Uchanga wa kiroho una tabu nyingi sana ndio maana unapaswa kupingwa kwa nguvu zote, mchanga wa kiroho huwa ametawaliwa zaidi na mambo ya mwilini. Ukijaribu kumweleza vitu vya rohoni, lazima mtapishana kauli mbali sana na hatokuelewa kabisa.

Mchanga wa kiroho unapaswa kumlea kama yai, kama huwezi kumlea kama yai, uwe na uhakika mtashindwana muda sio mrefu. Uwe na uhakika atakuchukia kwa mafundisho yako unayotoa kwake kuhusu kumpendeza Mungu wake.

Mtu wa tabia ya mwilini ambaye ni mchanga wa kiroho yeye huwa ameshika kwamba, Mungu huangalia moyo wa mtu na si mambo ya mwilini. Maana yake hataki kabisa umguse vile anavyozungumza, vile anavyovaa, na vile anavyotenda mambo yasiyofaa hata kwa jamii isiyomjua Kristo.

Watu wa namna hii hawapendi mafundisho makali au magumu, mafundisho yanayogusa maovu yao, ukishagusa machafu yao, utaanza kusikia huyu mtumishi yukoje. Hawatakufurahia hata kidogo, hawapendi waambiwe acheni njia zenu mbaya wamgeukie Bwana.

Vizuri kufahamu hili ukiwa kama mtumishi wa Mungu unayetumikia, unaweza kufika mahali ukakemea uovu. Ukaishia kuchukiwa kiasi kwamba umefanya kitu kibaya sana, uwe na uhakika mahali umefanya hayo walikuwa bado hawapaswi kulishwa chakula kigumu. Walichozoea wao ni kunyweshwe vitu vilaini laini kama vile chakula cha watoto ambacho ni maziwa.

Usishangae mtu wa tabia ya mwilini akachukia Neno la Mungu, maana yake anauchukia ukweli, hataki kabisa uguse mambo yake anayoyafanya. Tofauti kabisa na mtu wa rohoni, mtu aliyekomaa kiroho mwenye uwezo wa kula chakula kigumu, anapokutana na ukweli yupo tayari kubadilika na sio kupingana na ukweli.

Nakueleza haya ili usiwe unapata shida na watu ambao chakula chao kikubwa ni chakula cha watoto wachanga, ambacho ni maziwa. Nakueleza haya ili pia uweze kujijua upo kundi gani, kama huwa ukiambiwa ukweli unakasirika na kuzira, uwe unajua wewe bado ni mtoto mchanga.

Rejea: Lakini, ndugu zangu, mimi sikuweza kusema nanyi kama na watu wenye tabia ya rohoni, bali kama na watu wenye tabia ya mwilini, kama na watoto wachanga katika Kristo. Naliwanywesha maziwa sikuwalisha chakula; kwa kuwa mlikuwa hamjakiweza. Naam, hata sasa hamkiwezi, kwa maana hata sasa ninyi ni watu wa tabia ya mwilini. Maana, ikiwa kwenu kuna husuda na fitina, je! Si watu wa tabia ya mwilini ninyi; tena mnaenenda kwa jinsi ya kibinadamu? 1 KOR. 3:1-3 SUV.

Umeona hayo maandiko matakatifu, tena watu wa tabia ya mwilini, wana husunda na fitina, ambazo huwa ni tabia za watu wasiomjua Kristo ila utakuta mtu ameokoka kabisa ila ana mambo kama hayo. Ukishaona hayo yote huyo ni mtu wa mwilini bado, tena ukijaribu kumkemea kwa tabia yake hiyo anaweza kukuchukia kweli.

Ukiona Mtu anapenda sana chakula cha watoto ambacho ni maziwa, yaani anapenda mafundisho laini laini ambayo yanamrembaremba hata kama anamtenda Mungu dhambi. Uwe na uhakika huyo mtu hana Neno la Kristo ndani yake, kwa sababu bado ni mtoto mchanga.

Rejea: Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya. EBR. 5:13-14 SUV.

Kutoka kwenye eneo hili la uchanga wa kiroho, tunapaswa kuipenda kweli ya Mungu, usikubali miaka yote tangu uokoke bado una tabia za mtoto mchanga. Lazima ufike mahali uamue kubadilika kweli kweli, kama unapenda kwenda mbinguni, lazima upende chakula cha watu wazima.

Jizoeze kusoma Neno la Mungu, jifunze kupenda mafundisho ya Neno la Mungu kupitia kwa watumishi wake. Utaanza kuona mabadiliko makubwa ndani yako, taratibu utaona upo tofauti kabisa na siku zilizopita.

Unaweza kuwachukia watumishi wa Mungu bure, kumbe tatizo ni lako mwenyewe, kubali kubadilika kuanzia sasa.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.