Mara nyingi tunapopita kwenye changamoto ngumu, huwa tunapata mawazo ya kumpuzika kwanza kwa kile tulichokuwa tunakifanya. Kumpuzika kwetu sio kwamba kunatusaidiaga kuondoa changamoto tunazokabiliana nazo wakati huo, bali kunaleta uzembe wa kuanza kuona uvivu kufanya kile tulichokuwa tunakifanya.

Mawazo ya kupumzika kwanza kwa kile tulichokuwa tunakifanya, huwa tunafikiri tunasaidia jambo fulani. Huwa tunafikiri tunaleta unafuu wa kuondoa msongamano wa vitu katika maisha yetu. Bila kujua kuna vitu hupaswi kuacha kufanya hata kama unapitia magumu kiasi gani katika maisha yako.

Tuseme kwamba huwezi kuacha kula chakula cha mwili, kwa sababu unapitia changamoto fulani ngumu, unajua ukifanya hivyo matokeo utakayopata kwenye kuacha kula. Yatakuwa ni mabaya zaidi kuliko changamoto unayopitia, ndio maana wengi hawawezi kuacha kula. Hata kama wanajilazimisha kula kwa kukosa hamu kutokana na hali wanayopitia.

Kuna vitu unapovifanya vinakusaidia kuona changamoto unayopitia wakati huo si kitu sana, ufahamu huu unaupata kwenye kile unachokifanya na unachojifunza kila siku. Ujasiri huu wa kuchukulia changamoto yako kama darasa, hauji kwa ghafla, ipo gharama kubwa unakuwa umetoa kwenye maisha yako.

Wengi huwa tunakosea sana tunapokutana na changamoto, huwa tunaona tusitishe kwanza zoezi la kusoma Neno la Mungu. Wazo hili huwa linapata nguvu pale mtu anaposoma anakuwa anaona hana utulivu kabisa ndani yake. Wazo la kuacha kwanza kusoma Neno la Mungu hadi pale atapokuwa na utulivu, ndio wazo ambalo huwa linapata nguvu kwa wengi wetu.

Hatari iliyopo kwenye hili la kuacha kwanza kusoma Neno la Mungu hadi mtu atapojisikia utulivu ndani yake, wazo hili la kumpuzika kwanza huwa linaondoka na bidii ya mtu ya kusoma Neno la Mungu. Asilimia kubwa ya watu ambao nimewahi kuwa nao karibu katika kusoma nao Neno la Mungu, wengi waliacha kusoma Neno la Mungu wanavyojipa mapumziko.

Ukitaka kujirudisha nyuma kirahisi kwa wewe ambaye hujakomaa vizuri kwenye eneo hili la kusoma Neno la Mungu kila siku. Jipe likizo katika hili la kusoma Neno la Mungu, nakwambia ndio itakuwa tiketi yako ya kuacha moja kwa moja kusoma Neno la Mungu.

Kikubwa sana utakachobaki nacho katika kumbukumbu zako ni kukumbuka bidii yako ya nyuma ya usomaji wako wa Neno la Mungu, utabaki unawasimlia watu ulikuwa msomaji mzuri wa Neno la Mungu. Wakati huo unasimlia haya hukumbuki mara ya mwisho ulishika Biblia yako lini ukaanza kuisoma, unachokumbuka ni kuibeba Biblia yako kila siku za ibada na kupitishwa mistari michache.

Miongoni mwa vitu ambavyo hupaswi kuviruhusu katika maisha yako ya usomaji wako wa Neno la Mungu, ni kutojipa mapumziko wakati unapitia changamoto. Hakikisha unaweka bidii yako kwenye usomaji wa Neno la Mungu, katikati ya changamoto usiruhusu kujipumzisha kwanza, kama hiyo changamoto haihusiani na kushindwa kuona.

Kweli kabisa utafika mahali utaona huna unachokipata kwenye usomaji wako wa Neno la Mungu, hilo lisikusumbue na kukupa sababu ya wewe kuacha kusoma Neno la Mungu. Endelea kusoma Neno la Mungu bila kuacha, tena utaona ukitiwa nguvu mpya ndani yako, utaona ukipata tumaini jipya katikati ya changamoto yako, na utaona ushindi mkubwa ukiwa upande wako.

Sasa umeshaelewa huwa unajipotezea wapi, hakikisha hufanyi hili kosa tena unapokuwa kwenye changamoto yeyote ile. Umeshaelewa hata ukiacha kusoma Neno la Mungu hakukuondolei changamoto zako, zaidi unapoteza kitu cha thamani katika maisha yako.

Kukatisha kusoma Neno la Mungu kwa sababu unapitia magumu, hakutakusaidia kuondoa hayo magumu unayopitia zaidi inakuongezea maumivu zaidi ndani yako.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu.

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.