Hebu fikiri unapitia katika jaribu fulani gumu sana, huku ukiwa na mtazamo kwamba Mungu yupo mbali sana. Maana tangu ukue uliambiwa Mungu yupo mbinguni, ukiangalia mbingu zilivyo mbali, unaona hata maombi yako unayoomba mpaka yaje yafike mbinguni ni kazi sana.

Wakati upo katika mtazamo wa kwamba Mungu yupo mbali sana, katika kujifunza kwako Neno la Mungu ukakutana na Neno lake lenye kukuonyesha jambo tofauti kabisa na ulivyokuwa unawaza moyoni mwako.

Sio tu utafurahia kujua kitu tofauti na ulivyoamini miaka mingi, bali inakufanya kuinua imani yako upya na kuona unayemwamini yu karibu nawe sana. Hayupo umbali vile ulivyokuwa unafikiri miaka mingi iliyopita.

Unapofika muda ukajua Mungu wako yupo karibu, upendo wako kwa Mungu unaweza kubadilishwa kimtazamo. Sio kwamba zamani ulikuwa huonyeshi upendo wako kwa Mungu ila unapojua Mungu wako alivyokaribu nawe, tofauti na ulivyokuwa unafikiri zamani. Inakupa hatua nyingine tena ya kujua uliyeweka imani yako kwake hayupo mbali.

Unapojua Mungu wako hayupo mbali, kwanza maombi yako yatabadilika, yatabadilikaje? Ndani ya mtazamo wako utaanza kufikiri tofauti na mwanzo ulivyokuwa unafikiri. Hii inakuja baada ya kujifunza jambo jipya katika maisha yako ya wokovu.

Tunaposema Neno la Mungu ni muhimu sana kila mmoja kuwa na muda wa kulisoma, na kupata muda wa kutafakari yale aliyojifunza. Ipo maana kubwa sana, huenda ukachukulia jambo la kawaida sana ila ipo nguvu inayopatikana ndani ya Neno la Mungu.

Kuna mistari ya Biblia utakutana nayo wakati unasoma Neno la Mungu, inaweza ikakushangaza na kukufanya uanze kujiuliza maswali mengi, moja ya swali linaweza likawa, kwanini tangu zamani hukulijua hilo. Maana yake kuna kitu kilikuwa kinakusumbua sana miaka mingi bila kupata majibu yake ila kupitia kusoma kwako Neno la Mungu ukapata majibu yake.

Kupitia usomaji wa Neno la Mungu, zipo faida nyingi sana na zimegawanyika katika makundi mengi, na katika nyanja mbalimbali. Huwezi kuzitaja ukazimaliza, ndio maana ipo vita kubwa katika usomaji wa Neno la Mungu, inahitaji ujitoe haswa bila kuangalia mazingira uliopo.

Leo tunapata kujua Mungu wetu yupo karibu sana, tukimwita anaitika, inaweza ikawa ngumu kwako kuamini ila leo unaenda kuamini hili ninalokueleza hapa. Hata kuomba kwako leo kunaenda kubadilika, maana umeongeza maarifa mengine sahihi ndani yako.

Rejea:Mimi ni Mungu aliye karibu, asema BWANA, mimi si Mungu aliye mbali. YER. 23:23 SUV.

Sijui umeona nini ndani ya huo mstari, huo mstari umebeba Neno kubwa sana lenye kukuonyesha ukaribu wa Mungu wako. Mungu mwenyewe anasema hivi, mimi si Mungu aliye mbali, asema BWANA.Anasema BWANA na si mwanadamu, yeye mwenyewe Mungu anathibitisha ukaribu wake.

Jukumu letu kuendelea kutafuta maarifa sahihi ya Neno la Mungu, mtazamo wako unapaswa kubadilika namna unavyolichukulia Neno la Mungu. Huenda unalichukulia ni kitu cha ziada sana, yaani usome, usisome ni yale yale tu. Mtazamo huu unaweza kuwa umejengeka miaka mingi sana ndani yako, kuutoa na kuingiza mtazamo mpya inahitajika gharama na nidhamu ya hali ya juu.

Utakutana na changamoto nyingi katika kuanza kwako kusoma Neno la Mungu, lakini hupaswi kurudi nyuma. Hutaanza kusoma Neno la Mungu leo na wiki ijayo uwe umepata kile ulikuwa unataka, pia hutoweza kuondoka haraka kwenye tabia yako ya awali ya kupuuza Neno la Mungu. Itakuchukua muda sana kujenga tabia mpya na nzuri.

Usifikiri itatokea ghafla ukawa msomaji mzuri wa Neno la Mungu, kuna mahali pagumu utapita kwanza ndipo uje uwe imara katika eneo hilo la usomaji wa Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081