Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai.

Utakutana na mtu anaziimba kweli amri za Mungu, kiasi kwamba unasema amezaliwa nazo, kumbe ameshika kwenye kichwa chake. Ambapo anaweza kukutajia amri ya kwanza hadi ya kumi, hizi zote anazijua vizuri sana.

Pamoja na mtu huyu kuzishika amri zote, utamshangaa bado anazivunja zile amri, anajua kabisa Mungu anakataza kuzini, lakini utamkuta ni fundi mzuri tu wa mambo hayo. Anajua kabisa kuua ni kosa, ndio utamkuta wa kwanza kutoa mimba, anajua kabisa kuiba ni vibaya, lakini anakuwa anakabiliwa na hiyo changamoto wizi.

Unaweza kushindwa kuelewa inakuwaje mtu ameokoka, lakini bado anasubuliwa na tatizo la kuzini ovyo na wake/waume za watu. Sio kwamba huyu mtu hajui anachofanya, anajua vizuri sana, ila ndani yake kuna upungufu wa kitu ambacho kingemsaidia kutofanya mabaya.

Unaweza kuomba sana na unaweza kuombewa sana, ila ukajikuta bado ni mzinzi, muuaji, mwizi, na kutamani vya watu, unapaswa kufahamu sio kila kitu ni cha kuomba/kuombewa. Mambo mengine yanahitaji uwe na maarifa, ukiwa na maarifa sahihi, huhitaji kuteswa na kitu/jambo lolote wakati unayo njia sahihi ya kuliepuka.

Haya yote Neno la Mungu linatufungua ufahamu wetu siku ya leo, tunapata kujua utimilifu wa sheria/amri zote za Mungu, upo kwenye upendo. Ukimpenda Mungu kisawasawa, utakuwa msomaji wa Neno lake, utakuwa mwombaji mzuri asiye wa kulazimishwa, na wala hutaweza kumchukia jirani yako.

Ukimpenda Mungu, hutoweza kuzini, wala huo ujasiri hutokuwa nao kabisa, sio kwamba ni mwoga sana la hasha, ile hofu ya Mungu iliyo ndani yako. Ndio itakayokusaidia kuona vibaya kutenda lililo baya mbele za Mungu.

Ukiona kaka/dada yeyote ametulia, hana kona kona mbaya, usifikiri ni kwa ujanja wake, ipo nguvu ndani yake, nguvu iliyojengwa na pendo la Mungu ndani yake. Labda utaanza kujiuliza mbona nampenda sana Mungu ila bado nasumbuliwa na hayo yote? Sio kweli, upo nusu nusu kwa Mungu ndio maana yanakushinda hayo.

Rejea: Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria. Maana kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani; na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi pendo ndilo utimilifu wa sheria. RUM. 13:8‭-‬10 SUV.

Haleluya, sijui kama umesoma vizuri hiyo mistari niliyokuwekea hapo, kumbe kushindwa kuzifuata sheria, ni ukosefu wa pendo la Mungu ndani yetu. Kwa maana nyingine ni kukosa maarifa sahihi ya Neno la Mungu, maana yapo mambo maovu tunafanya kwa sababu ya uchanga wa kiroho.

Mungu ni pendo, tena waliozaliwa na Mungu, yaani waliozaliwa mara ya pili, wana pendo la kweli ndani yao. Ukijiona ndani yako huwezi kumpenda mwenzako, ujue bado hujamjua Mungu wako vizuri, bado unaopungufu mkubwa ndani yako.

Tumeagizwa kupendana, tena kupendana kweli kweli, ikiwa mwanaume unashindwa kumpenda mke wako, elewa hujamjua Mungu vizuri. Na mwanamke vivyo hivyo, ukishindwa kumtii mume wako, hutokuwa na upendo kwake. Kukosa upendo kwa mume wako, utakuwa hujamjua Mungu wako, na kama ulikuwa unamjua, utakuwa umerudi nyuma.

Rejea: Wapenzi, na mpendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo.
1 YOH. 4:7‭-‬8 SUV.

Je! Ipo haja tena ya kusukumwa kumpenda ndugu/jirani/jamaa yako? Hakuna haja ya kusukumwa tena, anayemjua Mungu wake vizuri, anajua huo ni wajibu wake kufanya hivyo. Mungu ni pendo, ukiwa na Yesu Kristo ndani yako, unalo pendo la kweli ndani yako.

Siri hizi zote utazijua ukiwa msomaji mzuri wa Neno la Kristo, usiache kusoma Neno.

Mungu akubariki sana.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081