Ukijitoa kwa ajili ya kuwaelimisha watu wengine waweze kuelewa jambo fulani unalotamani waelewe, usifikiri itakuwa kazi rahisi. Utapaswa kuwa mvumilivu sana, tena uvumilivu wenye Mungu ndani yako, maana wapo watu hawatakuelewa haraka. Unaweza kutoa elimu sana, kumbe wakati unaitoa hiyo elimu alikuwa anapingana na unayosema.

Anachokielewa yeye na unachomweleza wewe, ni vitu viwili tofauti vinapingana ndani yake, maarifa aliyonayo yeye yanapishana mbali sana na maarifa yako sahihi unayompa. Inaweza kukuumiza sana unapoona unatoa elimu nzuri alafu watu wakawa hawakuelewi, badala yake wakawa wanaendelea kushikilia yale wanayojua wao ni sahihi kwao.

Unapokutana na changamoto kama hii, isikutoe kwenye kile kizuri ulianza nacho kukifanya, elimu mpya au maarifa yeyote mapya unayompa mtu. Yanaweza yasieleweke kwa haraka sana, yatachukua muda mrefu sana kubadilisha kile alichokuwa amekijaza mtu moyoni mwake.

Unapohubiri ukaona mtu/watu wakaamua kuokoka, sio mara zote wanaokoka wanakuwa wamesikia kwa mara ya kwanza habari za Yesu Kristo. Mara nyingi wanakuwa wameshahubiriwa sana huko nyuma, ila walikuwa bado wanasita kuchukua maamzi, siku umemhubiri wewe, wakaona kile wamesikia sana siku za nyuma, na hicho unachowaeleza ni bora wachukue hatua.

Kubadilika kwa mtu inachukua muda sana, hasa unapozaliwa ukakuta wanafanya mambo yasiyompendeza Mungu na wewe ukaunga humo humo kufanya yale mabaya. Bila kujua hicho unachofanya ni chukizo mbele za Mungu, siku anatokea mtu akakuambia ndugu hili jambo unalofanya halifai mbele za Mungu. Uwe na uhakika utamkatalia huyo mtu anayekueleza habari tofauti za kukuzuia usiendelee kufanya jambo, ambalo tangu utoto wako umekua ukilifanya.

Wakati mwingine umeona Mungu akikufanyia mambo makuu kupitia hayo unayoamini na kuyatenda, kumbe hayo mambo unayoona Mungu anakutendea. Sio kweli Mungu amekutendea, ila imani yako inakusukuma kuamini Mungu ametenda mambo makuu maishani mwako, bila kujua mafanikio mengine yanaweza kuwa ni juhudi zako binafsi ulizofanya kwa kutumia uwezo uliozaliwa nao.

Ndivyo ilivyo hata kwenye kujifunza kwako Neno la Mungu, sio kila andiko takatifu utaweza kulielewa pale pale. Mengine kadri unavyozidi kujifunza hatua kwa hatua, utaona ukizidi kufunguka taratibu ufahamu wako kadri unavyozidi kutenga muda wa kusoma Neno la Mungu.

Wengi wanashindwa kuelewa hili, anaanza kusoma Neno la Mungu leo, anakutana na changamoto kadhaa kwenye usomaji wake anaona njia rahisi ni kuacha, na kuendelea na utaratibu wake wa zamani. Ambapo ni kosa kuacha, angeendelea kujifunza Neno la Mungu kila siku, angeanza kuona mabadiliko kwenye maisha yake.

Uchanga wa kiroho hautoki siku moja, usijidanganye kwa kusoma Neno la Mungu miezi 6 ukaona umeuaga uchanga wa kiroho, usisome neno la Mungu mwaka mmoja ukaona umetoka kwenye uchanga wa kiroho. Bado kuna hatua zaidi mbele, ukitaka kujua hili vizuri angalia kiwango chako cha uelewa ulivyokuwa mwaka jana. Kama ulianza kusoma Neno la Mungu mwaka jana, na sasa unaendelea mwaka huu, utakuwa unaona kuna vitu fulani vimebadilika sana tofauti na mwaka jana.

Unapofika mahali ukaona kuchoka, ukaona hakuna unachofanya, ukaona hakuna unachoingiza kichwani, omba sana Mungu akufungue ufahamu wako. Utaona kipo kitu umekipata na unaendelea kuvipata vingine vingi sana, sema huoni hayo yote, unachoona wewe ni madhaifu tu. Ambacho ni kitu cha hatari sana kwako, hasa kwa wewe unayeanza kujifunza utaratibu mpya ambao hukuwa nao hapo awali.

Haijalishi unaelewa kwa kiwango cha chini sana kwenye usomaji wako, endelea kusoma zaidi Neno la Mungu, bila kuangalia mazingira uliyonayo sasa. Baadaye utaanza kuona matunda yake, haya matunda utayaona kwa kuwa mvumilivu sana.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

Tovuti: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081