Vizuri kujiuliza hili swali mapema, itakufanya ujenge sura fulani ndani yako, itakayokusaidia siku haupo kwenye mazingira uliyozoea, kuendelea na ratiba zako kama kawaida. Mazingira yana mchango mkubwa sana kukuondoa kwenye kile ulichokuwa unapenda kufanya, na vile vile mazingira yanaweza kukuvuta kufanya kitu ambacho hukuwa ukikifanya hapo awali.
Wengi wetu huwa tunashindwa kuelewa hili, ndio maana unakuta mtu alikuwa na bidii sana alipokuwa mahali fulani. Baada ya kuondoka mazingira hayo, bidii ya mtu yule iliishia hapo, anakuwa hana nafasi tena ya kufanya kile alichokuwa anafanya. Anakuwa mzito kufanya kile alipaswa kufanya, sio kwamba anakuwa amebanwa sana, la hasha.
Hata ukimuuliza shida nini, anaweza asiwe na majibu mazuri kuhusu kile kimemkwamisha kufanya, pamoja na kutokuwa na majibu ya uhakika, hiyo haimwondolei uvivu alionao. Kinachobaki kwake ni kuendelea kuhangaika na kujipa sababu nyingi zisizo na mashiko yeyote.
Labda nikutolee mfano huu utanielewa vizuri zaidi, umewahi kuona mtoto akiwa kwa watu, yaani nje na kwao, anakula vizuri sana mpaka unashangaa. Ila akiwa nyumbani kwao anakataa kabisa kula, hata umlazimishe vipi kula hataki, na hata akila hali vizuri ukapenda, hili wamama wanaolea watoto wanalielewa vizuri sana.
Unafikiri ni nini inasababisha hivyo, chakula ni kile kile tena cha nyumbani kwao kinaweza kuwa kizuri zaidi, ila hataki kula, akiwa kwa watu ndio anapata hamu ya kula. Au umewahi kuona ukiwepo karibu na mtoto wako hataki kula hadi unatumia fimbo kumlisha. Ila ukiwa mbali naye anakula vizuri tu mpaka unashangaa ni yeye au mwingine.
Unaweza kuona kuna mazingira fulani hivi ambayo ukiwepo mambo yanaenda vizuri, sio kwamba ni mtazamo hasi, sio kwamba ulipokuwepo mwanzo ulikuwa na nafasi ya kutosha sana kufanya hayo mambo na ulipo sasa hauna kabisa muda wa kufanya hayo. Inakuwepo hali fulani tu ya uzito, na usipokuwa makini unaweza kuacha kabisa kile ulikuwa unafanya.
Hili limewakumba wengi sana katika usomaji wao wa Neno la Mungu, wakati wapo kwenye mazingira fulani hivi walikuwa wasomaji wazuri sana wa Neno la Mungu. Tena mazingira hayo yalikuwa yanawabana sana mpaka muda mwingine wanashindwa kufanya kile wamejiwekea kukifanya kila siku, ila pamoja na kubanwa huko walikuwa wanasoma Neno la Mungu.
Mazingira ya mwanzo hukuwa na uhuru wowote kufanya mambo yako vizuri, ila pamoja na kukosa uhuru, ulikuwa unafanya vizuri sana. Umeenda mazingira yenye uhuru mkubwa wa kufanya hayo hayo uliyokuwa unafanya, badala ya kufanya vizuri zaidi, unarudi nyuma zaidi, tena sio nyuma tu unaacha kabisa.
Nikisema mazingira labda unaweza kupata shida kuelewa, ngoja nikupe mfano huu; wakati upo shule/chuo ulikuwa unapagiliana mambo yako vizuri sana, siku ilikuwa haipiti bila kusoma Neno la Mungu. Umekuja likizo au umemaliza kabisa shule/chuo, ukifikiri hapa ndio naenda kuwa na uhuru mwingi wa kusoma Neno la Mungu, unashangaa badala yake unakuwa mzito kusoma.
Wakati upo kwenye mafunzo ya jeshi ulikuwa unapagilia ratiba zako vizuri sana, pamoja na ulikuwa umebanwa sana, pamoja na ulikuwa unachoka sana. Lakini ulikuwa huachi kumpa Mungu wako nafasi hata kwa dakika chache, katika kulisoma Neno lake na kulifakari. Umemaliza mafunzo sasa, na muda unao wa kutosha kufanya mambo yako kwa uhuru, unashangaa unakuwa mzito kufanya.
Ukifuatilia hiyo mifano, unaweza kuona kuna upungufu wa jambo fulani hapo, hasa hii mifano miwili ya mwisho, wa shule/chuo na mafunzo ya jeshi. Japo ipo mifano mingi unayoweza kutolea, na huenda mingine umeikumbuka baada ya kusoma hii mifano niliyokutolea.
Ninachotaka kukueleza hapa ni nini hasa, unapaswa kujitengenezea nidhamu isiyotazama mazingira, nidhamu itakuyokufanya ujisukume kufanya bila kujipa sababu zisizo na msingi wa kushindwa kufanya. Nidhamu hii ukiitengeneza ndani yako, haijalishi utakuwa mazingira gani nje na uliyoyazoea, utaendelea na ratiba yako ile ile. Hata kama kwa kujibana sana, hata kama kwa kujilazimisha sana, utahakikisha unafanya kile umejipangia kukifanya kwenye maisha yako yote.
Labda unajiuliza nitawezaje kuitengeneza hiyo nidhamu unayoisema, ni wewe kukaa chini kujiwekea utaratibu usioweza kuukiuka/kuuvunja kirahisi. Maana wewe unajijua vizuri kuliko mtu mwingine yeyote, madhaifu yako unayajua, unapaswa kujiuliza uliwezaje kufanya ukiwa umebanwa sana, na wakati hujabanwa unashindwa kufanya.
Ukishapata majibu ya hayo, hutokuwa msomaji wa Neno la Mungu kwa msimu fulani unapotea, hili litakuwa ni zoezi lako la kila siku. Maana ni jambo ambalo lipo moyoni mwako, haijalishi utakuwa wapi utasikia kukumbushwa kutekeleza wajibu wako. Hutoweza kutulia mpaka umesoma Neno la Mungu, nakueleza kitu ninachokiishi mimi siku zote za maisha yangu.
Usije ukaanza kusema hujui tu, najua ninachokueleza, kwa sababu nakiishi, ni vile tu ukiamua kujiwekea nidhamu ya kusoma Neno la Mungu inawezekana kabisa. Hakuna mazingira yatakuzuia kusoma Neno la Mungu, muda ambao ulipaswa kuutumia kupumzika, ndio unakuwa muda wako mzuri wa kusoma Neno la Mungu.
Bila shaka kuanzia sasa hutosumbuliwa tena na mazingira yeyote, maana umeshajua namna ya kufanya, ili uweze kuepuka hali yeyote itakayokujia kutaka kukuzuia usisome Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana kwa muda wako.
Facebook: Chapeo Ya Wokovu
Website: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081