Bwana Yesu asifiwe sana mwana wa Mungu, tunayo siku nyingine tena mpya kabisa Bwana ametupa kibali cha kuweza kuiona. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa nafasi hii aliyotupa.

Chochote unachokifanya ukiwa na furaha nacho, utakifanya vizuri zaidi, hata unapokutana na kikwazo ni rahisi sana kukitatua. Kwa sababu kipo kitu kinachokusukuma kwa nguvu ndani yako, ambacho ni furaha ndani yako juu ya kile unachokifanya.

Usipofurahia kazi unayofanya, uwe na uhakika itageuka kuwa mzigo mzito kwako, haijalishi hiyo kazi nzuri kiasi gani kama utakosa furaha ndani yako juu ya hiyo kazi. Utaona mwenyewe unakuwa mzito kwa kila kitu, hata ule ujasiri wa kusema nafanya kazi fulani, na mahali fulani unakuwa haupo tayari kabisa.

Sio kwamba ni siri kutokusema unapofanyia kazi, ni vile huna furaha kabisa na kile unafanya, unapokosa furaha kwa kile unafanya unaanza kuona unachukia kabisa ndani yako. Na kadri siku zinavyozidi kwenda mbele, unaona unazidi kurudi nyuma zaidi katika ufanisi wako wa utendaji.

Achana na kuvunjwa moyo, nasemea kukosa furaha kwa kile unafanya, unaweza kuvunjwa moyo lakini ukashangaa ukapata nguvu mpya ya kuendelea mbele. Kwa sababu kile unachovunjwa moyo, wewe una furaha nacho ndani ya moyo wako, wala huhitaji kusukumwa katika hilo.

Haijalishi ni kitu gani au ni jambo gani, ukikosa furaha nalo uwe na uhakika umekaribia kushindwa kwa hilo jambo. Inawezekana ikawa mahusiano ya ndoa au uchumba, ukiona umeanza kukosa kumfurahia mwenzako ujue kugombana kupo karibu sana na kama ni wachumba ujue kuachana ni muda wowote.

Furaha ni ya muhimu sana katika jambo unalolifanya, ukiacha kufurahia unachofanya, utaona uvivu umeanza kukuingia, utaanza kuona hilo jambo linakukera kulifanya, utaanza kuona ugumu unaingia kwako. Na wakati siku za nyuma ulipokuwa unafurahia kufanya ulikuwa huoni yote hayo, hata kama hali ya kukosa furaha ilikuja hukuizingatia sana.

Kusoma kwako Neno la Mungu unapaswa kufurahia siku zote, ukiona umeanza vizuri ukiwa na furaha alafu ghafla ile furaha ikakatika, ukaanza kusoma Neno la Mungu kwa kusitasita. Uwe na uhakika unaenda kuacha kabisa kama utaruhusu hiyo hali iendelee kwako.

Rejea: Furahini, basi, enyi wana wa Sayuni, mkamfurahie Bwana, Mungu wenu; kwa kuwa yeye huwapa ninyi mvua ya masika, kwa kipimo cha haki, naye huwanyeshea mvua, mvua ya masika, na mvua ya vuli, kama kwanza. Yoeli 2:23 SUV

Kufurahia ni agizo la Mungu, ukiona umeanza kukosa furaha kama nilivyoanza kusema mwanzo, ujue hicho ulichokuwa unakiamini au unakifanya utakiacha. Furaha isikosekane ndani ya moyo wako, linda sana hili.

Furahia usomaji wako wa Neno la Mungu, hata utakojisikia kuchoka, ile furaha iliyo ndani yako itakusukuma kufanya tu, ile furaha itakufanya usione ugumu wa kutokufanya. Maana ukikumbuka unafurahia kwa sababu unafanya kwa ajili ya Bwana, inakupa nguvu zaidi ya kufanya huku unafurahia.

Unaweza kuwa unapenda kusoma Neno la Mungu Lakini ukikosa furaha ndani yako, hutoweza kusoma zaidi utaendelea kusema moyoni napenda kusoma Neno la Mungu ila sina muda, mara biblia ngumu, sababu zinakuwa chungu nzima.

Mfurahie Mungu wako na mambo yake utayafurahia bila kusukumwa na mtu yeyote, utashangaa ukijisukuma mwenyewe kutoa muda wako kwa ajili yake. Neno la Mungu utaliona ni chakula chako cha kiroho, bila kula chakula hicho utaona hutoweza kuishi maisha matakatifu yanayompendeza yeye Bwana Yesu.

Rejesha furaha yako.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

+255759808081