Kuna watu kuwaonya kwa maneno matupu anaweza asikusikie/asikuelewe kwa haraka, anaweza kusema nimekuelewa alafu kesho ukamkuta amerudia yale yale uliyomkataza jana. Ili aweze kuona ulichomkataza hakipaswi kufanywa, utatoka kwenye maneno ya mdomoni na kumpa adhabu kwa kosa alilofanya.
Kuna watu hawezi kufuata jambo bila kuwekewa sheria kali, pale atakapovunja utaratibu uliowekwa akutane na adhabu. Hapo ndio utamwona mtu anakuwa makini zaidi kwa kile alichoambiwa asikosee.
Wengi wetu tunaweza kuona adhabu ni kitu kibaya sana, ukaona sisi kama wakristo hatupaswi kujihusisha nacho kabisa ila nakueleza ukweli. Adhabu ina faida kubwa sana kuliko huzuni unayoweza kuipata/kuiona kwenye adhabu uliyopewa.
Adhabu inaweza kukufundisha mambo mengi ya msingi sana ukiwa unaitumikia hiyo adhabu, unaweza kuona kufungwa mtu gerezani ni vibaya sana kwako. Inaweza ikawa na faida kubwa kuliko mtu huyo angeachwa mtaani, kuachwa kwake huru angeendelea kuleta madhara makubwa zaidi katika jamii.
Adhabu inakufanya urejee katika njia sahihi, unaweza kumchukia sana aliyekupa hiyo adhabu ila ukiitazama hiyo adhabu kwa mtazamo chanya. Unaweza kuondoka na darasa kubwa sana na ukajiona una mabadiliko makubwa ndani yako kuliko ulivyokuwa mwanzo.
Ndio maana ukiwa kama mzazi hupaswi kumnyima mtoto wako fimbo, hupaswi kumlea mtoto wako kama yai, ukimzoesha kumlea hivyo. Utatengeneza kizazi kibaya kisicho na adabu, adhabu ni muhimu sana kwa mtoto wako, awe anajua nikifanya hili jambo nililokatazwa, nitachapwa.
Mtu kutengwa kanisani kutoshiriki baadhi ya mambo, wengi wetu tunaweza kuona ni jambo baya sana ambalo watumishi wa Mungu hawapaswi kulifanya. Usilolijua ni kwamba, hicho kitendo kinaleta heshima ya kanisa, watu wawe wanajua ukijulikana umefanya jambo fulani baya. Lazima utapewa adhabu ya kutengwa kanisani.
Kama nilivyotangulia kusema mwanzo bila kuwepo sheria/kanuni fulani zilizowekwa, na bila kuwepo na adhabu kwa atakayevunja hizo kanuni. Unaweza ukawa na kizazi kisicho na adabu, maana hakuna kitu kinachowarejesha pale wanapokosea. Adhabu ni moja ya silaha nzuri ya kumrejesha mtu pale anapoenda kinyume.
Unaweza kusema mbona pamoja na kuwepo adhabu kali, mbona kuna watu bado wanakosea, mbona watu wanazidi kutenda dhambi, hilo huwezi kuzuia ila adhabu zimesaidia wengi sana kumrudia Mungu wao. Kuna watu baada ya kupigwa na malaria kali iliyotaka kuwaondoa duniani, walimkumbuka Mungu wao na kurejea upya.
Ndio maana ni muhimu sana kuyafahamu maandiko matakatifu, unaweza ukawa na chuki na waalimu mashuleni wanaompa mtoto wako adhabu kali. Ukaona wanamwonea mtoto wako, kumbe wanafanya hivyo kumsaidia kumrejesha kwenye mstari ulionyooka kutokana na tabia yake mbaya aliyokuwa nayo.
Hebu tuone Neno la Kristo linasemaje kuhusu hili, uone ni jinsi gani hatupaswi kuichukia adhabu hata kama ina maumivu makali. Pia uone adhabu sio kitu kibaya kama ulivyokuwa unaitazama kwa upande mmoja.
Rejea: Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani. EBR. 12:11 SUV.
Umeona huo mstari, unasema hivi, adhabu huleta matunda ya haki yenye amani.Unaweza kuona sio kila adhabu kwako ina nia mbaya na wewe, adhabu zingine zinakusaidia ujutie makosa yako, adhabu zingine zinakukumbusha ulichokifanya sio kizuri, adhabu zingine zinakulazimisha kuacha tabia ambayo ulikuwa umeshindwa kuiacha kwa hiari.
Kuna methali moja inasema hivi, asiyefunzwa na mamaye hufunzwa na ulimwengu, ikiwa na maana yapo mambo ya msingi ambayo mzazi alipaswa amfundishe mtoto wake ila hakufanya hivyo. Kama hakufanya majukumu yake, Dunia itamsaidia kumweka mtoto wake katika mstari ulionyooka.
Nimalize kwa kusema, adhabu ipo kibiblia hupaswi kuichukulia kama kitu kisichofaa, popote utakapoadhibiwa japokuwa inauma sana. Hakikisha utaondoka na somo juu ya hilo lililokupelekea upewe adhabu, chukulia umelipia shule/mafunzo kwa gharama ya maumivu.
Haya yote utayafahamu zaidi ukiwa msomaji wa Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081