Ukifanya jambo lolote ambalo wengi hawajazoea kulifanya, tegemea vipingamizi vingi vitatokea kwako, vinaweza vinakawa vipingamizi vya watu. Na vinaweza kuwa vipingamizi vya ndani yako mwenyewe, utakuwa unaona kelele za kuacha kufanya ni nyingi, kuliko za kufanya.
Usitegemee kuanza kufanya jambo ambalo hukuwa ukilifanya, alafu ukalifanya kwa amani bila kukutana na vikwazo, usitegemee utaukwepa upinzani mkubwa kwa hilo unalofanya. Lazima ukutane na upinzani/vipingamizi vikali kwa hilo uliloamua kulifanya.
Umekua mazingira ambayo unaona watu wanazibeba Biblia zao siku za ibada, ila kumsikia au kumwona mtu akisema ana ratiba ya kila siku kusoma Neno la Mungu. Hujawahi kuona hilo jambo likitendeka zaidi sana wengi wanaongea tu kuonyesha kulipenda Neno la Mungu, lakini hakuna anayeweka huo upendo wa Neno la Mungu katika matendo yake.
Tegemea unapoanza kusoma Neno la Mungu, utakutana na upinzani mkubwa sana, tena upinzani wenyewe utaanzia kwako mwenyewe, baadaye kwa marafiki zako au washirika wenzeko. Unaweza kumweleza rafiki/mshirika mwenzako habari ya kusoma Neno la Mungu, akakueleza maneno magumu ya kukuvunja moyo.
Unaweza kumwambia ndugu yako kabisa kabla ya kulala iwepo ratiba ya kusoma Neno la Mungu, anaweza kukuunga mkono siku ya kwanza, ila kadri siku zitakavyozidi kwenda mbele. Utajikuta umebaki peke yako, kama hukuwa umejipanga, utajikuta na wewe umeacha kusoma Neno la Mungu.
Lingine ambalo linaweza kukuvunja moyo wa kushindwa kuendelea kusoma Neno la Mungu, ni kuwa na marafiki wengi wasiopenda msimamo wako wa kusoma Neno la Mungu. Kama huna kundi kubwa linalokuzunguka la kusoma Neno la Mungu, kama huna watu wa kukuhimiza kusoma Neno la Mungu pale unapojikuta umechoka. Ni rahisi sana kwako kuishia njiani, tena ni rahisi kutiwa moyo wa kutoendelea kujifunza na wale wasiopenda kusoma Neno la Mungu.
Elewa kwamba umejiingiza kwenye jambo ambalo halipendwi na wakristo wengi, wanaonyesha kulipenda mdomoni, lakini ukija kwenye matendo hakuna anayethubutu kusoma Neno la Mungu. Na kama amewahi kuthubutu kusoma Neno la Mungu, hakuweza kuendelea, aliishiaga njiani siku nyingi.
Sababu za aliyewahi kusoma Neno la Mungu, akafika mahali akaachilia njiani, zina nguvu sana ya kukufanya ushindwe kuanza au kuendelea kusoma Neno la Mungu. Kama ulikuwa unasoma, na kama ulitaka kuanza kusoma Neno la Mungu, utajikuta unaona jambo hilo ni gumu sana kwako.
Makundi yana nguvu kubwa sana, ndio maana ni muhimu sana kuwa na makundi ya marafiki wazuri, hasa kwa kile unachopenda kukifanya. Ndio maana Chapeo Ya Wokovu wasap group, tumejikusanya pamoja kwa ajili ya kusoma Neno la Mungu, kuna wakati utakuwa unapita kwenye changamoto ngumu inayokufanya ushindwe kusoma Neno la Mungu. Lakini kupitia marafiki wazuri wanaokuzunguka wenye nia moja, unajikuta unatiwa moyo wa kuendelea mbele bila kujalisha changamoto unayopitia.
Utasema wewe umekomaa kiroho, marafiki hawawezi kukuvunja moyo kwa kile unachofanya, utakuwa hujui maandiko matakatifu. Marafiki wabaya wana mchango mkubwa sana kukuharibu au kukujenga, hata kama hawataonyesha kukuharibu moja kwa moja, mazungumzo yao na vile unavyoambatana nao kwa muda mwingi. Utajikuta kuna maneno hasi wamekupandikiza kwako.
Rejea: Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema. 1 Wakorintho 15:33.
Asikudanganye mtu yeyote, marafiki wenye tabia mabaya, wenye mazungumzo mabaya, watakuharibu tu, ukubalia ukatae, utaharibiwa tu. Ndio maana kama mzazi hupaswi kuruhusu mtoto wako kuwa na marafiki ambao tabia zao sio nzuri, unapaswa kujua marafiki wa mwanao ni wa namna gani, hili ni muhimu sana.
Unaweza kuwa unasoma ujumbe huu, alafu ulifika mahali ukaona uache kusoma Neno la Mungu baada ya kukutana na maneno ya kukuvunja moyo. Usikubali kuacha kusoma Neno la Mungu, cha kufanya ni kuangalia vitu gani vinakuja kukuvunja moyo, mazingira gani huwa yanachangia wewe uache kusoma Neno la Mungu. Ukishapata chanzo chake, shughulikia hicho chanzo, hiyo ndio itakuwa pona yako.
Soma Neno Ukue Kiroho.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.