Tunapaswa kuweka bidii sana katika shughuli zetu za kimwili na kiroho, unapokuwa mfanyakazi/mfanyabiashara unapaswa kuweka nguvu na muda wako mwingi katika hilo unalolifanya. Na unapokuwa mtumishi wa Mungu, utapaswa kuwekeza muda wako mwingi katika huduma.

Katika kuwekeza muda wako mwingi katika hayo maeneo niliyoanza nayo, unapaswa pia kuwa na muda na familia yako, ikiwa hutokuwa na muda na familia yako. Utakuwa unatengeneza jambo ambalo baadaye litakuwa mzigo mkubwa kwako.

Kuketi na watoto wetu, kujua maendeleo yao, kuwekeza maarifa ya kiMungu ndani yao, kuwajengea misingi mizuri ya kumjua Mungu wao, na kuwajengea uwezo wa kuweza kujisimamia wenyewe ni jambo la msingi sana kwa mtoto/watoto wako.

Njia utakayomtengenezea mtoto leo, ukamwelekeza unapaswa kupita hii njia, hiyo njia hataiacha hadi uzee wake. Kila atapokuwa anapita atakuwa anafuata zile njia ulizomwambia apite, na yale uliyomkataza akiwa mtoto hatafanya.

Vile unavyoweka nguvu nyingi ya muda wako kwa watoto wako, ndivyo unavyomtengeneza na yeye kuja kuwa baba bora wa baadaye, na ndivyo unavyomtengeneza kuja kuwa mama bora wa baadaye. Hakuna kubahatisha hapa, vile unaishi sasa ni matokeo ya malezi yako tangia ukiwa mtoto mdogo.

Mtoto akiwa mdogo, anamwamini zaidi mzazi wake au yule anayekuwa naye karibu muda mwingi, leo tunaona wazazi wengi wameachia watoto wao walelewe na wafanyakazi wao, na wengine wamewapeleka shule za watoto wakelelewe huko. Bila kujua maarifa ya mzazi ni ya muhimu sana kwa mtoto, bila kujua mzazi anapaswa kuhakikisha ameweka vitu vya msingi kwenye ufahamu wa mtoto wake.

Na ili uweze kumjenga mtoto wako katika maandili mema, wewe kama mzazi unapaswa kuwa mcha Mungu, unapaswa kumjua Mungu wako vizuri. Itakuwa ngumu kumwelekeza mtoto wako njia impasayo kuenenda, wakati wewe mwenyewe njia zako ni za ovyo. Kumbuka mtoto wako anajifunza kwako kwa kuona na kusikia.

Unaweza kumfundisha jambo fulani zuri lenye kumsaidia, alafu akaja kukuona wewe hulifanyi. Badala yake ukawa unafanya lile ambalo hutamani mtoto wako aje awe kama wewe, utashangaa na yeye ataanza kutamani kufanya kama wewe.

Mfano ukiwa mvutaji wa sigara, unaweza kutumia njia nyingi mtoto wako asije akawa kama wewe ila ukashangaa kadri anavyozidi kukuona unavuta sigara. Hiyo picha inajengeka kichwani mwake, siku na yeye ameanza kujiona amekua, utamkuta anavuta, utajaribu kumpiga ila inaweza kushindikana.

Nikirudi katika suala la usomaji wa Neno la Mungu, ukiwa na utaratibu wa kusoma Neno la Mungu kila siku, na ukamwelekeza mtoto wako awe msomaji wa Neno la Mungu. Ukahakikisha hili jambo analifanya kila siku, uwe na uhakika hataacha hili la usomaji wa Neno la Mungu hadi uzee wake.

Nilikuambia mtoto anajifunza kwa kusikia na kuona/kutazama, unapomkazania mtoto wako asome Neno la Mungu na akawa anakuona na wewe unasoma. Ataona ni jambo la zuri na la muhimu sana kwake, utashangaa mtoto wako analipenda Neno la Mungu kuliko hata wewe, chanzo ni wewe mwenyewe.

Ukiwa kama mzazi na unasoma ujumbe huu, na umepata bahati ya kujijengea utaratibu wa kusoma Neno la Mungu kila siku. Hakikisha unawajengea watoto wako hii tabia, hasa wale ambao bado wadogo, si unajua mtoto atabaki kuwa mtoto kwa mzazi wake hata kama ni mtu mzima? Bila shaka unaelewa hilo.

Kama hukuwa na utaratibu wa kusoma Neno la Mungu, nakusihi uanze sasa hivi kusoma Neno la Mungu, itakuwa rahisi sana kwako kumfundisha mtoto wako jambo ambalo unajua faida zake. Nakwambia uwe msomaji wa Neno la Mungu, kwa sababu najua kuna faida nyingi katika hilo.

Hebu tutazame Neno la Mungu linasemaje kuhusu hili la kumlea mtoto katika njia impasayo, huenda ukafikiri ni jambo la kawaida tu.

Rejea: Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee. MIT. 22:6 SUV.

Naomba ulishike sana hilo andiko uwe unaliimba katika moyo wako, unaweza kukazana kumpa mtoto wako elimu nzuri ya darasani/ya kidunia. Lakini ukaacha kuwekeza maarifa ya kiMungu ndani yake, ukaacha kumwelekeza njia nzuri za kuweza kumsaidia katika maisha yake ya kiroho.

Hakikisha unamfundisha mtoto wako umhimu wa Neno la Mungu, hataliacha kamwe hadi uzee wake, sio mimi niliyesema ni maandiko matakatifu yamesema. Malezi mazuri ni pamoja na kuwekeza eneo la kiroho, ukisahau hili hata elimu yake ya dunia hii haitamsaidia kushinda dhambi.

Na mwalimu mzuri wa kumsaidia mtoto wako ni wewe mwenyewe, hakikisha unakuwa na muda na mtoto/watoto wako wakati bado unaweza kuwaambia jambo wakalifanya. Kuna msemo unasema hivi, samaki mkunje angali mbichi, ukisubiri akauke hutoweza kumkunja.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu.

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081