Kujaribu siku moja kusoma Neno la Mungu na kuacha, kwa sababu ya ugumu uliokutana nao ulipokuwa unasoma Neno la Mungu. Kuacha kwako kusoma Neno la Mungu hakukufanyi uwe na uelewa mpana, zaidi kunafanya uzidi kubaki na uelewa wako mdogo.

Wengi hili tunashindwa kulitambua, mtu anaanza kusoma Neno la Mungu leo, anataka siku hiyo hiyo awe na uelewa mpana kama wengine walivyo. Amesahau hatua aliyonayo anastahili kuwa nayo, ila kadiri siku zitakavyozidi kwenda mbele kwa kujituma kwake, kutamfanya azidi kuwa viwango vya juu anavyovitamani.

Nimeona wengi wanaingia kusoma Neno la Mungu kwa hamu kubwa, ila baada ya siku chache unamwona ameacha kusoma Neno la Mungu. Ukimuuliza sababu ni nini, anaweza asikupe sababu ya msingi sana kwa kuogopa kukueleza ukweli. Ila ukweli amekutana na ugumu katika kusoma kwake, akaona achane na zoezi hilo la kusoma Neno la Mungu.

Hupaswi kuogopa mwanzo wako, wala hupaswi kuonea haya mwanzo wako mdogo, wanasema mwanzo ni mgumu, unapaswa uwe mvumilivu sana. Elewa kwamba jambo ulioanza nalo hukuwahi kulianza kwa namna uliyoamua kuanza nalo, tena umeanza ukubwani.

Kujenga tabia mpya ambayo hukuwa nayo hapo awali, itakuchukua muda mrefu sana mpaka kuja kusimama vizuri. Ukiwa mtu wa kukata tamaa mapema, hutoweza kufikia lengo lako, hutoweza kufikia viwango unavyotamani ufikie.

Huwezi kuwa mwalimu mzuri wa Neno la Mungu kama hufanyi mazoezi ya kufundisha, hata kama Mungu amekupa karama hiyo ya kufundisha wengine. Ukiwa mwoga wa kufundisha, alafu una karama ya kufundisha, hakuna hatua yeyote utasogea, na hakuna mtu atafaidika na kitu ulichonacho ndani yako.

Huwezi kulijua Neno la Mungu kwa kulipenda mdomoni, huwezi kuwa na maandiko matakatifu ya kutosha kwenye moyo wako. Ikiwa hutochukua hatua ya kusoma Neno la Mungu, ndio maana ni muhimu sana kuanza kusoma Neno la Mungu hata kama unaona ugumu mbele yako.

Usiogope hali yako ilivyo sasa, usijihukumu sana kwa jinsi unavyopata shida kuelewa, huo mwanzo wako unaouona ni mdogo, ndio utakaokupeleka kwenye hatua nyingine kubwa. Hata kama umeokoka kweli, kama husomi Neno la Mungu, siku ukianza kusoma uwe na uhakika utakutana na changamoto.

Bora yako unapata maarifa haya ya kukusaidia kusimama vizuri katika usomaji wako wa Neno la Mungu, wengine tulianza hivi hivi bila kupata maarifa yeyote. Ndio maana nakueleza kitu ambacho nina uzoefu nacho, nilivyokuwa wakati naanza kusoma Neno la Mungu sio nilivyo sasa, kuna hatua naiona ninayo tofauti kabisa na mwanzo.

Utasingizia huna muda wa kusoma Neno la Mungu, lakini tukija katika uhalisia tunakuta muda unao wa kutosha, sema ukikumbuka jana ulijaribu kusoma Biblia yako. Ukakutana na maneno ambayo hukuelewa, hiyo hali inakupa uvivu, inaeleweka wala sio kitu cha kushangaza sana, chochote unachokiona kwa mara ya kwanza lazima kikupe changamoto. Lakini kadiri unavyozidi kujifunza na kukiona, ndivyo unavyozidi kuwa imara na mzoefu wa hicho/hilo jambo.

Haijalishi una mwezi/miezi kadhaa tangu uanze kusoma Neno la Mungu, lakini bado unaona hujafikia vile viwango vya uelewa unavyovitamani kuvifikia. Hilo lisikuvunje moyo, endelea kusoma zaidi Neno la Mungu kuliko wakati mwingine wowote, huku ukimwomba Mungu akusaidie kuelewa vizuri yale unayosoma.

Usipokata tamaa mapema, utaanza kuona mabadiliko ndani yako, utaanza kuona uelewa wako unazidi kuongezeka siku hadi siku. Hayo ndio matunda ya mtu mvumilivu, mtu ambaye hakuvunjwa moyo na hali yake dhaifu aliyokuwa nayo wakati anaanza kusoma Neno la Mungu.

Soma Neno Ukue Kiroho.

Chapeo Ya Wokovu.

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.