Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.
Ipo misisitizo inayotegemea hali ya mtu, akiwa na hali nzuri atasisizwa kufanya mambo fulani kutegemeana na hali aliyonayo. Akiwa kwenye hali ngumu naye atasisitizwa kutokana hali yake ngumu, na inaweza kutokea akaachwa kusisitizwa kufanya lile alilokuwa analifanya.
Misisitizo ipo maeneo mbalimbali katika maisha yetu, ipo kwenye familia, ipo makazini, ipo makanisani, ipo kwenye biashara, ipo mashuleni/vyuoni, ipo mashambani na maeneo mengine mengi.
Misisitizo mingi inakuwa na msimu maalum wa kuhamasishwa, baada ya hapo huwezi kusikia ukihimizwa hilo jambo mpaka pale msimu utapofika tena. Na ipo misisitizo mingine yenyewe inapaswa kuwepo kila siku ya maisha yako hapa duniani.
Fungu tuliochagua ni fungu la kusisitizana kila wakati ili tuweze kwenda pamoja siku zote za maisha yetu, hili fungu limekaa kama hiari ya moyo wako na upande mwingine limekaa kama lina ulazima wa mtu kujituma yeye binafsi. Bila kuangalia mazingira mazuri au mabaya, bila kuangalia yupo mahali anapitia pagumu sana au palaini sana.
Haijalishi msimu wa kiangazi wala masika, msisitizo huu upo pale palepale wa kuhakikisha kila mmoja anaenda pamoja na wenzake. Bila kujalisha mazingira na msimu fulani.
Kama ni Wimbo basi utabaki kuwa uleule, haijalishi watu watakubaliana nao wala haijalishi watu wataukataa, bado msisitizo utabaki pale pale. Ili kama yupo alianza kuchoka aone hapaswi kuchoka, na kama alikuwepo mwenye moyo mgumu, moyo wake upate kuwa mlaini kwa jinsi anavyozidi kusikia msisitizo huo.
Nia haswa ya msisitizo huu ueleweke vizuri kwetu sisi au kwako wewe na mimi, pia uende kizazi hadi kizazi, wakati wa kufanya hayo ni sasa. Hatuwezi kutishwa na hali ya sasa tukaacha kusisitizana yale ya muhimu kuyazingatia.
Kwa namna moja ama nyingine unaweza kufika mahali ukaona kawaida kawaida kutokana na kusikia sana msisitizo huu. Na huenda imefika mahali umeanza kuona kero ya makelele, na huenda msisitizo huu umekuwa kiongozi kwako kukusaidia pale unapotaka kujisahau kama ulikuwa na safari.
Msisitizo huu ni upi? Msisitizo huu ni SOMA NENO UKUE KIROHO,hakuna siku tutaacha kulisema hili, inaweza kubadilika namna ya kulisema. Lakini lengo litakuwa palepale kwenye Neno la Mungu, haiwezi kubadilika kwa namna ya kusema haina maana tena kusoma Neno la Mungu.
Ukerwe ama ufurahie huu msisitizo, hautazuia chochote katika hili, unaweza kufanikiwa kunyamazisha mdomo ila mioyo yetu itabaki na wimbo ule ule. Hadi unamaliza safari yako hapa duniani, utakuwa huna mahali utasingizia sikusikia hili.
Kama huwa unasoma tu Neno la Mungu ukiwa na hali nzuri kifedha, tabia hiyo uache mara moja, na kama huwa unasoma tu Neno la Mungu ukiwa na hali mbaya kiuchumi na kiafya. Wakati unatafuta msaada wa Mungu ndio unakuwa na bidii sana, hiyo tabia uache mara moja, usimpende Mungu na kumtafuta kwa bidii kwa matukio fulani.
Siku zote za maisha yako hapa duniani unapaswa kumpenda Mungu wako, na kuishi maisha matakatifu yanayompendeza Mungu wako. Bila kuangalia mazingira mazuri au mabaya, nafasi ya Mungu wako ibaki pale pale.
Msisitizo huu wa wewe kusoma Neno la Mungu sitauacha kamwe, madamu nipo hai, sio nakusisitiza wewe tu alafu mimi nakaa pembeni sifanyi kile nakuambia. Nakusisitiza kitu ninachokiishi mimi kila siku, usione tu nakuambia soma Neno la Mungu, nami nasoma.
Nikiacha mimi kusema, Mungu atainua mwingine wa kulisema hili, ndio maana nikakuambia msisitizo huu hutoacha kuusikia kwenye maisha yako yote hapa duniani. Hakuna mahali utaenda usiweze kusikia hili la kusoma Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081