Tunakuja kukwama kwa vile vitu vizuri tulivyovianzisha katika maisha yetu, bila wengine kuelewa nini kimetufanya tushindwe au tuishie njiani. Hata sisi wenyewe wahusika inaweza ikatupa changamoto kujua sababu kwa haraka, kwa sababu ile picha tuliyoijenga wakati tunaanza kufanya kile kitu. Ndio iliyotufanya tuvunjike moyo baada ya kutopata yale matokeo tuliyoyatengemea.
Kuna ndugu mmoja aliniomba nimuunganishe kwenye group la Chapeo Ya Wokovu la kusoma Neno la Mungu kila siku. Binafsi nilijua nia yake ilikuwa kusoma kweli Neno la Mungu, kumbe nia yake haswa haikuwa hiyo. Japo alitaka kusoma Neno la Mungu.
Huyu ndugu alivyojiunga hakuwa mhudhuriaji mzuri wa vipindi vya Neno la Mungu, maana tuna utaratibu wa kusoma sura moja kwa siku na kushirikishana tafakari zetu kwa kile ulichojifunza. Na usipofanya hivyo utakuwa umejiweka kwenye nafasi ya kuondolewa kwenye group.
Baadaye huyu ndugu alijitoa kwenye group, ndugu mmoja ndani ya group akaja inbox yangu kunitaka nimwendee yule ndugu aliyejitoa. Ili kujua nini kimempelekea yeye kujitoa kwenye group, ilibidi nitii wito ule.
Nilivyomfuata kumuuliza nini shida mbona amejitoa, alinipa jibu ambalo lilinifanya nishangae kidogo, madai yake yalikuwa ni kwamba; haoni ushirikiano wowote kwenye group, akiposti ujumbe watu wapo kimya. Sio kwamba ameuliza swali, alafu watu wakakaa kimya bila kumjibu la hasha haikuwa hivyo.
Kingine ukifuatilia ameposti ujumbe mara ngapi, utakuta ni mara moja, na tangu ajiunge kwenye group ushiriki wake wa Neno la Mungu ni zero kabisa. Anachotazama yeye watu wamjali anavyotaka yeye.
Ukijiona una tabia hii ujue bado una utoto ndani yako, yaani unakabiliwa na uchanga wa kiroho. Haijalishi umri ulionao, kama una tabia ya namna hii ndani yako, huo ni utoto, kama unafanya vitu watu wakuone sio kukuona tu wakupe sifa nyingi hata kama sio za kweli. Huo ni uchanga wa kiroho.
Tabia ya watu makini, huwa hawawezi kukuamini haraka, hata kama utafanya kitu kizuri cha namna gani. Ndani ya mioyo yao watasema huyu anafanya vizuri ila watataka waone ni kweli au ni nguvu za soda.
Wengi wameacha huduma kwa sababu ya uzembe huu, alianza huduma kwa kutegemea watu wampe sifa kibao. Badala ya sifa amekuwa akikutana na changamoto za kuvunjwa moyo, kama hujakomaa kiroho, na hajajawa kwa wingi na Neno la Mungu au mafundisho ya neno la Mungu. Huyu mtu hatofika mbali atakuwa ameachana na kile kizuri alichokuwa anakifanya.
Moja ya sababu zinazowafanya wengi washindwe kuendelea na usomaji wao wa Neno la Mungu ni hii ya kutosifiwa na watu aliotegemea watamsifu. Alivyoona hakuna maneno yeyote ya kumtia moyo kama alivyotarajia, anajiona alichokuwa anakifanya hakijamzalia matunda ya sifa.
Kuwa makini sana na hili, usifiwe ama usisifiwe, ukatishwe tamaa ama usikatishwe tamaa, upongezwe ama usipongezwe. Hilo lisikupe shida wewe Mungu anakuona, hata kama ni jambo jema mtu kukupongeza kwa kazi nzuri uliyofanya. Kama hujakutana na hilo isikufanye ukaacha kusoma Neno la Mungu, kwa sababu unasoma Neno la Mungu kwa manufaa yako mwenyewe.
Soma Neno la Mungu kwa manufaa yako mwenyewe, achana na habari zingine, ukifanya hivi hata wakitokea watu wa kukuvunja moyo. Bado utaweza kusimama tena na kuendelea na ratiba yako ya usomaji wako wa Neno la Mungu.
Ufike mahali ukomae kiroho, hata kama ulitakiwa kusifiwa ila wakaanza kukuponda, isikuondoe kwenye lengo lako hata kama itakuumiza moyoni. Huo ndio ukomavu wa kiroho, sio unakutana na vikwazo kidogo unazira na kuacha kufanya kile ulikuwa unafanya, uwe unajikumbusha hufanyi kwa ajili ya mtu.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081