Tunaweza kukutana na mambo mengi ya kutuvunja mioyo yetu, ukafika mahali ukaona kila kitu ni kibaya kwako, ukawa unatamani kufa tu. Ukawa huoni tena maana ya kuendelea kuishi, hata kama machoni unaonekana unaenda kazini, lakini moyoni mwako unajua kabisa unaenda tu ila ndani yako umechoka, yaani ndani yako ukawa umekata tamaa kabisaa.

Hata kama kwa nje unaonekana unaenda kanisani, lakini ndani yako umechoka sana, unaenda tu kwa sababu unaogopa maswali ya mchungaji, ya kwanini hujaja ibadani siku nyingi. Ujitahidi kufika kwenye ibada ili uonekane bado ni mshirika hai ila moyoni umechoka, umevunjika moyo, huna tena tumaini katika maisha yako.

Watu wanakuona unaimba kwaya ila moyoni mwako unajua ulivyochoka, kwenye kwaya upo tu kutimiza wajibu ila kiuhalisia ndani ya moyo wako unajua ni kiasi gani umechoka. Unajua mwenyewe ni kiasi gani umerudi nyuma hatua kubwa sana, maana huoni tumaini tena, huoni nguvu ya Mungu ikiwa ndani yako, yapo mambo yamekuvunja moyo.

Umefika mahali ulikuwa unaenda kwa kujikongoja ila sasa umeona uache kabisa kufanya hivyo, umeona huna haja ya kuendelea kujikaza na wakati moyoni mwako unajua kabisa hufanyi vizuri. Unafanya ilimradi tu siku ziende, ndani yako hakuna msukumo wowote wa kufanya lolote, kwa sababu lipo lililokupelekea kuvunjika kwako moyo.

Siku za mwanzo ulikuwa mwombaji mzuri, ulikuwa na imani kubwa ndani yako, maana Mungu alikuwa anakutumia kuponya watu wake kupitia huduma yako ya uombaji. Mungu alikuwa anaponya watu wengi kupitia huduma yako ya uimbaji, Mungu alikuwa anaponya watu kupitia utumishi wako wa kuhubiri injili.

Uliona kweli Mungu anatenda, wasiozaa walizaa, waliolala vitandani kwa ugonjwa waliinuliwa tena, waliokata tamaa ya maisha na kutaka kujiua. Kupitia huduma yako Mungu aliyokupa, walipokea uponyaji ndani ya mioyo yao, walipata tumaini jipya la kusonga mbele baada ya kusikia Neno la Mungu likisema nao juu ya maisha yao.

Pamoja na kuona hayo yote Mungu akikutumia, lipo jambo Mungu hajafanya kwako, umeomba sana ila bado huoni tumaini lolote la kupokea jibu lako. Miaka mingi imepita ukiwa na tumaini Mungu atatenda na kwako ila umefika mahali ukaona hatendi tena, kuvunjika moyo kumeanza kukutesa maisha yako. Ule moto wa Roho Mtakatifu uliokuwa nao unazidi kushuka siku hadi siku, unaona unazidi kukaukiwa ndani yako.

Ulikuwa mwenye bidii sana ya kuomba, umefika mahali unaona hata kuomba haina haja tena, na kadri siku zinavyozidi kwenda mbele unatamani kufa na sio kuishi tena. Unaona ya nini kuendelea kuishi maisha ya mateso kama Mungu hasikii maombi yako.

Ulikuwa na matumaini makubwa ya kuolewa na mwanaume anayempenda Yesu Kristo, mwanaume anayemcha Mungu katika roho na kweli. Badala yake umekuwa mshuhudiaji wa wengine wakiolewa, uliokuwa ukishirikiana nao katika maombi, wote wameolewa na wengine wanaitwa mama sasa ila kwako imekuwa changamoto.

Umefika mahali unaona bora tu kuolewa na mwanaume yeyote atakayekuja mbele yako, Haitajalisha ameokoka ama la! Utaolewa naye tu. Umefika mahali unaona bora kuzaa na mwanaume yeyote hata kama hatakuoa, wewe unachohitaji ni kuitwa mama, maana umesubiria miaka mingi umeona imeshindikana.

Ulikuwa na matumaini ndoa yako itasimama upya tena baada ya kusambaratika, baada ya kutengana na mume wako muda mrefu, baada ya kutengana na mke wako muda mrefu. Umeomba sana Mungu airejeshe ndoa yako, siku za mwanzo ulikuwa na matumaini makubwa baada ya kuona wengine wakirudiana na waume/wake zao. Lakini kwako imekuwa ndoto, na huoni tena tumaini la kusimama tena kwa ndoa yako.

Hiyo yote ni kwa sababu umevunjika moyo wako, umechoka kiasi kwamba hutaki kusikia ushauri wa aina yeyote. Hata mafundisho ya Neno la Mungu hutaki tena kusikia, maana unaona hayana msaada wowote kwako, na hata Kusoma kwako Neno la Mungu umeona haina haja tena.

Ninalo neno la mwisho kwako, sitaki uangalie nini huko nyuma, nataka nikuambie INUKA TENA USONGE MBELE.Imetosha kulia, imetosha imetosha imetosha, Yesu Kristo amekuona, anakwambia inuka usonge mbele. Maneno haya aliambiwa pia mtumishi wa Mungu Elia, Elia alifika mahali akakata tamaa kama wewe, akawa anatamani kufa tu. Lakini sikia Mungu alivyomwambia;

Rejea: Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee BWANA, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu. Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule. Akatazama, kumbe! Pana mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akajinyosha tena. Malaika wa BWANA akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako. Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu. 1 FAL. 19:4‭-‬8 SUV.

Sijui umechoka kiasi gani, Bwana anakwambia inuka ule, bado una safari ndefu sana, bado hujamaliza kazi aliyokuletea hapa duniani, bado hujafika viwango alivyovitaka Mungu ufikie. Mungu anajua hitaji lako, ndio maaana anasema hivi; Ombeni bila kukoma. 1 THE. 5:17 SUV.

Mbona wewe umekoma, mbona wewe umeacha kuomba, mbona imani yako imekutoka? Ni kwa sababu Neno la Mungu lilikupungukia ndani yako, rudi tena usimame na Mungu wako kisawasawa, Neno la Mungu linasema INUKA.

Moyo wako uliokata tamaa, uinuliwe tena, ukaona furaha ya wokovu wako, ukajione wewe ni mshindi wa washindi, maana unaye Yesu Kristo aliyeshinda kifo na mauti. Kwanini wewe unajiona u mshindwa? Wewe sio mshindwa, wewe ni mshindi katika jina la Yesu Kristo aliye hai.

Mungu akubariki sana.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.