Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.
Mengi tunahalalisha kuwa ni dhambi kwa mitazamo yetu binafsi, na mengine jinsi hisia zetu binafsi zinavyotutuma tunajiambia jambo fulani ni dhambi. Bila kufuatilia kwa umakini hayo tunayofikiri ni dhambi au sio dhambi.
Mambo mengi tunayabebesha u dhambi, kwa sababu fulani tunayemwamini sisi alisema ni dhambi kwa mtazamo wake binafsi. Kwa kuwa na sisi ni wavivu wa kusoma maandiko matakatifu, nasi tulioambiwa tunaanza kusambaza uongo kuufanya ni dhambi.
Tunapaswa kuelewa hata hawa manabii, mitume, wachungaji na walimu wa uongo, sio kila wanchokifanya ni uongo la hasha. Yapo ya ukweli mengi sana tena mengine yapo ndani ya Neno la Mungu, sema katika hayo ya ukweli uongo unachomekwa ndani yake.
Usijenge dhana mbaya/potofu sana kwa kila unayesikia ni nabii wa uongo, wakati mwingine sio wa uongo, ila kwa kuwa anayeyafanya watu hawayajui au kwa kuwa ni hila tu za watu, na wewe unajiunga na kundi linalofikiri ni wa uongo.
Leo wengi wanayapa mambo mengi kuwa dhambi, kwa sababu mimi silipendi jambo fulani kwa sababu zangu binafsi, nawaambia wengine ni dhambi, bila kuwaambia ukweli kwa nini silipendi hilo jambo. Ili niamue mwenyewe niliyesikia na mimi halinifai kulifanya au niwe mwangalifu katika kulifanya.
Nakueleza haya mambo ili uwe mwangalifu sana, hasa kwa wewe unayetoa muda wako kila siku kusoma Neno la Mungu. Najua huko nyuma kuna mengi sana ulikuwa unafikiri ni dhambi, ila baada ya kuanza kusoma Neno la Mungu umeanza kugundua mengi.
Ukisikia jambo fulani ni dhambi alafu hujalielewa vizuri, usiwe mwepesi kutamkia watu ni dhambi, kwa sababu aliyekuambia au uliyemsikia ni mtu unayemwamini. Huwezi kujua na yeye huenda kuna mtu wake anayemwamini alimwambia ni dhambi.
Tuwe kama watu wa Beroya, watu waliokuwa wanachunguza maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu yale waliyofundishwa. Hawakujalisha aliyewafundisha alikuwa mtume kweli wa Mungu, wao walijenga utaratibu huo wa kuchunguza maandiko matakatifu.
Rejea: Watu hawa walikuwa waungwana kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa walilipokea lile neno kwa uelekevu wa moyo, wakayachunguza maandiko kila siku, waone kwamba mambo hayo ndivyo yalivyo. Matendo 17 :11 SUV.
Leo hatuchunguzi maandiko matakatifu, bali tunaendeshwa na hisia zetu binafsi za chuki, kwa sababu fulani simpendi, basi namtengenezea mazingira kila anachokisema yeye ni dhambi. Hata kama lipo la ukweli ndani yake, na mwingine kwa sababu anaaminika na wengi basi kila anachokisema dhambi kinakuwa dhambi. Hata kama Neno la Mungu halisemi dhambi wenyewe wanalipa u dhambi.
Tuwe makini sana, tujifunze kurudi kwenye Maandiko Matakatifu yanasemaje, tuwe watu wa kulinganisha maneno au mahubiri au mafundisho tunayofundishwa, yamo ndani biblia zetu au hayamo. Pia tujifunze yale tunayosikia ni dhambi, tujifunze kurudi kwenye Maandiko Matakatifu tuone yana ukweli ndani yake au ni hila tu za watu.
Neno la Mungu likiwa kwa wingi ndani yako, hata ile hekima ya kiMungu inakuwa ndani yako, kuna vitu vidogo vidogo havimo ndani ya Neno la Mungu. Lakini ukivifanya ni dhambi, na moyoni unashuhudiwa hivyo kabisa kuwa hichi ulichokifanya hakimpendezi Mungu, kwa sababu Roho Mtakatifu ni mwaminifu atakuletea na fundisho linalokusaidia kujua hilo jambo ni dhambi.
Tuachane na mitazamo ya kibinadamu, turudi kwenye Neno la Mungu linasemaje, na tuache tabia ya kudokoadokoa maandiko, tusome kwa kina kujua mambo kwa upana wake. Tutaanza kuona nguvu ya Neno la Mungu ikitenda kazi ndani yetu.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081