Uthamani wa kitu unakuja pale unapoliona linakusaidia katika maisha yako, pia uthamani unakuja pale unapoona jambo linagusa maisha yako moja kwa moja. Kwa namna ya kukutoa sehemu ambayo ulikuwa umekwema na kukupeleka hatua nyingine mbele ambayo hukutegemea kwa akili zako za kawaida kufikia.

Hilo jambo la kukusogeza hatua moja mbele, bila kusukumwa na chochote au yeyote, utalithamini sana, maana umeshajua ni daraja lako la kukupeleka hatua nyingine mbele. Hutokubali kirahisi likupite kwa namna yeyote ile na kwa gharama yeyote ile, hii inakuja kwa kujua uthamani wa jambo lenyewe.

Tuchukulie hii michezo ya bahati nasibu, wengi wanaingia mle na kuwa walevi wa hii michezo kwa sababu walijaribu kucheza mara ya kwanza wakabahatika kula pesa. Hiyo imewafanya wanakesha usiku na mchana kucheza hiyo michezo bila kujua athari zake, wakiamini ipo siku watabahatisha tena kama mwanzo.

Na wale ambao waanza kucheza hii michezo ya bahati nasibu, ni kwa sababu wameona marafiki zao wakiondoka na kiasi kikubwa cha pesa. Lakini ukija katika uhalisia ni michezo ambayo inakula pesa nyingi sana za watu, na kile kidogo wanapewa wachache waliobahatisha.

Utaona uthamani wa kuipenda hii michezo ulikuja kwa kupata jambo fulani, ndivyo ilivyo na dhambi yeyote ile, huwa haianzi kwa matokeo ya ubaya. Ubaya unakuja baadaye sana ukishakolea sana na huwezi kujiondoa kwa haraka kwenye kifungo ulichofungwa.

Neno la Mungu wengi wetu tunalisoma kama historia fulani za nyuma sana waliotendewa mambo makuu wana wa Israel, tunaona kwetu sisi inakuwa ngumu Mungu kutenda mema na mambo mengine makuu katika maisha yetu.

Ndio maana tunapopatwa na shida, tunaomba Mungu atusaidie kama alivyomsaidia mtu fulani aliyeandikwa kwenye Biblia. Lakini ndani ya mioyo yetu tumejaa hofu na mashaka, hatuna imani kabisa kama Mungu anaweza kutenda na kwetu leo.

Hasa inapofika katikati ya jaribu tunalopitia bila kupata majibu kwa Mungu wetu, huwa tunaanza kuona Mungu hawezi kutenda kwetu alitenda zamani ila sio sasa. Unapofikiria hayo yote ile ladha, ile bidii yako ya kusoma Neno la Mungu inakatika kabisa, kwa sababu hujapata matokeo chanya katika kumwamini kwako Kristo.

Wale waliomwona Yesu Kristo akitenda mambo makuu katika maisha yao, huwezi kuwaambia kitu wanapofika eneo la kumpa Mungu muda wao. Huwezi kuwasukuma kwa nguvu kuhusu ibada, huwezi kuwasukuma kuhusu maombi, huwezi kuwasukuma kuhusu kusoma Neno la Mungu.

Wanajua Mungu alipowatoa kwenye tobe zito ambalo wasingeweza kutoka kwa nguvu zao, wanajua uthamani wa Yesu Kristo kufa msalabani kwa ajili yao. Wakisikia semina ya Neno la Mungu, hawana visingizio vya kuwafanya wasihudhurie semina ile, maana wanajua nguvu iliyopo ndani ya Neno la Mungu.

Tofauti kabisa na mtu ambaye bado hajajua nguvu ya Neno la Mungu katika maisha yake, huyu mtu atakuwa mzito sana kwenye Neno la Mungu. Huyu mtu lazima asukumwe kila saa, huyu mtu asome, asisome, yeye hajisikii kupungukiwa kitu walacha kuongezeka kitu.

Hebu nikupitishe kwa ufupi mistari michache ya kukuonyesha umhimu wa Neno la Mungu, uone ni jinsi gani hili ukilijua utaanza kukosekana kwenye majina ya watu wasiopenda kusoma Neno la Mungu. Na utaanza kupatikana kwenye majina ya wanaosoma Neno la Mungu kila siku bila kujalisha wakati gani unapitia.

Rejea: Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Yohana 5:24 SUV.

Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli. Yohana 8:31 SUV.

Yesu akajibu, akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Yohana 14:23 SUV.

Naomba urudie tena kusoma maandiko hayo matakatifu, huenda ulisoma kwa haraka, rudia tena kwa utulivu na umakini, utaona Neno la Mungu lilivyo la muhimu kwako. Usipoliona hili utaendelea kumtafuta mchawi wako, unapaswa kujua thamani ya Neno la Mungu.

Unapaswa kujua/kufahamu Neno la Mungu sio historia fulani iliyopita, neno la Mungu ni halisi kabisa kwako, kazi yako ni kuliamini na kulishika moyoni mwako. Hapo utaona mambo makubwa Mungu akitenda katika maisha yako, ndio usikatae ni mambo makubwa na sio madogo.

Kumbuka hili, Kujitoa kwako kwa jambo lolote lile, inategemea sana uthamani wako unaoupata kwenye hilo jambo.

Tukutane wakati mwingine.

Chapeo Ya Wokovu

www.chapeotz.com

WhatsApp +255759808081.