Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, ashukuriwe Yesu Kristo ametupa nafasi nyingine tena ya kuweza kuiona siku ya leo.

Vipo vitu vinavyoonekana vya maana sana kwetu hadi kutufanya tushindwe kupata muda wa kutosha kujifunza mambo ya Mungu. Pamoja na kuonekana vina umhimu sana hivyo vitu, vitafika wakati vinapita na kutuacha mikono mitupu.

Yapo mambo yanaonekana mazuri sana kwetu, mambo hayo hutufanya tunakuwa bize kiasi kwamba tunakosa muda wa kutosha kumpa Mungu wetu, hasa katika eneo la kujifunza Neno lake. Lakini pamoja na hayo mambo yote mazuri yanaonekana ni ya maana sana kwetu, yatafika kipindi yatatoweka kwetu.

Wapo watu tunawapenda sana kuwaona katika maisha yetu, pamoja na upendo huo, utafika wakati hatutaweza kuwaona tena. Maana watakuwa wameshapita muda wao wa kuwepo hapa Duniani, ila lile ambalo tutaendelea kuwa nalo siku zote, yule ambaye ataendelea kuwa nasi siku zote. Ndio hatuna muda naye kabisa, ingekuwa ni rafiki wa kushikilia kwa nguvu zote ni huyu wa kudumu siku zote.

Vitu vidogo vidogo vya kupita vinatufanya tuwe bize kiasi kwamba tunakosa muda wa kusoma Neno la Mungu ambalo linadumu nyakati zote. Lakini tunashindwa kulijua hili, labda kutokana na kupuuza kwetu au labda kutokujua kwetu.

Kutokujua kwetu hakuwezi kutufanya kubadili ukweli wa hili jambo, Neno la Mungu ndio msingi imara wa mwanadamu, kama umekiri Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Unapaswa kuelewa vizuri hili jambo, bila kuangalia mazingira wala hali uliyonayo wakati huo.

Rejea:Majani yakauka, ua lanyauka; Bali neno la Mungu wetu litasimama milele. ISA. 40:8 SUV

Rafiki mzuri uliyenaye leo, itafika muda hutokuwa naye, ila Neno la Mungu litasimama milele, kazi nzuri uliyonayo leo, itafika muda hutokuwa nayo, ila Neno la Mungu wetu litasimama milele. Huenda nguvu zako nyingi umeziweka kwenye mambo ya mwilini kuliko ya rohoni, ila fahamu kwamba hayo yatapita, ila kile unakikwepa kitadumu siku zote.

Kama ni kutoa muda kwa mambo ya msingi, tungejikita kwenye kujenga urafiki mkubwa kwenye Neno la Mungu, hili lipo na wewe wakati wote. Tena linakupa namna ya kukabiliana na changamoto ngumu za hapa Duniani, pia linakuelekeza namna ya kuishi maisha matakatifu yanayompendeza Mungu wako.

Huwezi kushinda dhambi pasipo kuwa na Neno la Mungu la kutosha ndani yako, ndio itakuwa ngumu kushinda dhambi pasipo kuwa na Neno la Mungu ndani yako. Ni ngumu kuepuka kudanganywa na watumishi waongo pasipo kuwa na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwako.

Rejea: Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. Zab. 119:11 SUV.

Sijui moyoni mwako unawaza nini juu ya hili, sijui umeweka mipango gani juu ya usomaji wako wa Neno la Mungu, sijui umewekeza nguvu gani katika usomaji wako wa Neno la Mungu. Fahamu hili ndilo linaishi siku zote, ila vingine vyote vitapita.

Haijalishi kuna kitu gani unakipenda, wala haijalishi kuna mtu gani unampenda sana, amini hivyo vyote vinapita, ila Neno la Mungu wetu litadumu Milele. Sio kwamba vya kupita tuvidharau la hasha tunapaswa kutoa muda wetu kwa kile kinachodumu milele, sio tuwekeza nguvu zetu nyingi kwenye vya kupita, ila cha kudumu tunawekeza nguvu kidogo.

Unaweza kusema cha kudumu chenyewe si kipo tu, ngoja tuwekeze nguvu kwa vinavyopita, ndio unaweza kufanya hivyo ukakosa muda wa kujiweka vizuri kwa maisha ya umilele. Kutojiandaa kwa maisha ya umilele ni hatari zaidi kuliko unavyofikiri, maana hicho ndicho utakachodumu nacho siku zote tofauti na maisha ya hapa Duniani.

Bila shaka umejifunza kitu kupitia ujumbe huu, endelea kutafakari zaidi lipo la kuweka moyoni mwako.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081