Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, siku nyingine tena mpya kabisa tumepata kibali cha kuweza kuiona. Tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu na kumrudishia sifa na utukufu, kwa uzima aliotupa.

Mazingira rafiki kwa jambo lolote lile unalolifanya, ni muhimu sana, biashara yako inahitaji mazingira mazuri ya kuweza kuvutia wateja na bidhaa unazouza. Kazi unayofanya inapaswa kuwa na mazingira rafiki katika utendaji wako wa kazi.

Ili afya yako iwe imara na ili upate usingizi mzuri, unapaswa kuwa na mazingira mazuri ya kulala, bila kulala mazingira safi na yenye hewa nzuri. Afya yako itakuwa mbovu, kwanza mazingira machafu yanaleta wadudu wabaya, watakaokudhuru afya yako.

Kanisani pia panahitaji sana mazingira yaliyo safi, mazingira rafiki ya kuweza kukufanya ujisikie salama unapomwabudu Mungu wako. Ndio maana waliojua hili, unakuta sehemu ya ibada panakuwa pametengenezewa mazingira fulani tulivu. Sio tulivu tu, na yanakuwa safi pia.

Unaona ni jinsi gani mazingira yalivyo na mchango mkubwa wa kuweza kukufanya ujisikie vizuri, mahali popote pale pasipo kuwa na mazingira mazuri. Kuna asilimia kubwa sana yale mazingira kukuondoa kwenye uwepo fulani wa kiMungu, na mazingira yakiwa mazuri yana mchango mkubwa sana ya kuvuta uwepo wa Mungu.

Kwanini nakueleza haya, unaweza kuwa msomaji mzuri sana wa Neno la Mungu, lakini ukawa unasoma tu bila kupata kile ulikusudiwa kukipata. Wenzako wanaweza kukuambia raha wanayoipata wakati wanasoma Neno la Mungu, lakini ukirudi kwako unaona kabisa hujawahi kuona raha yeyote tangu uanze kusoma Neno la Mungu.

Ikiwa unasoma Neno la Mungu wakati mwingine unatoka bila kuelewa kitu chochote, hupaswi kupeleka moja kwa moja Neno la Mungu limekuwa gumu siku hiyo. Unachopaswa kufanya ni kutengeneza mazingira mazuri, mazingira yatakayokufanya akili yako itulie sehemu moja.

Ukishaweka mazingira vizuri, hata usomaji wako wa Neno la Mungu utakaa vizuri, utaona utofauti wa awali na sasa. Shida ni kwamba unakuta mtu anasoma Neno la Mungu huku anaangalia taarifa ya habari, anachati na simu, yupo na marafiki zake wanaongelea habari zingine tofauti kabisa. Japo unaweza kutoka kwenye mazingira yale kifikra ukiwa mwili wako upo pale pale, ila ni wachache sana wanaweza kufanya hivyo.

Unapofika muda uliojiwekea wa kusoma Neno la Mungu, tengeneza mazingira rafiki ya usomaji wako, kama ulikuwa na marafiki unaona mazungumzo yao yanakuondoa kwenye utulivu. Vizuri ukajitenga nao kwa muda kuliko kung’ang’ana nao alafu ukashindwa kupokea ujumbe wa Mungu kupitia Neno lake.

Haijalishi upo kwenye gari la abiria, ukiamua kutengeneza mazingira ya utulivu, hata zile kelele za abiria wenzako hutozisikia kabisa, si umewahi kuona mpo na watu. Katikati ya mazungumzo unakuta akili yako imehamia sehemu nyingine kabisa, unakuwa husikii mazungumzo yao tena, hadi pale unakuja kushtuliwa.

Ukiona huwezi kujenga mazingira ya utulivu ukiwa kwenye gari la abiria, vyema ukasubiri ushuke kwanza, maana nia ya wewe kusoma Neno la Mungu ni ili upate kitu cha kuondoka nacho, cha kuweza kukusaidia katika maisha yako ya wokovu.

Hatusomi Neno la Mungu kutimiza wajibu, tunasoma Neno la Mungu kusikia Mungu anasema nini juu ya maisha yetu kupitia Neno lake. Hili ndio lengo kuu ya kujifunza Neno la Mungu, hatusomi ilimradi tunasoma, kipo kitu tunakipata kupitia usomaji wetu.

Ukijikuta siku yeyote ile unasoma Neno la Mungu alafu unajiona huelewi, jambo la kufanyia kazi ni kutafuta utulivu kwenye mawazo/akili yako. Na kuweka mazingira rafiki ya wewe kufurahia usomaji wako wa Neno la Mungu, mazingira ambayo yatakufanya ujihisi vizuri wakati unasoma Neno la Mungu.

Kama huwezi kutengeneza mazingira mazuri ya usomaji wako wa Neno la Mungu, utabaki kusikia simulizi za wengine wanavyofurahia Neno la Mungu. Ila kwako utaendelea kuona gumu na hupati chochote cha kuweza kukusaidia katika maisha yako ya wokovu.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081