Huwa tunajipoteza wenyewe bila kujua, pale tunapofikiri tumejua kila kitu kwa kujifunza sana vya kutosha yale ambayo tulikuwa hatuyajui, tunapofika wakati tukaridhika na yale tuliyoyajua. Tunasahau kwamba, tuliyoyajua ni sehemu ndogo sana kati ya mengi ambayo tulipaswa kuendelea kuyajua zaidi kadri tunavyozidi kujifunza.
Elimu haina mwisho, elewa hilo siku zote, unapotaka kuendelea kuwa vizuri kwenye jambo lolote lile, hupaswi kuchoka kujifunza zaidi, unapofika mahali ukaacha kujifunza. Uwe na uhakika umekubali kushindwa, hata kama unajiona upo vizuri sana, unapaswa kuendelea kujifunza kila siku.
Kujifunza jambo lolote lile zuri, lenye manufaa kwako, sio lazima ukakae darasani, vipo vitabu vingi vyenye maarifa sahihi yanayokusaidia kuwa imara zaidi kwa kile unachokifanya. Huna kisingizio chochote katika hili, labda uwe hujui kusoma, pia ipo njia nyingine ya kusikiliza vitabu vilivyosomwa tayari.
Leo hii mtu akisoma biblia akapata bahati ya kuimaliza yote, anaona amemaliza kila kitu, kitu ambacho ni hatari sana kwake. Amesahau yeye ni mwanafunzi wa Yesu Kristo, na sifa ya mwanafunzi ni kujifunza.
Hii haipo kwenye kujifunza tu, hata unapokuwa umeokoka, hupaswi kusema sasa nimeokoka imetosha, unapaswa kujilinda sana usije ukarudi nyuma ukaikosa mbingu. Si umeona watu wengi walijiona wamesimama vizuri katika wokovu, ila mwisho wake waliishia kumwasi Mungu wao.
Ndio maana maandiko matakatifu yalitupa tahadhari mapema, ili tusifika mahali tukajisahau, tusijiona tupo vizuri, hata pale tunapotoka nje ya njia ya Yesu Kristo, watumishi wanapotaka kuturejesha huwa tunakuwa wagumu kuwaelewa haraka.
Rejea: Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke. 1 KOR. 10:12 SUV.
Unapokuwa na mahusiano mazuri na Mungu wako, utakuwa unajua kabisa moyoni mwako, unapokuwa huna mahusiano mazuri na Mungu wako, unakuwa unajua kabisa moyoni mwako. Sasa unapojiona umesimama vizuri na Mungu wako, uwe mwangalifu sana usije ukaanguka.
Wengi sana wameanguka dhambini kwa uzembe wao wa kufikiri wamesimama na Mungu, kujidhania kwao wamesimama, wamekuwa wanapuuza vitu vidogo vidogo vinavyoweza kuwapelekea kuanguka dhambini.
Ndivyo ilivyo katika kujifunza, unapofika mahali ukajiona kabisa kuna baadhi ya vitu umeshavijua na havikupi tena shida. Usiache kujifunza, bado vipo vingine vingi huvijui kabisa, kadri unavyozidi kujifunza ndivyo unavyozidi kujua zaidi.
Nakueleza hili uweze kujipanga vizuri katika usomaji wako wa Neno la Mungu, haijalishi umepita kwenye chuo cha Biblia, kama hutokuwa na muda wa kujifunza zaidi Neno la Mungu. Kwa kufikiri umemaliza kila kitu, nakueleza ukweli, utakuwa umeamua mwenyewe kuwa kama mtu asiyejua kitu.
Unapokuwa unasoma Neno la Mungu, kuna mahali utasoma hutolewa papo hapo, ila ukija kurudia kusoma tena kwa wakati mwingine utaona umekutana na jambo jipya kabisa. Kumbe sio jambo jipya, huenda wakati huo unasoma huo mstari hukukugusa moja kwa moja, sasa wakati umerudia tena unaona umekugusa moja kwa moja maisha yako.
Si umewahi kukutana na mwalimu anafundisha somo linalogusa andiko lile unalolijua kila siku, ila jinsi alivyofundisha, unaliona hilo andiko kama vile ni jipya kabisa. Unaweza kuliangalia mara mbili mbili usiamini kama ni kweli, ila ukweli utabaki vile vile umewahi kulisoma sio kulisoma tu, umekariri na kichwani.
Unapoona hali inakujia ya kujiona umejua kila kitu, na hupaswi kujifunza tena, jiondoe haraka kwenye hali hiyo. Kusoma kwako Neno la Mungu, iwe maisha yako yote mpaka unaondoka hapa duniani. Usijaribu kuingiza sababu yeyote ya kuacha kusoma Neno la Mungu, lione Neno la Mungu kwako ni jipya kila siku.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Website: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081