Yapo mambo mengi sana tunayojifunza katika maisha yetu, hasa ukiwa mtu wa kupenda kujifunza mambo mapya kila siku. Hii inakupa nafasi nzuri ya kujifunza mengi zaidi, maana si wote wanapenda kujifunza mambo mapya. Wengine yale yale waliyojifunza zamani wanapenda kubaki nayo, na wakitaka kujifunza jambo jipya wanaona kile walichojifunza zamani ndio bora zaidi kuliko hicho cha sasa.

Unapopata nafasi ya kujifunza jambo jipya, na jambo lile ukaona vyema na wengine walijue, njia utakayotumia ni kuwashirikisha yale umejifunza. Sio rahisi kuwashirikisha yote uliyojifunza ila kuchukua hatua ya kuwashirikisha kile umejifunza, sio tu watapata faida wale unaowashirikisha hayo mazuri. Wewe kama wewe, unaongezeka uelewa zaidi wa yale uliyojifunza.

Huishii tu kuongeza uelewa, unaweka kumbukumbu isiyosahaulika kwa yale uliyojifunza, hutosahau kirahisi kitu ulichojifunza. Utaendelea kukumbuka zaidi na itakufanya usiwe msahaulifu kwa yale unayojifunza. Unapokumbuka kitu/jambo ulilojifunza, inakupa urahisi wa kutokwenda kinyume pale unapokumbuka kufanya hivyo ni kosa.

Hili la Kumshirikisha mwingine ulichojifunza ni jambo zuri sana kwa mtu anayependa kujifunza mambo mbalimbali, inamsaidia yeye kuendelea kupata faida zaidi. Tena atabarikiwa na Mungu, kwa kumsaidia mtu mwingine ambaye hakuwa akilifahamu hilo jambo, ila kupitia yeye amelifahamu.

Unaweza kuona ni jinsi gani faida zinazidi kuongezeka kwa mtu anayependa kujifunza mambo mapya na kuwashirikisha wengine yale anayojifunza. Mtu huyu aishii kupata faida yake mwenyewe, anaongeza watu wengine zaidi wenye ufahamu wa jambo hilo alilojifunza yeye.

Kama kuna tabia unapaswa kuijenga kwako, moja wapo ni hii ya kupenda kuwashirikisha wengine yale unayojifunza. Bila kuharibu maana halisi, hii itakufanya uzidi kupanua wigo wako wa uelewa. Tena hili zoezi la kuwashirikisha wengine, inakupa changamoto ya kuwa makini zaidi wakati wa kujifunza kwako.

Kwanini nasema inakupa changamoto ya kuwa makini zaidi, unapotaka kuwashirikisha wengine ulichojifunza, ukikurupuka katika hili utawadanganya watu. Huwezi kuwa tayari kuwapotosha watu, lazima utakuwa makini zaidi unapojifunza na unapotaka kuwashirikisha wengine ulichojifunza.

Wengi wanaona kuwashirikisha wengine ni zoezi gumu kwao, wanaona kama usumbufu fulani hivi, wanaona ni heri wao kujifunza jambo. Alafu hilo walilojifunza libaki tu kwao, ni sawa na mtu aliyeambiwa jambo fulani, yule aliyemwambia, anampa tahadhari ya kutokusema sehemu nyingine. Maana ni jambo la siri, halipaswi kila mtu kulijua, japo wanasemaga hakuna siri ya watu wawili.

Kusoma Neno la Mungu ni jambo la muhimu sana kwa mkristo yeyote yule mwenye safari ya kwenda mbinguni, unaposoma Neno la Mungu, alafu ukapata nafasi ya kumshirikisha mwingine kile umejifunza. Inakupa nafasi zaidi ya kupanua uelewa wako, na inakupa nafasi ya kuweka kumbukumbu zaidi kwa yale unayojifunza.

Unapokuwa kwenye kikundi mlichopangiana kusoma Neno la Mungu kila siku, sio tu inakusaidia wewe kuwa na Neno la Mungu kwa wingi moyoni mwako. Unapotoa tafakari yako kwa kile ulichojifunza, inawafungua wengine macho kwa hicho ulichowashirikisha, maana wakati wa kujifunza kuna yupo hakuelewa vizuri huo mstari unaoutolea maelezo.

Unaona hapo umemsaidia mtu mwingine ambaye hakuelewa vizuri, na hapo hapo umeongeza uelewa wako na kutosahau kirahisi kile ulichojifunza kwa kusoma. Ukijua haya, utakuwa huoni adhabu kusoma Neno la Mungu na kutoa tafakari yako kwa kile ulichojifunza.

Ukiona unapata shida kuwashirikisha wengine yale unaayojifunza, kuna sababu kadhaa hapo, huenda ulichojifunza hukuelewa kabisa, na huenda unafikiri ukiwashirikisha wengine ni kupoteza muda wako. Lakini kwa mtu aliyejua faida ya kusoma Neno la Mungu, na kumshirikishe mwingine aliyojifunza, ni furaha kwake kufanya hivyo.

Usione tena mzigo moyoni mwako, kumshirikisha mwenzako tafakari yako unaposoma Neno la Mungu, maana inakupa faida nyingi sana.

Soma Neno Ukue Kiroho.

Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.