Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo aliye hai, karibu sana tujifunze pamoja.
Namna ya kufikiri mambo, namna ya kuchukulia mambo, na namna ya kuyabeba mambo moyoni, haipaswi kufanana kabisa na kabla hujaanza kujifunza Neno la Mungu. Na haipaswi kulingana kabisa na mtu asiyemjua Mungu kupitia Neno lake takatifu.
Utofauti wenu lazima uwepo, utofauti wako lazima uwepo kadri unavyozidi kujifunza Neno la Mungu, ndivyo unavyozidi kusogea hatua zingine zaidi mbele. Ikiwa utaonekana upo pale pale kila siku, lazima tuanze kupata mashaka na wewe.
Mfano mzuri ni mimi, kabla sijaanza kujifunza Neno la Mungu kwa njia ya kusoma, nilikuwa na upungufu mwingi sana, ambao upungufu huo tunauita uchanga wa kiroho. Pamoja na nilikuwa nimeokoka, kuna maeneo nilikuwa siwezi kuwa jasiri, kwa sababu nilijiona nina mapungufu, yaani nilikuwa naona nitakuja kukosea nikifanya.
Sikuwa sahihi kabisa kuwaza hivyo, ila kwa sababu sikujua Neno la Mungu linasemaje kuhusu kusema nini au kujibu nini mbele za watu, nilibaki hivyo. Yapo mambo mengi nakuwa nahisi nikifanya au nikimjibu mtu nitakuwa nimekosea, hata kama nilikuwa sahihi, najiona labda nitakuwa nimekosea. Hii ni kutokana na kukosa uhakika wa maandiko matakatifu.
Nilivyoamua kuanza rasmi kujifunza Neno la Mungu bila kukwamakwama, nilianza kukutana na changamoto nyingine tena ya kushindwa kuelewa vizuri kile nasoma. Muda mwingine naona nakutana na mambo mageni kabisa, ambayo yananifanya nishindwe kuelewa vizuri.
Sikuridhika na hali hiyo, nikawa namwomba Roho Mtakatifu anisaidie kuelewa kile nasoma, taratibu kadri nilivyozidi kusoma Neno la Mungu nilianza kuona utofauti fulani mkubwa sana ndani yangu. Ujasiri ulizidi kuongezeka siku hadi siku, kuona Neno linasema nini juu ya maisha yangu, nikaanza kuliona kwa jicho la tofauti kabisa.
Kitu ambacho nilijifunza kipindi hicho, nilikuwa naona mambo mageni kwa sababu sikuwahi kuyasoma au kuyasikia kwenye masikio yangu. Labda kwa ile mistari iliyozoeleka na kila mtu, maana kuna mistari haipiti muda mrefu bila kuisikia mtu akiitaja. Mistari kama hiyo ndio unakuta kila mtu anaitumia kuhubiri/kufundisha, sasa ile isiyofahamika ndio ilikuwa inanipa wakati mgumu.
Bila shaka umeanza kuelewa utofauti ninaouzungumzaia hapa, pamoja na kutoka kwenye eneo ambalo kwangu lilikuwa ni changamoto, bado kuna hatua natamani kuiona katika usomaji wangu wa Neno la Mungu. Vile nilivyokuwa jana, sitamani kuwa leo hivyo, natamani kusogea hatua nyingine mbele tofauti kabisa na wakati wowote ule nyuma.
Namna ya kutafakari kwangu Neno la Mungu, natamani kuona utofauti kila iitwapo leo, utofauti wangu unapaswa kuonekana na yule asiyesoma Neno la Mungu. Hata kama ameokoka, lazima tuwe tofauti kwa sababu jinsi anavyobeba mambo, ubebaji wake hauwezi kufanana na mimi kabisa.
Huku ndipo tunasema kukua kiroho, sio miaka yote tangu uanze kusoma Neno la Mungu, bado upo vile vile, namna ya kutafakari kwako Neno la Mungu kupo vile vile, namna ya kuchukulia mambo na kuyabeba moyoni, bado kupo vile vile. Namna unavyofikiri na kuzungumza kuhusu Mungu, huna tofauti kabisa na yule asiyesoma Neno la Mungu.
Fika mahali jifanyie tathimini, usifurahie tu kusoma Neno la Mungu, na wakati hakuna mabadiliko yeyote yanayoonekana katika maisha yako. Neno la Mungu likusaidie kutoka hatua moja uliyokuwepo na kusogea hatua nyingine mbele zaidi, ambayo hukuwa nayo kabisa hapo awali.
Sio unakazana kila siku kusoma Neno la Mungu, alafu bado unakimbizana na imani potofu, yaani unakuwa huna tofauti kabisa na yule asiyejua Neno la Mungu. Hata mahali unaposali kila siku, uanze kujua upo mahali sahihi ama la, bila kuambiwa na mtu yeyote ulipo ni mahali si sahihi au ulipo ni mahali sahihi.
Itakuwa haina maana yeyote unasoma Neno la Mungu kila siku, alafu mahali ambapo sio sahihi wewe kusali, na wewe unakuwepo humo, tofauti yako na asiyelijua Neno la Mungu inakuwa hakuna. Ingekuwepo tungeanza kuona matunda yake kwa nje, tena vitendo vyako tungeanza kuviona vikitenda kazi kwa kasi kubwa mno.
Anza leo kutamani kusogea hatua uliyopo na kwenda hatua nyingine mbele, kujua unapaswa kwenda hatua nyingine mbele, napo inasaidia kutoridhika hatua uliyonayo. Itakufanya uanze kujisukuma kwenda mbele zaidi, kiu yako inaweza kukupa hatua nyingine tofauti kabisa na jana.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081