingi imara tangu mwanzo. Na jambo la kujifunza ukubwani usipokuwa makini utaanza vizuri ila kadri siku zinavyoenda uwezekano wa kuacha ni mkubwa.

Unapojifunza tabia mpya ukubwani, hupaswi kujipa sababu sana ya kutokufanya, uwe unajisikia vizuri au vibaya unapaswa kufanya tu. Ili kuliweka vizuri ndani ya moyo wako jambo uliloanzisha katika maisha yako ya kila siku.

Kusoma biblia takatifu ni kama shule, usipoenda leo, kesho utawakuta wenzako wamekuacha, maana yake hapo una kazi mbili, ya siku iliyopita na siku uliyoenda shuleni. Lakini wenzako wanakuwa na kazi moja tu ya siku husika.

Wengi wanakuja kushindwa kuendelea kusoma Neno la Mungu, pale wanapoacha kwenda na wenzao waliopatana kusoma Neno la Mungu kila siku. Maana peke yao walishindwa kutokana na kuanza kujifunza hili ukubwani, na wale aliokuwa anasoma nao Neno la Mungu nao wanakuwa wamemwacha sana nyuma kwa kupumzika kwake.

Changamoto ni kwamba, kadri anavyozidi kupumzika wenzake wanazidi kwenda mbele, siku anakuja kusema ngoja nianze tena. Anaona ameachwa sana, anaona ngoja aendelee kupumzika, mapumziko yasiyo na ukomo.

Ukweli kabisa tulio wengi kusoma Neno la Mungu tumejifunzia/tunajifunzia ukubwani, unapojipa mapumziko ni sawa na kujipa tiketi ya kuacha kabisa kusoma Neno la Mungu. Maana unajua hakuna atakayekuja kwako kukuuliza mbona husomi Neno la Mungu, tofauti na shule unaweza kufuatiliwa na ukachukuliwa hatua kali za kinidhamu.

Mambo mengine hupaswi kupumzika kufanya, unavyozidi kujipumzisha ndivyo unavyozidi kurundika mzigo mkubwa wa kazi. Na mzigo wa kazi ukishakuwa mkubwa hata ule ufanisi wako wa utendaji unakuwa mdogo, na kuna asilimia kubwa kuruka ruka baadhi ya kazi.

Nitakushangaa sana umeanza kujifunza juzi kusoma Neno la Mungu, alafu unajipa mapumziko, huko ni kujipeleka kwenye maisha yako ya zamani. Ambayo hukuwa unasoma kabisa Neno la Mungu zaidi ya kusomewa jpili au kuambiwa fungua mstari fulani usome.

Binafsi sijui kama mtu anaweza kuchoka kukaa na Mungu, sijui kama yupo mtu anasema ngoja nikae mbali kidogo na Neno la Mungu kwa muda fulani alafu akabaki salama. Huko ni kuasi ndugu yangu, ukishakaa mbali na Neno la Mungu, unafikiri kinachofuata ni kipi kama sio shetani kuingiza agenda zake.

Usijiambie moyoni mwako una mapumziko/likizo, huko ni kujirudisha nyuma mwenyewe, Neno la Mungu ni chakula chako cha kiroho, huwezi kuacha kula kwa miezi miwili, hata kama ni maombi ya kuvunga huwezi. Inakuwaje wewe unajipumzisha kula Neno la Mungu miezi sita hadi mwaka mzima?

Bila shaka umejifunza mengi, nami naamini hivyo, maana nimekupitisha maeneo mbalimbali katika maisha yako ili uelewe zaidi hili ninalokueleza. Usiache kusoma Neno la Mungu katika maisha yako yote.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

WhatsApp 0759808081