Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa tumepata kibali cha Bwana kuweza kuiona leo. Fursa kwetu kwenda kumzalia Bwana wetu matunda yaliyo mema.

Shida haipo kwenye Neno la Mungu, shida ipo kwetu wanadamu jinsi tunavyoliona Neno la Mungu kwa kulifasiri/kulitafisiri kwa mtazamo wa mapokeo ya mila na desturi zetu, na Dini zetu. Hili linawafanya walio wengi wetu kuona wapo sahihi kutokana na mapokeo yao, kwa msukumo huo wa mapokeo ya wanadamu wanaona Roho Mtakatifu anahusika kwao.

Tunaweza kuona Neno la Mungu ni gumu sana, sio kwa sababu nyingine, ni vile tunaona tulivyofundishwa, linapingana na tunavyolisoma. Unakuta vitu viwili vinaanza kushindana ndani yako, unaanza kulinganisha jinsi ulivyopokea mapokeo ya dini yako na jinsi Neno la Mungu lenyewe linavyosema na kukuelekeza.

Kadri unavyozidi kutafakari Neno la Mungu, usipokuwa makini yale mapokeo ya wanadamu yanakuwa na nguvu zaidi kwako kuliko Neno la Mungu. Kwa sababu wakati unafundishwa siku hiyo ulikuwa makini sana, sio kufundishwa tu, na wengi wanaamini hivyo. Maana fundisho lenu ni moja na kuuliza sehemu nyingine nje na wa Dini yako unaona kama vile hatokuambia ukweli.

Wengi sana tunalihalifu Neno la Mungu kwa mapokeo yetu, hili hatuwezi kulikubali, wala hatuwezi kulielewa haraka. Kwa sababu tukitaka kutoka nje ya mapokeo yetu, tunaonekana tumeasi Dini, tutaonekana tumeanza kupotea njia sahihi tuliyoelekezwa, na hakuna aliye tayari kuonekana hivyo. Isipokuwa kwa mtu kuijua kweli na kuamua kuifuata njia ya kweli yeye binafsi.

Natamani kuanza kukupitisha taratibu kwenye Neno la Mungu uone kuhusu mapokeo yalivyo na uharibifu kwa mfia Dini, na yule aliyejaza maarifa ya wanadamu kuliko Neno la Mungu. Mtu aliyefika mahali anaona Neno la Mungu si kitu sana kupita maarifa aliyonayo ndani yake.

Rejea: Ndipo Mafarisayo na waandishi toka Yerusalemu walipomwendea Yesu wakisema, Mbona wanafunzi wako huyahalifu mapokeo ya wazee, kwa maana hawanawi mikono walapo chakula. Akajibu, akawaambia, Mbona ninyi nanyi huihalifu amri ya Mungu kwa ajili ya mapokeo yenu? Mathayo 15:1_3.

Hapa unaona ni kama mashtaka aliyopelekewa Yesu Kristo kuhusu wanafunzi wake, mafarisayo na waandishi toka Yerusalem walimwendea Yesu Kristo kumuuliza. Maana waliona inakuwaje wanafunzi wake wanaenda kinyume na vile walivyofundishwa na wazee wao.

Leo makanisani tuna watu wangapi wanaifuata iliyo kweli ya Mungu bila kuingiza mapokeo ya wazee wao, kama wale mafarisayo na waandishi toka Yerusalem? Sikuambii uanze kudharau wachungaji wako wala viongozi wako wa Dini yako, wala wazee wako Mila na Desturi zenu.

Tunahitaji kujua na kuelewa ni wanafunzi wangapi wa Yesu Kristo umepeleka mashtaka kwa Mungu wao? Kuwashtakia jinsi wanavyoenenda, jinsi wanavyovaa, jinsi wanavyokula, jinsi wanavyomtumikia Mungu wao, jinsi wanavyosali/kuomba?

Neno la Mungu linasema hivi; Ninyi mwaiacha amri ya Mungu, na kuyashika mapokeo ya wanadamu. Marko 7:8.

Je! Akina nani wanaiacha amri ya Mungu na kuyashika mapokeo ya wanadamu? Ni wale washikao mapokeo ya wazee wao, ni wale washikao mapokeo ya dini zao, ni wale washikao mapokeo ya mila na desturi zao.

Rejea: Akawaambia, Vema! Mwaikataa amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu. Marko 7:9.

Je! Ni sahihi kwetu tuliokoka na kukiri ya kwamba Yesu Kristo ni Bwana na Mwokozi wa maisha yetu kushika mapokeo ya wanadamu wasio na Yesu moyoni? Bila shaka umeona sio sahihi kushika mapokeo yanayopingana na elimu ya kiMungu, yaani kuamini mapokeo yako kuliko kuliamini Neno la Mungu.

Tena Neno la Mungu limetuweka wazi, na kutupa angalizo kuhusu mapokeo ya wanadamu, elimu zinazotupeleka kuwa mateka. Tuwe makini nazo sana, najua ni ngumu sana kutoka kwenye mapokeo au kuamini Neno la Mungu nje na mapokeo yako.

Lakini pamoja na hayo yote, sikia Neno la Mungu, sikia tahadhari kutoka ndani ya Neno la Mungu, ninaposema Neno la Mungu usilichukulie kawaida. Usione Neno la Mungu si kitu sana kuliko mapokeo yako, utakuwa unakosea sana sana.

Rejea: Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. Wakolosai 2:8.

Haleluya, sijui kama naeleweka vizuri hapa, umesoma vizuri huu mstari? Naomba urudie tena kwa umakini zaidi, unasema hivi;Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya Kristo. Wakolosai 2:8.

Natamani sana Roho Mtakatifu akufunulie huu mstari uone kwa namna ambavyo nauona kwangu, Lakini naamini Mungu ni mwaminifu sana kwetu. Kupitia Roho Mtakatifu ataenda kukusaidia kuelewa vizuri haya, tena ukisoma kwa makini huu mstari utaona kumbe zipo elimu zilizochomekwa kwa watu kinyume na fundisho la Kristo.

Mungu akusaidie uweze kuelewa haya, ili uweze kutoka kwenye kifungo cha mapokeo ya wanadamu, na ili uweze kutoka kwenye elimu ya madanganyo ya wanadamu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081