Kuna hali tukiwa kama wakristo wenye safari ya kwenda mbinguni, na walio na jukumu la kuzaa matunda mema kwa Mungu. Hatupaswi kupuuza baadhi ya hali tutakazoziona kwetu, kuzipuuza hizo hali zinatufanya tuendelee kujiona wanyonge.
Kuwa na woga uliopitiliza hadi kwenye mambo ya msingi, hadi kwenye kushindwa kudai haki zako za msingi, hadi kwenye kushindwa kufanya vizuri huduma aliyokupa Mungu ndani yako. Huo sio uoga wa kuchukulia kawaida, lazima ukae chini na kufahamu nini kinakusababisha uwe hivyo.
Kama umeokoka alafu huna ujasiri wa kukiri wazi kwa marafiki zako, ndugu zako, majirani zako, wafanyakazi wenzako, na wanafunzi wenzako, kuwa umeokoka, na maisha yako yanampendeza Mungu. Na hakuna mahali umekaa vibaya, hiyo hali ya woga hupaswi kuipuuza hata kidogo.
Kama umeokoka vizuri kabisa, ukisikia habari ya kuombea mgonjwa mwenye pepo wabaya. Ghafla ndani yako unasikia woga na hofu kubwa, hiyo sio hali ya kuacha hivi hivi iendelee kukusanyanyasa ndani yako.
Tulivyompokea Yesu Kristo kama Bwana na mwokozi wetu, hatukupokea roho ya woga, bali tulipokea nguvu, tulipokea upendo, na moyo wa kiasi.Kama umeokoka umejaa woga, huna nguvu za kiMungu ndani yako, huna upendo wowote ndani yako, na huna moyo wa kiasi. Ukristo wako una walakini, unapaswa kuchukua hatua ya kumwomba Mungu au kutafuta msaada wa maombi kwa watumishi wa Mungu.
Rejea:Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. 2 TIM. 1:7 SUV.
Kama umejulikana huna tatizo lolote la kiroho, yaani hakuna nguvu zozote za giza zinazokufanya uwe na woga mbele za Mungu na mbele za watu. Shida Yako itakuwa kukosa maarifa ya kiMungu ndani yako.
Tumesoma andiko takatifu linasema hatukupewa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. Ukiwa na mambo haya matatu, yaani nguvu/ujasiri, upendo, na moyo wa kiasi, wewe mwana wa Mungu kweli kweli. Maana roho wa woga hayumo ndani yako.
Rejea: Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi. 2 TIM. 1:7 SUV.
Ni ajabu sana unasema umeokoka alafu huna nguvu za kiMungu ndani yako, huna moyo wa upendo, na huna moyo wa kiasi, tunakuwa na wasiwasi na wokovu wako. Maana ukiwa na roho ya woga ndani yako, huwezi kumweleza mtu habari za Yesu Kristo, huwezi kumshudia mtu akaokoka.
Ukiwa na roho ya woga, huwezi kukemea dhambi wazi wazi, upo tayari kutetea uovu ili usionekane mbaya. Wakati mwingine unaweza kujiona kufanya hivyo ni hekima, kumbe ni roho ya woga iliyo ndani yako.
Ukiwa kama mkristo, alafu ukawa huna upendo kwa watu, kama umeoa ukawa humpendi mke wako, utakuwa bado hujampokea Yesu Kristo sawasawa. Unaishi na majirani zako kwa chuki, huna upendo wowote juu yao, huo sio wokovu.
Umeokoka alafu huna moyo wa kiasi, unafanya vitu mpaka wale wasiomjua Kristo wanakuwa wanaona kabisa kama ni kuokoka na wao watakuwa wameokoka. Ujue una mapungufu ndani yako, upungufu ambao unapaswa kupata msaada haraka sana.
Neno la Mungu linatusaidia kufahamu haya, kama ulikuwa na roho ya woga, kuanzia sasa ikatae kwa kupenda mafundisho ya Neno la Mungu. Na ikatae kwa kupenda kusoma Neno la Mungu, kama huwezi kupenda kusoma Neno la Mungu, jilazimishe kujizoeza tabia ya kusoma Neno la Mungu.
Yapo mambo tunafanya tunafikiri ni utakatifu kumbe ni kutojua kwetu, mtu yeyote aliyeokoka na akalifahamu Neno la Mungu. Lazima mtu huyo atakuwa jasiri, mtu asiye na woga mbele za watu inapofika suala la imani yake.
Kuanzia sasa fahamu kwamba Mungu hajatupa roho ya woga, ametupa nguvu, upendo na moyo wa kiasi. Hakikisha una vitu hivi ndani yako.
Mungu akubariki sana.
Chapeo Ya Wokovu
www.chapeotz.com
chapeo@chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081.