Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.
Tunaenda kumaliza mwaka huu 2017, ni mwaka ambao hatutauona tena katika maisha yetu, ndio hatutaweza kuona tena huu mwaka 2017.
Haijalishi uliupenda sana kuendelea kuwepo mwaka huu, hiyo haiwezi kuzuia kuingia mwaka mwingine. Bado siku chache ibaki kusimulia mwaka 2017 nilifanyaga hili na lile, wakati huo ukiwa mwaka mwingine kabisa.
Haijalishi mwaka huu 2017 ulikuwa ni mwaka wa changamoto ngumu sana kwako, amini tunaenda kuumaliza huu mwaka, mangapi umejifunza, mangapi umeyafanya. Hilo linabaki moyoni mwako, ila fahamu tunaenda kufunga mahesabu ya mwaka 2017.
Haijalishi ulitabiriwa nini mwaka huu, na hicho ulichotabiriwa hakijaweza kutimia kwako, kutotimia kwa hilo ulilotabiriwa hakuwezi kuzuia mwaka 2017 kuisha.
Haijalishi mwaka huu uliahidiwa kupewa nini, kama hujapewa hakuwezi kufanya mwaka huu ukaendelea kuwepo, utaondoka na kuingia mwingine. Hata kama bado ulikuwa unatamani kuendelea kujiona ndani ya mwaka 2017, bado haiwezi kufanya utaratibu ubadilike wa kutouona mwaka mwingine.
Kilicho cha mhimu ni kuangalia kipi umefanikiwa, na kipi hujafanikiwa, ili uweze kuchukua hatua zaidi unapoanza mwaka 2018. Hii itakufanya kutorudia makosa yale yale, itakusaidia kuongeza bidii/nguvu zaidi pale ulipolegeza mwendo. Pia itakusaidia kutoishi kwa mazoea, ambapo mazoea hayo yamekufanya uzidi kurudi nyuma badala ya kusonga mbele.
Hatua zako zilizoonekana ndogo ulivyoanza mwaka 2017, kama hukuchoka njiani tangu January hadi leo December, bila shaka utakuwa umeonekana umepiga hatua kubwa sana. Hata kama mwanzo ilionekana inakupa shida, hata kama siku za mwanzo ulikutana na changamoto ngumu.
Ikiwa hukukubali kurudi nyuma, leo ninapokuandikia haya utakuwa mtu mwingine kabisa mwenye hatua nyingine tofauti na yule aliyerudia njiani. Hamwezi kulingana kamwe hata kama mnaonekana wote mna urefu/ufupi ule ule, kimaarifa hamlingani kabisa.
Faida ya kusoma Neno la Mungu sura moja kila siku, huenda ikaonekana ni hatua ya kipuuzi kabisa kwa mtu anayeanza au kwa anafikiri kuanza. Ila faida yake ni kubwa sana kwa yule atakayezingatia na kuelewa kile anafanya.
Sura moja tunaweza kuifananisha na mwaka mmoja mmoja tunaoingia, kuingia huku mwaka mmoja imetufanya leo tupo 2017 ambapo muda sio mrefu tunaenda kuacha huu mwaka. Nguvu ya mwaka mmoja imetupelekea tunazidi kuona miaka mingine zaidi iliyo mbele yetu.
Unaweza usielewe sana faida ya kusoma Neno la Mungu sura moja kila siku kwa wakati huo, ila nakuhakikishia hutochukua muda mrefu bila kuona matunda ya kusoma sura moja kila siku. Sura moja tu, ndio ni sura moja tu ya kitabu kitakatifu cha Biblia.
Kaa utafakari sura moja kila siku tangu mwaka uanze, imeweza kugharimu dakika ngapi za muda wa kazi yako, masomo yako, na biashara zako. Unaweza kuona ni dakika chache sana ila zimekufanya uondoke na kitu kikubwa ambacho ukiendelea nacho utaendelea kuvuna matunda yake zaidi kila siku.
Usipuuze hata siku moja sura moja ya kitabu kitakatifu cha Biblia, ina matokeo mazuri sana kama hutokata kamba njiani. Siku moja ikikupita hutoiona tena, ndivyo ilivyo na kusoma sura moja hutorudia pale pale kila siku, utasogea sura nyingine.
Ukisoma leo sura moja, amini kesho utasoma nyingine, lakini hiyo hatua inaletwa na sura moja, hata kama utamaliza vitabu kumi kwa mfumo wa kusoma sura moja.
Unapopuuza kusoma Neno la Mungu kwa sababu unaona kusoma sura moja kila siku ni kupoteza muda, unapaswa kujiuliza ulivyopanga kusoma sura nyingi. Je! Umesoma vitabu vingapi hadi sasa? Je! Umendelea na mpango wako huo huo au umeishiaga njiani?
Nguvu ya sura moja katika kusoma Neno la Mungu, ina faida kubwa sana hasa kwa mtu ambaye anajua akisubiria kusoma sura nyingi hatopata huo muda. Lakini kupitia sura moja moja kila siku ameweza kusoma Biblia nzima, na kuendelea kurudia tena kwa utaratibu ule ule wa kupata kitu kipya cha kumsaidia katika maisha yake ya wokovu.
Fuata hii kanuni ya nguvu ya sura moja kila siku, utaona matunda yake kila unapomaliza mwaka kama hivi.
Mungu akusaidie kuelewa hili.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081