Maisha ya mkristo ili yawe safi katika njia iliyonyooka, yanapaswa kuongozwa, huwezi kuishi maisha yanayompendeza Mungu wako bila kuwa na mwongozo sahihi wa kuyaishi hayo maisha. Japo tunaweza kujua hili ni dhambi na hili si dhambi ila si yote tutaweza kuyafahamu, na kama tutayafahamu tunalolitenda ni dhambi, tutapaswa kujua tukiliacha tunafuata lipi lililo sahihi.

Ndani yetu lazima pawepo na dira inayotuongoza tuishije na tuenendeje, bila hiyo tutajikuta tunamtenda Mungu dhambi kwa mambo madogo madogo tusiyodhania kama yanaweza kutufanya tusiione mbingu.

Maisha yetu ya kila siku ya kimwili, tunategemea sana macho yetu ya nyama, miguu inapata ujasiri wa kusonga mbele kwa sababu macho yetu yanaona. Inapofika usiku, ule uwezo wetu wa kawaida wa kuweza kuona unakuwa mdogo, tunaanza kuhitaji kitu kingine kitusaidie kuyapa uwezo macho yetu yaweze kuona.

Jua linatupa mwanga, na jua linapotoweka huwa tunatumia mwezi, inapofika wakati mwezi nao haupo macho yanakosa uwezo wa kuona sawasawa. Inatulazimu tutumie vifaa vingine kama vile toshi/simu ya mkononi ili tuweze kutembea usiku, usipotumia tochi yenye mwanga unaweza kujikwaa vibaya sana kwa sababu ya kutokuona vizuri kwenye giza.

Tunapokuwa na usafiri wa gari au pikipiki, kinachotufanya tuendeshe gari kuelekea mahali tunapokwenda ni taa yenye mwanga mzuri. Bila taa na mwanga mzuri wa gari, ukiwa kama dereva wa gari hilo hutaweza kuliendesha gari lako kwenye giza, maana mwanga ndio unakuwedhesha kuona barabara vizuri.

Ndivyo ilivyo katika maisha yetu ya kiroho, tunahitaji kuongozwa ili tusijikwae, ili tusiingie kwenye mashimo, ili tusipamie madaraja, na ili tusiiache njia sahihi. Tunahitaji sana taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu.

Hatuwezi kuishia kuongozwa sala ya toba na kulikiri jina la Yesu Kristo tukasema imetosha, bado tupo duniani, tuna safari bado, tutawezaje kuyaishi maisha matakatifu yanayompendeza Mungu? Lazima tuwe na kitu kinachotuongoza kuyaishi hayo maisha matakatifu.

Kitu hicho Mungu ametupa ambacho ni Neno lake, Neno la Mungu ndio taa ya miguu yetu, na mwanga wa njia zetu, ukilishika Neno la Mungu huwezi kujikwaa njiani, utaishi maisha ya kumpendeza Mungu wako bila kusukumwa na mtu yeyote. Hutokuwa na ujasiri wa kumtenda Mungu dhambi hata kwa siri, haijalishi watu wanakuona, wala haijalishi watu hawakuoni, hutoweza kumtenda dhambi, kwa sababu moyo wako umejaa Neno la Mungu.

Rejea: Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu. ZAB. 119:105 SUV.

Haleluya, umeona hilo andiko, linatupa kujua kumbe tunaweza kuwa salama katika maisha yetu ya wokovu. Ipo taa ya miguu yetu ambayo ni Neno la Mungu, na upo mwanga unaotumlika njia yetu ambao ni Neno la Mungu.

Kwanini utembee kwa mashaka? Kwanini uwaze kuanguka? Lipo Neno la Mungu linaweza kukuondoa kwenye mashaka, huna njia nyingine ya kuweza kuishi maisha matakatifu, maisha yanayompendeza Mungu wako pasipo kulishika Neno la Mungu, Neno la Mungu linapaswa kujaa moyoni mwako.

Rejea:Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. ZAB. 119:11 SUV.

Bado tu huamini kuwa Neno la Mungu ni kila kitu kwako? Bado tu unalichukulia kawaida Neno la Mungu? Umesoma ujumbe huu hadi hapa na bado huoni umhimu wa Neno la Mungu katika maisha yako ya kiroho/wokovu, unahitaji msaada wa haraka sana. Kama umeelewa unapaswa kuhakikisha Neno la Mungu linakaa kwa wingi ndani yako, na kulitendea kazi katika matendo, nikiwa na maana usikariri mistari ya Biblia kama haikusaidii kitu.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu.

Blog: www.chapeotz.com

Email: chapeo@chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081