Unaweza kupata shida sana kwanini unaposoma Neno la Mungu huwa mara nyingi sana huelewi unachosoma, utajihidi kusoma kweli ila hupati ule ujumbe uliokusudiwa kwako. Hii inaweza kukufanya usione ladha ya Neno la Mungu, hata pale unapoambiwa kusoma Neno la Mungu ni kuzuri sana. Kwako utaona hizo ni hadithi tu, maana huoni ule uzuri unaozungumzwa.

Hali hii inaweza kumkuta kila mtu ila unapaswa kujua namna ya kujitoa haraka kwenye hali hiyo, usipojua namna ya kujitoa haraka kwenye hali hiyo unaweza kusoma Neno la Mungu ukatoka mtupu. Badala ya kutoka na kitu cha kukusaidia katika maisha yako ya kiroho na kimwili.

Wenzako wanaweza kutoa shuhuda mbalimbali jinsi walivyobadilishwa na Neno la Mungu, kwako utaona ni kama vile wanajifanyisha ila hakuna ukweli wowote. Unaweza ukawa sahihi kabisa kutokana na wewe mwenyewe ndiye shahidi wa hilo, maana unasoma sana Neno la Mungu ila huoni hicho kinachosimliwa na wengine.

Nisikupeleke mbali sana, niende moja kwa moja kwenye lengo ili uweze kujua huwa unakosea wapi na unapaswa kuchukua hatua gani, ili uweze kufurahia usomaji wako wa Neno la Mungu.

Unapokuwa kwenye usomaji wa Neno la Mungu(Biblia) hakikisha unasoma akili yako ikiwa mahali pamoja. Nikiwa na maana kwamba, usiwe unawaza mambo mengine alafu unaendelea kusoma Neno la Mungu, hapo moja kwa moja hutopata ule ujumbe uliokusudiwa kwako.

Kujua unachosoma kinakuingia na unakielewa vizuri, utaanza kupata picha inayohusiana na unachosoma. Labda unaweza ukawa unasoma habari za Elia, kuna picha ya Elia itakuja kwenye akili zako, sio kwamba unamfahamu ni vile unasoma habari zake unapata picha kuhusu yeye.

Si umewahi kuona mtu anakusimlia kuhusu mahali fulani palivyo pazuri, vile anakusimlia unapata picha ya mahali pale, unaanza kuona huo uzuri wake sio kana kwamba umewahi kufika. Jinsi anakusimlia inakupa picha ya huo uzuri anaouzungumzia kwako.

Ndivyo ilivyo katika usomaji wako wa Neno la Mungu, akili/mawazo yako yakiwa sehemu moja, inakuwa rahisi kwako kuona ladha ya Neno la Mungu ilivyo. Unaposoma habari za Mungu, unaanza kumwona Mungu alivyo na uweza/ukuu wake, sio kwamba anaonekana kwa macho ila ule ukuu wake unazongumzwa unapata picha fulani akilini/kichwani kwako kwa imani.

Unachotakiwa kufanya ni kujiangalia kwanza kabla hujaanza kusoma Neno la yote Mungu, au unapaswa kujihoji unapoendelea kusoma Neno la Mungu. Kujihoji huko ni kujiangalia akili zako zipo kwenye Neno la Mungu au zinawaza madeni, au zinawaza familia, au zinawaza kula, au zinawaza ndoa yako, au zinawaza waliokutendea mabaya, au zinawaza kesho utakula nini na nk.

Huwezi kuepuka hivyo vitu ila unapaswa kuyapa muda wake hayo yanayotaka kuingilia muda wako wa Neno la Mungu. Kweli inaweza kuwa kuna jambo gumu sana linakukabili mbele yako ila usiruhusu likutawale kiasi kwamba ushindwe kufanya mambo yako mengine.

Huenda nimekupa somo geni kwako ila anza kulifanyia mazoezi, utaona ukiwa huru kufanya mambo yako, utaona ukiwa huru kusoma Neno la Mungu bila mwingiliano wa mawazo mengine. Baada ya kumaliza kufanya ulichopaswa kufanya unaweza kuruhusu mawazo mengine.

Njia hii nimekuwa nikiitumia sana wakati wa kulala, zamani nilikuwa sipati usingizi mzuri kwa sababu ya kuwaza sana changamoto fulani inayonikabili. Baadaye nikapata njia ya kuondokana na hiyo hali, muda wa kulala ukifika tu huwa naweka pembeni mambo mengine. Nalala usingizi mzuri sana, nikiamka ndio naanza kufikiri kile kilichokuwa kinanikabili, wakati mwingine huwa naamka tayari nimeshapata namna ya kulitatua hilo jambo.

Ukiweza kukabiliana na wewe mwenyewe, hata kama utaletewa taarifa mbaya utaweza kukabiliana nayo. Unaweza kuletewa taarifa mbaya ukiwa unafanya jambo nyeti sana, hutoweza kuondolewa haraka kwenye hilo jambo kama hiyo taarifa ukitekeleza hakuna utakachookoa. Mfano, unaletewa taarifa za msiba, kimsingi huwezi kubadilisha matokeo yale, hata kama utakibilia. Huenda nimekutolea mfano mgumu ila unaweza kuufanyia mazoezi taratibu.

Bila shaka umefahamu namna ya kuweza kufurahia usomaji wako wa Neno la Mungu kwa kuweka mawazo/akili zako kwenye usomaji wako. Haijalishi unapitia kwenye jaribu gani gumu, hakikisha unapofika muda wa kusoma Neno la Mungu na kutafakari, unakuwa umejitoa kwenye mawazo mengine.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu.

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.