Yapo mambo mengi sana, yanatuchelewesha sana, na tunajikuta tumetumia muda wetu mwingi kwa mambo yasiyofaa. Tukija kusema tufanye yale yanayotufaa kufanya tunakuwa hatuna tena nafasi ya kufanya hivyo. Kwa sababu muda mwingi tuliupoteza kwa mambo madogo madogo, ambayo ki kawaida yalionekana hayali sana muda.

Tunaweza kusingizia kila siku, au tunaweza kulalamika sana kila siku, kuwa hatuna muda wa kutosha wa kusoma Neno la Mungu na kulifakari. Ukija katika uhalisia kabisa, unaona kuna mahali unatumia muda wako mwingi kwa mambo ambayo ki msingi hayakuwa na sababu.

Yapo majukumu kweli mtu anakuwa nayo, ila ndani ya hayo majukumu mtu anakuwa anatumia muda wake vibaya kwa mambo madogo madogo. Ambapo kwa kawaida anaweza kuona haina madhara makubwa kwake, kumbe hayo mambo madogo madogo yanachukua muda wake mwingi sana kupotea.

Muda unapotea kwa mambo mengine nje na majukumu yake, anakuja kufikiri kilichopoteza muda wake ni kubanwa na majukumu mengi ya siku, kumbe kubanwa kwake ni asilimia ndogo sana. Tofauti na ule muda mwingi anaouacha umwagike bila sababu za msingi, pamoja na ukweli kwamba anakuwa amebanwa sana, ila kuna wakati anakuwa na muda wa kutosha.

Kwanini nasema hivi? Mtu anapokuwa na majukumu mengi, anapopata muda wa kutulia haendi moja kwa moja kusoma Neno la Mungu. Anaanza kupitia kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii, anapita kwanza kwenye makundi yake ya whatsApp ya kuchati. Anakuja kushtuka tayari muda umeenda sana, bila aibu anaunganisha na majukumu yake ya siku kusema alikuwa ametingwa sana.

Kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kuanza kufanya vitu vya msingi ndipo aje ahamie kwenye kuzunguka huku na kule kwenye makundi yake ya whatsApp na mitandao mbalimbali ya kijamii. Hili huwa hatulijui kama linakula muda wetu, na kama tunalijua huwa hatukubali haraka kama linatupotezea muda wetu.

Vizuri kuliangalia hili kwa umakini sana, usisingizie kazi zimekuchosha sana, kumbe kinachokuchosha sio kazi, ni hiyo mizunguko yako isiyo na sababu yeyote kuifanya kwa wakati huo. Jifunze kufanya ya muhimu kwanza, kuchati na kuzunguka kwenye mitandao ya kijamii, kufanye ni jambo la mwisho kabisa baada ya kumaliza ratiba zako za muhimu.

Inaweza kukuwia ngumu katika hili, ila ukiona upo kwenye magroup yanayotumia muda mwingi kuongelea mambo yasiyofaa na hayana mafundisho yeyote kwako. Vyema ukajiondoa, ukishindwa kufanya hivyo ujue bado haupo siriaz na usomaji wako wa Neno la Mungu.

Itashangaza jamii kila ujumbe unaorushwa na marafiki zako huko facebook, twitter na instagram, lazima utoe maoni yako au lazima u like. Ila ukija kwenye Neno la Mungu unakuwa hauna muda wa kulisoma, huenda hujui kama una shida.

Fanya mambo yako kwa mpangilio unaofaa, kila jambo lifanye kwa muda wake sahihi, katika yote kipaumbele chako kiwe kwenye Neno la Mungu. Baada ya ratiba zako zote za siku, hakikisha ratiba ya kusoma Neno la Mungu haisahauliki kamwe kwako.

Ukiona unafanya mambo yote hadi muda wa kulala unafika, ndio unakumbuka hukusoma Neno la Mungu, ujue hili jambo bado halijakukaa vizuri moyoni mwako. Likishakukaa vizuri moyoni mwako, utaona mwenyewe ukikumbuka kila wakati.

Usisingizie unakuwa unabwa sana na majukumu mengi, hebu pata muda uangalie ratiba yako ya siku, kweli inakuwa imebanana kiasi kwamba huwezi kupata hata nusu saa ya kusoma na kulifakari Neno la Mungu? Utaona kuna mahali huwa unaacha muda wako umwagike bila sababu za msingi.

Mungu akubariki sana kwa muda wako.

Facebook: Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081