Kila mmoja ukimgusa kuhusu Mungu, ataonyesha mwenye hofu ya Mungu, ataonyesha anampenda sana Mungu wake. Lakini ukija katika matendo yake yanamkataa Mungu, yanamchukiza Mungu, hayaonyeshi upendo wowote wa kiMungu ndani yake.

Wengi tunafikiri kusema tunampenda Mungu mdomoni tu huku mioyoni mwetu tunamkataa, huku matendo yetu ya nje haonyeshi yale tunatamka mdomoni au kwa vinywa vyetu. Haiwezi kubadilisha ukweli kuwa hatumpendi Mungu wetu.

Mtu anayempenda Mungu wake, atatafuta kwanza kuzijua amri zake, na kuzishika hizo amri za Mungu. Huwezi kushika kitu ambacho hukifahamu, na ili ukifahamu, itabidi uwe na muda wa kujifunza hizo amri kupitia Neno la Mungu.

Rejea:Yeye aliye na amri zangu, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye; naye anipendaye atapendwa na Baba yangu; nami nitampenda na kujidhihirisha kwake. YN. 14:21 SUV.

Muda wa kuzijua amri za Mungu unaweza kuutenga mwenyewe kupitia siku yako, ni jambo la muhimu sana kuliweka kwenye ratiba zako za siku. Moja ya kuonyesha unampenda Mungu wako ni pamoja na kupenda Neno lake, kama huna muda wa kusoma Neno la Mungu huwezi kusema unalipenda.

Hapa Mungu anasema aliye na amri zake, na kuzishika, yeye ndiye anipendaye. Sio kumpenda tu, wala Mungu haishii hapo, kwa sababu mtu wake anampenda, anasema na yeye atampenda na kujidhihirisha kwake.

Mungu atajidhirisha wazi wazi kwako, utamwona akikushindia mambo magumu usiyoyaweza, utamwona akikupigia kila hatua ya maisha yako, utamwona akijihusisha na mambo yako. Mahali unafika watu wanasema hapa ndio mwisho wa maisha yake, hapo hapo yeye ndio ana jidhirihisha wazi.

Unaweza kuona sasa, mtu anayesema anampenda Mungu wake alafu hazishiki amri zake, huyo anadanganya. Aliye na amri za Mungu na kuzishika, huyo ndiye anayempenda Mungu, naye Mungu atampenda yeye.

Shida ipo pia kwa mtu anayezijua amri za Mungu kwa kuzisoma kupitia Neno lake, alafu hazishiki na kuzifuata hizo amri, hana tofauti yeyote na mtu asiyezijua kabisa. Maana kama anazijua amri za Mungu alafu hazishiki, wala hazitendi, wala hazifuati, huyo hawezi kusema anampenda Mungu.

Anayempenda Mungu, atafuta kuzijua amri za Mungu kupitia Neno lake, akishazijua amri zake Mungu, atazishika na kuzifuata. Naye Mungu atampenda mtu huyo na kujidhihirisha kwake, ndivyo maandiko matakatifu yanavyotuambia sisi.

Maneno matupu hayawezi kuonyesha kile kilichopo ndani ya moyo wako, matendo yako ndio yanaonyesha kile kimeujaza moyo wako. Kuishia kwenye maneno matupu, haikubaliki, lazima matendo yako yazungumze, bila hata wewe kusema nampenda Yesu Kristo. Matendo yako yatadhihirisha wazi huyu kaka, dada, mama, baba, anampenda Mungu wake.

Lazima tutafute kwanza kuzijua amri za Mungu, tukishazijua sasa, hatua inayofuata ni kuzishika hizo amri, tukishazika sasa. Hapo ndipo tunaonekana tunampenda Mungu wetu, inatia moyo zaidi anaposema hivi; tukishazijua amri za Mungu na kuzishika, naye Mungu atatupenda na kujidhihirisha kwetu.

Jambo la kuzingatia hapa ni kuwa na muda wa kusoma Neno la Mungu, Neno ndio litakupa kujua amri za Mungu, hizo amri huwezi kuzijua kwa kuzitunga mwenyewe. Utazijua kupitia Neno lake takatifu, na ukishazijua muhimu kuzishika na kuziishi.

Usije ukasema mbona nazishika amri za Mungu, siibi, sizini, wala sisemi uongo, lakini pamoja na hayo yote hufanyi, kuna kitu huna, upendo. Upendo kwako haupo, na kama upo ni wa kinafiki, unamchekea mtu machoni ila moyoni mwako umejaa chuki naye.

Msingi wetu wakristo ni Neno la Mungu, Neno la Mungu ndilo linatufanya tuishi maisha yenye kuvutia wengine wasiomjua Kristo. Bila kuwa na msingi huu, tutageuka kero kwa wale wasiomjua Kristo, wataanza kusema kama huyu anasema ameokoka. Hata na mimi nitakuwa nimeokoka, maana yake kuna mambo tunafanya kinyume.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu.

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081