Usipolijua Neno la Mungu, yapo mambo ya msingi utaacha kuyafanya, kwa sababu ulitendewa mabaya na huyo uliyeamua kujitenga naye. Au unaweza kuacha kabisa kuwatendea wengine mema, kwa sababu kuna watu/mtu hawakukutendea mema ulivyowatendea wewe badala yake walikutendea mabaya.

Unaweza kutengeneza hadithi kama hii; zamani nilikuwa nawatendea sana watu mema ila nilikuja kuacha kufanya hivyo. Baada ya kuambulia kusemwa vibaya, baada ya wao kukaa pembeni nilivyohitaji msaada wao na mengine mengi ya kukuumiza moyo wako.

Hatuwezi Kuukataa ukweli, kweli kabisa kuna mambo yanaumiza sana mioyo yetu, hasa kama umekuwa ukijitoa sana kwa wengine. Inafika siku unahitaji ushirikiano/msaada wao, wanakaa pembeni wote kama hawakujui. Kibinadamu inaumiza sana na usipokuwa makini inaweza kukufanya ukawa na roho mbaya ya chuki ndani yako, na inaweza kukufanya ukajitenga kabisa na watu.

Usipokuwa mtu makini na mtu imara wa kuweza kukabiliana na changamoto kama hizi zinapojitokeza kwako, unaweza kujenga picha mbaya sana kichwani mwako. Picha hii mbaya ikakufanya ukaacha kutenda mema kabisa hata kwa watu ambao hawajakukosea lolote, na hata kama wamekukosea unapaswa kufahamu, kisasi ni juu ya Bwana.

Unapokuwa mtu wa kusoma Neno la Mungu, unajengwa katika msingi mzuri na imara wa kuweza kukabiliana na hali yeyote ngumu inayokupata. Na unakumbushwa mambo ya muhimu kuzingatia unapokutwa na hali ya kuumizwa na wale uliowatendea mema.

Maandiko matakatifu yanatuonyesha na kutukumbusha mambo mawili, la kwanza ni kutenda mema na la pili ni kushirikiana.Haya mambo mawili Mungu anasema ni sadaka zimpendezazo yeye, kumbe tunapoacha kutenda mema na kushirikishana na wengine tunakuwa tunakosa baraka za kiMungu.

Rejea: Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu. EBR. 13:16 SUV.

Kwa sababu ulifanya sherehe, hakuna ndugu aliyeshirikiana na wewe, unapata hasira moyoni mwako na kusema hutakaa ushiriki mambo ya watu wengine. Unapaswa kujiuliza maswali mwenyewe, wewe umeshirikiana mangapi na watu? Umejitoa kiasi gani kwa mambo ya wengine?

Kwa sababu kama umekuwa mtu wa kujitoa mambo ya wengine, likifika la kwako Mungu atakuinulia watu wengine wa kukusaidia. Hata kama hao ndugu uliowategemea wakikaa pembeni, kwa sababu ulitoa sadaka inayompendeza Mungu wako, hatakuacha uibike.

Wengi tumeshindwa kulitambua hili, na tumejitoa kabisa kushirikishana na wengine, na tumeacha kabisa kutenda mema, kwa sababu ya kuumizwa mioyo yetu na hao tuliowatendea mema. Kama tungejua Mungu alivyotutetea katika hayo tuliyofikiri watu hawakuonyesha ushirikiano wowote kwetu, tungeongeza bidii ya kutenda mema na kushirikiana na wengine.

Tenda mema na shirikiana na wengine katika mambo yao, na wewe Mungu atakuinulia watu wake wa kushirikiana na wewe. Sio unakaa pembeni kwa mambo ya wengine, yaani huwatendei wengine mema, wala hushirikiani nao kwa chochote. Alafu unataka likifika jambo lako unataka watu wakutendee mema na waonyeshe ushirikiano mkubwa kwako.

Kama uliacha kutenda mema kwa wengine, na kama uliacha kushirikiana na wengine, kwa sababu zozote zile, nakusihi leo urudi haraka kwenye mstari. Maana kutokufanya hivyo ni chukizo kwa Mungu, kama MUNGU anapendezwa na kutenda mema na kushirikiana, je! unafikiri usipofanya hivyo inakuwaje? Ni mbaya sana kwako.

Usipompendeza Mungu, je! Utampendeza mwanadamu mwenzako? Unafikiri jambo lako linalohitaji ushirikiano wa watu, je! Litapata huo ushirikiano? Unafikiri usipotenda hayo mema, siku unataka watu wakutendee hayo mema, je! Watakutendea?

Tafuta kumpendeza Mungu wako kwa kutenda mema na kwa kushirikiana na watu, acha kujiweka mbali na watu, maana ndipo baraka zako zilizo. Usifanye kwa sababu ya watu, fanya kwa sababu ya kutafuta kumpendeza Mungu wako.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.