Kuwa na uhakika Mungu yupo pamoja na wewe ni jambo lingine, na kusema umeokoka ni jambo lingine kabisa. Wengi wetu tunasema tumeokoka ila mioyoni mwetu tumejaa mashaka/hofu ya kwamba Mungu anaweza kutusaidia au hawezi kutusaidia.
Imani zetu hazipo imara kwenye kumwamini sana Mungu, ndio maana wakati mwingine tunakuwa rahisi kutoka katika njia sahihi ya Bwana. Na kuelekea katika njia isiyo sahihi, inayomchukiza yeye Mungu.
Kukiri jina la Yesu Kristo aliye hai kama Bwana na mwokozi wa maisha yako, na kuishi maisha matakatifu yanayompendeza Mungu. Alafu ukawa huna uhakika/imani ndani yako kuwa wewe ni mtoto wa Mungu na ulinzi wa Mungu u juu yako. Hilo ni tatizo lako mwenyewe ambalo linatokana na kukosa Neno la Mungu moyoni mwako.
Wale walio na Neno la Mungu ndani yao, wanao uhakika mkubwa ya kuwa Mungu yupo pamoja nao. Hata wanapopitishwa kwenye majaribu mazito, imani zao huwa hazitetereki zaidi zinakuwa zipo pale pale mbele za Mungu.
Sababu haswa zinazowafanywa wawe na imani isiyotetereka mbele za Mungu, ni kule kulijua Neno la Mungu linalinasemaje juu ya maisha yao. Wanajua kabisa pamoja na tunapita katika changamoto nzito za maisha yetu, yupo Baba yetu aliye mbinguni anatuona na mkono wake u juu yetu.
Mtu aliyeshiba Neno la Mungu sawa sawa hawezi kufika mahali akaanza kufikiri kumwacha Yesu Kristo, kwa sababu za aina yeyote ile. Atakutana na vikwazo vizito sana ila utamkuta amesimamia imani yake mbele za Mungu.
Haya ninayokueleza hapa tunapata kuyajua kutoka kitabu kitakatifu cha Biblia, kinatueleza wazi kabisa jicho la Mungu lipo kwa wale wamchao. Wale ambao maisha yao yapo salama mbele zake, yaani hawajichanganyi na maovu ya dunia hii.
Rejea: Tazama, jicho la BWANA li kwao wamchao, Wazingojeao fadhili zake. ZAB. 33:18 SUV.
Hebu ona nafasi yako ilivyo kubwa mbele za Mungu, huwi na uhakika hivi hivi, unakuwa na uhakika kwa sababu umelijua Neno la Mungu linavyosema juu ya maisha yako.
Huenda ulifika mahali ukaona Neno la Mungu si kitu sana kwenye maisha yako, uwe na uhakika wazo hilo limetoka kwa mwovu shetani. Maana anajua madhara ya wewe kulijua Neno la Mungu, madhara yake kwake ni wewe kutokumtenda Mungu dhambi.
Ukiwa mwenye haki wa Mungu, uwe na uhakika jicho la Mungu li juu yako. Hata kama unapita mahali pagumu sana, Mungu anajua kwanini unapitia hayo, na jaribu haliwezi kukuzidi uwezo wako ulionao ndani yako. Kuwa mvumilivu huku ukiwa na uhakika Mungu yupo pamoja nawe.
Rejea:Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. ZAB. 34:15 SUV.
Kilio chako mbele za Mungu kinasikilizwa sana kwake, kitendo cha kuwa mwenye haki wake, yaani mtu unayemcha Mungu katika roho na kweli. Macho ya Mungu yatakuwa kwako kwa asilimia zote, tena kilio chako mbele zake kinasikika masikioni mwake.
Umeona ni jinsi gani Neno la Mungu lilivyo na nguvu ya kutujaza imani kadri linavyozidi kuingia mioyoni mwetu. Unaweza kuona vile ulivunjika moyo baada ya kusoma mistari hii michache, unasikia kuinuka tena. Je! Ukiwa unasoma zaidi ya mstari mmoja si utakuwa imara zaidi? Usiache Kusoma Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Blog: www.chapeotz.com
Email: chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081