Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.

Mapatano siku zote huwa zaidi ya mtu mmoja, mnaweza kuwa wawili,watatu au watano au kikundi cha zaidi ya watu watano. Katika kikundi chenu mnaweza kuwekeana utaratibu wa kufanya jambo lolote lile mtakalopatana.

Kupanga mtapanga vizuri, na kupatana mtapatana vizuri, inabaki kila mmoja kujisimamia ili aweze kutekeleza lile ambalo mlipangiana kuhakikisha mnalifanya mkiwa pamoja.

Mara nyingi mnapofika katika utendaji, hutokea changamoto mbalimbali, hasa katika kutenda pamoja, tena kuna vitu vipya kabisa hutokea ukiwa ndani ya patano. Ambavyo vitu hivyo hukuvijua kabla, katika kuvijua hivyo vitu, vipo vitakusababisha upate moyo wa kuendelea mbele, na vipo vitakufanya uvunjike moyo wa kutoendelea mbele.

Vikundi ni vizuri sana, na vile vile vikundi vinaweza kutumika kukurudisha nyuma kwa jambo ulilodhamiria kulifanya katika mpango wako wa maisha. Hasa unapofika wakati ulipanga kufanya alafu ikatokea ukavunjwa moyo, huwa ni ngumu sana kuja kurudi tena kufanya.

Wengi wanapanga pamoja kusoma Neno la Mungu, wanapopanga pamoja, wengi wanakuwa hawajajipanga na changamoto ngumu wanazoweza kukutana nazo mbele ya safari yao. Wanapofika wakati kama huo, hujikuta wanarudi nyuma zaidi ya kabla hawajaanza kusoma Neno la Mungu.

Kurudi nyuma huko, wengi hukufanya kama changamoto yao ya kuweza kujipanga upya tena, na wengine hufanya ndio mwisho wao wa kuendelea na usomaji wao wa Neno la Mungu.

Unapokuwa kwenye mapatano ya kikundi fulani, usifikiri utahamasishwa tu, upo wakati pia unaweza kuvunjwa moyo na mtu tu. Kama ulikuwa na moyo mwepesi, na ulikuwa hujakomaa vizuri kiroho na kiakili, unaweza kukichukia kile ulichokianzisha kukifanya.

Vizuri ukalijua hili, katika mapatano hasa ya vikundi, sio yote yatakupa moyo wa kusonga mbele, yapo yanakuvunja moyo. Na utatamani kurudi nyuma, na usipotamani kurudi nyuma utajikuta huna hamu ya kuendelea kufanya kile ulikuwa unafanya.

Hili lipo sehemu yeyote ile, unapaswa kujifunza kusimama haswa, hasa unapogundua ulichoamua kufanya ni sahihi kwako na kina manufaa kwenye maisha yako. Hii inabaki ni binafsi yako, yaani maamzi yasiyoegamia kwa mtu mwingine, unabaki kusimama wewe kama wewe na Mungu wako.

Tabia ya kuzira zira, sio tabia njema sana, uwe mwangalifu sana katika hili, kuna vitu unaweza kuzira badala ya kuonekana hupendi masihara kwenye vitu vya msingi. Ukaonekana bado mchanga wa kiroho, na kweli ukijichunguza vizuri unaona bado una ka upungufu, japo mara nyingi huwa ni ngumu kujiona kama una tabia fulani isiyopaswa kuwa nayo.

Yapo mapatano unaweza kuingia, ila baadaye ukaja kugundua hayakuwa mapatano mazuri, haya ukijitoa haitakuwa hasara kwako bali itakuwa faida kwako. Lakini yapo mapatano mazuri unaweza kuyaona hayafai, kumbe yalikuwa yanakufaa sana.

Usiogope kuungana na wenzako katika kufanya vitu vya msingi, unapokuja kugundua aliyeanzisha hilo jambo hakuwa amejipanga. Hapo unaweza kufikiri namna nyingine, ila kama anaelewa kile anafanya, usije ukakubali mtu mmoja akakuvuta nyuma.

Hayo ni mapatano ya jumla, yapo mapatano ya mtu binafsi na Mungu wake, haya pia unapaswa kuyaangalia sana unapojikuta upo njia panda. Unapoamua kusoma Neno la Mungu, hili suala halipo kimapatano ya kikundi, bali lipo kibinafsi.

Hupaswi kuacha kusoma Neno la Mungu kwa sababu ya fulani alikukwaza, vyema ukajiondoa kwenye kikundi ambacho hakina msimamo wa kile mlipatana. Ikiwa tu unaona moyoni mwako kufanya hivyo, ila kama unaona unaweza kuendelea nao, unaweza kufanya hivyo.

Usije ukaacha kusoma Neno la Mungu kwa ajili ya watu fulani, hilo ni suala linalohusu maisha yako binafsi, na wala sio suala jumuiya. Shika sana hili jambo litakusaidia katika maeneo yako mengine ya maisha yako.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081