Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.

Zipo safari mnapanga pamoja na mkiahairisha, mnahairisha wote kwa pamoja kutokana na jinsi safari yenyewe ilivyokaa kwenu. Hii haiwezi kukuathiri mahali popote pale, kwa sababu haikuwa inagusa maisha yako moja kwa moja.

Zipo safari hata wengine waamue kuhairisha wote, unapaswa kwenda mwenyewe bila kuangalia wangapi wameamua kuachana na safari mliyopanga kwenda kwa pamoja.

Safari za maisha zipo nyingi, ila leo tuzungumzie sana safari yetu ya kwenda mbinguni, safari hii ina mkusanyiko wa mambo mengi ndani yake. Ila tunaenda kuangalia machache ambayo yanaweza kuwa msaada kwetu.

Tunapaswa kwenda kwa pamoja katika safari hii ya kwenda mbinguni, ambayo inatuhitaji kuishi maisha matakatifu yanayompendeza yeye. Katika kuishi huko maisha matakatifu, tunapaswa kumzalia Mungu matunda yaliyo mema.

Na ili tuishi maisha matakatifu, tunapaswa kuwa na mwongozo sahihi wa kutusaidia kuishi maisha yale ambayo hayana maswali hata kwa wale wanaotutazama. Maana ukishatangaza umeokoka, unakuwa barua inayosomwa na kila mtu.

Katika safari hii, wengi huwa wanakata kamba njiani na kuamua kuyarudia mambo yao ya kale, wengine kuacha bidii yao waliyokuwa nayo kwa mambo ya Mungu, kama vile kusoma Neno la Mungu, ibada za kanisani, maombi na mengine mengi yanayofanana na hayo.

Unapaswa kuelewa haya, kila mmoja anaenda kutoa hesabu ya matendo yake mwenyewe, pamoja na tunaonekana kama kundi kubwa tunaokusanyika pamoja siku za jpili. Elewa kila mmoja anaenda kuhukumiwa yeye kama yeye, hakuna undugu katika hilo.

Rejea: Kwani atamlipa binadamu kwa kazi yake, Naye atamfanya kila mtu kuona sawasawa na njia zake. Naam, hakika, Mungu hatatenda mabaya, Wala Mwenyezi hatapotosha hukumu. Ayubu 34 :11_12 SUV.

Inapotokea mwenzako amerudi nyuma na wewe unaanza kutamani kurudi nyuma kama yeye, naanza kupata wasiwasi huenda hukujua Neno la Mungu linasemaje kuhusu hili.

Ungejua usingeiga tabia ambazo wengine wanakuwa nazo, kwa sababu fulani ameacha bidii kwa mambo ya Mungu, na wewe unaacha. Kwa sababu fulani ameacha njia iliyo safi, na wewe unaamua kuacha njia safi.

Haijalishi wenzako wote wataacha kusoma Neno la Mungu, usikubali na wewe kuacha hili uliloamua kuliishi katika maisha yako ya wokovu. Lengo lako ni moja tu, kumpendeza Mungu wako na si mwanadamu, ukishajua haya huwezi kuishia njiani katika usomaji wa Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

+255759808081