Kipindi nimeamua kuokoka, niliwaweka wazi baadhi ya marafiki zangu niliokuwa nao karibu. Nilijiweka wazi kwao na kuwaambia kuanzia sasa sitaki mambo ya kipuuzi, mwanzo waliona kama nawatania, na wengine wakaona kama vile naigiza tu. Baadaye walianza kuelewa kuwa nilimaanisha kile niliwaeleza, kadri siku zilivyozidi kwenda mbele baadhi yao waligeuka maadui zangu.
Hilo halikunipa hofu, wala halikunifanya nione uamzi niliochukua haukuwa uamzi sahihi, sikuwahi kuficha wokovu wangu. Mtu yeyote atakayekuja kunieleza habari chafu, nilikuwa na ujasiri wa kumwambia siwezi kusikiliza/kufanya/kushiriki hilo jambo. Namweleza wazi kabisa mimi nimeokoka, na wakati mwingine nilikuwa najitenga nao kabisa.
Nilikuwa najivunia sana kuokoka kwangu, tena nilikuwa naona fahari kubwa mno, tena cha kushangaza zaidi kujiamini kwangu kuliongezeka mara ndufu. Nikawa natamani kila mtu amjue Yesu wangu, ili na yeye aweze kuacha dhambi na kumgeukia yeye, ambavyo natamani hadi sasa watu wamjue Yesu Kristo.
Nimekusimilia ushuhuda wangu kwa kifupi baada ya kuokoka nilikuwaje, na kama umekuwa rafiki yangu wa muda mrefu utakuwa umeona mengi na kujifunza mengi kupitia masomo mbalimbali. Na kama ndio mara yako ya kwanza kusoma ujumbe huu, usiwe na shaka, lipo jambo unaenda kujifunza kupitia somo hili.
Ninavyojua mimi, mtu yeyote anayechanganya wokovu na dhambi, hawezi kuwa na ujasiri wa kusema ameokoka mbele za marafiki/ndugu wanaomfahamu vizuri. Haijalishi ni mhudhuriaji mzuri wa ibada za kanisani, kama njia zake ni chafu huyo mtu hawezi kuwa na ujasiri wa kusema yeye ameokoka kwa watu wanaomfahamu vizuri.
Lakini ninachoshangaa siku hizi, wengi wanaokoka ila wanakuwa hawana ujasiri wa kusema mbele za watu kuwa wameokoka. Mtu anakuwa ameokoka kweli, nikiwa na maana ameachana na mambo ya Dunia, yaani akiwa ameamua kujitenga na dhambi. Mtu huyu anakuwa haeleweki, hata nyumbani kwao wanaweza wasijue kama ameokoka, hata ofisini kwao wafanyakazi wenzake wanaweza wasijue chochote.
Mtu wa namna hii anakuwa kawaida, ukimuuliza ndugu si umeokoka? Anaweza kukukataa wazi mbele za watu, anakuwa hajiamini na kile amekiamini, hajiamini kama yeye amekuwa mtoto wa Mfalme(Yesu Kristo). Muda mwingine hataki kabisa Yesu wake ajulikane, kwa kifupi anajisikia vibaya kumweka Yesu wake bayana.
Kuna mahali nilienda kufanya kazi, wakati najaza mkataba, mkataba ule ulikuwa unapaswa kufanya kazi hadi siku za jpili. Nilimweleza wazi kabisa mwajiri yule, siwezi kufanya kazi jpili, kama hawezi kuniachia siku ya jpili nikakusanyike pamoja na wenzangu sitakuwa tayari kufanya naye kazi. Alinielewa kabisa na tukafanya naye kazi.
Wengi wetu tunamkana Yesu wetu huko makazini, kwenye biashara zetu, kwa wazazi/walezi wetu, na mashuleni/vyuoni mwetu, hatupendi kujulikana kwa watu kuwa sisi ni wa upande gani. Kama hukujua hili jambo lina madhara makubwa sana kiroho, tena ni dhambi kubwa sana mbele za Mungu, unaenda kujua sasa.
Hebu tutazame Neno la Mungu linasemaje kuhusu hili, huenda ulikuwa unachukulia jambo hili kawaida. Leo unaenda kufahamu sio jambo la kawaida, leo unaenda kupata ukweli sahihi kupitia Neno la Mungu. Mwongozo wetu tuliolikiri jina la Yesu Kristo aliye hai ni Neno la Mungu, hatuna katiba/mwongozo mwingine wa maisha yetu ya kiroho isipokuwa Neno la Mungu.
Rejea: Basi, kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni. Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni. MT.10:32-33 SUV.
Umeona hilo andiko takatifu? Yesu anasema ukimkana mbele za watu na yeye atakukana mbele za Baba yake mbinguni. Na wote tunafahamu mbinguni hatutaingia bila kuliamini jina la Yesu Kristo, sasa unaposhindwa kumkiri Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wako. Unakuwa unajikosesha mbingu mwenyewe, maana Yesu akishakukataa huna nafasi nyingine ya kuingia uzima wa milele.
Wakati mwingine unaweza kumwambia mpendwa “Bwana Yesu asifiwe”akashindwa kukujibu kwa ujasiri. Usipomzingatia vizuri hawezi kukujibu, kisa umemsalimia mbele za watu wengi, kisa umemwambia mbele za marafiki zake. Huyu mtu anazuia nini? Lazima kuna kitu hakipo sawa.
Hupaswi kumwonea haya Yesu Kristo, popote unapokuwa matendo yako, tembea yako, na zungumza yako, inapaswa kukutambulisha kwa watu wewe ni mtoto wa Mungu. Mtu akija kukuuliza umeokoka ndugu, hupaswi kuwa na mashaka, unapaswa kumjibu NDIO, hapo ndipo utamuuliza kwanini unauliza hivyo.
Rejea: Kwa sababu kila atakayenionea haya mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wake na wa Baba na wa malaika watakatifu. Lk. 9:26 SUV.
Mweleze bayana mtu habari za Yesu Kristo, abaki yeye kuchagua, acha kuonea haya injili, lazima ujitofautishe wewe ni wa namna gani. Ndio maana hata vaa yako inapaswa kufanana na mtu aliyeokoka, kama vaa yako itafanana na asiyemjua Yesu Kristo, huwezi kujivunia Yesu wako.
Lazima tustahimili kejeli za watu, lazima tustahimili kukataliwa kwetu na ndugu, marafiki, na jamaa mbalimbali. Bila kuwa wastahimilifu, utashangaa uliokoka vizuri, baada ya kukutana na misukosuko mingi ukajikuta unarudi nyuma.
Rejea: Kama tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana sisi; 2 Tim. 2:12 SUV.
Haijalishi watu wanakupinga sana, chunga sana usije ukavunjika moyo, haijalishi utafika mahali utakataliwa usifike mahali ukasema wokovu basi. Jikubali wewe kama wewe ukijua uliyenaye ni Mkuu sana, na atakufungulia njia nyingi na hakuna kitachokudhuru.
Nimalize kwa kusema, wewe ni wa thamani sana mbele za Mungu, hata katika ulimwengu wa giza wanalitambua hilo. Ndio maana shetani anajaribu kukutisha ili uweze kurudi ulipokuwa, hakikisha humwonei haya Yesu wako popote utakapokuwa.
Mungu akubariki sana.
Email: chapeo@chapeotz.com
Blog: www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.