Yapo maswali mtu anauliza sio kana kwamba anataka kujifunza na kupata mwanga kwa kile ambacho alikuwa hakifahamu, wengine wanauliza maswali kuharibu amani uliyokuwa nayo. Kwa kuibua mabishano makali ambayo mwisho wake mtaishia kugombana na kutupiana maneno mabaya.

Wengi tumekuwa tukijiingiza kwenye mabishano makali na yanayoibua magomvi, kwa akili ya kawaida unaweza kujiona upo sawa ila mbele za Mungu haupo sawa. Mtu wa Mungu hupaswi kuwa mgomvi, anapaswa kuwa mtu mwenye busara na hekima nyingi pale anapozungumza jambo.

Tunapokuwa wagomvi, hata wale ambao walikuwa bado hawajamjua Kristo, wanaanza kuona haina haja ya kuokoka. Maana aliyeokoka mwenyewe ni mtu wa magomvi, mtu ambaye hakubali kujishusha, mtu ambaye anajiingiza kwenye mijadala ya maswali yasiyo na la kujifunza ndani yake zaidi ya magomvi.

Lazima tuwe na akili, hatupaswi kujibu kila swali tunaloulizwa, hatupaswi kushiriki kila midahalo yenye maswali ya upumbavu. Maana mpumbavu hayupo tayari kujifunza, yupo tayari kubishana tu, ukikasirika au mkikasirika na kuanza kugombana, kwake ni furaha.

Sasa wengi wetu tuliokoka, tumekataa kumsikiliza Roho Mtakatifu pale anapotuonya kuhusu maswali yasiyofaa. Badala yake tumejiingiza kwenye mijadala isiyofaa kabisa, mijadala ambayo mwisho wake imezaa magomvi makubwa.

Sisi tulioamini na kukubali kumpokea Kristo kama Bwana na mwokozi wetu, tunapaswa kuwafundisha wale wasioijua kweli, tena tunapaswa kuwa wavumilivu, tukiwaonya kwa upole wale wanaoshindana nasi. Ili ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli.

Badala kuwa waonyaji, badala kuwa watu wanaofundisha, badala kuwa wavumilivu, tukiwaonya kwa upole wale wanaoshindana nasi. Tumekuwa watu wa magomvi, tusiokubali kushindwa, bila kujua tunachofanya ni kupoteza muda. Maana wale tunaoshindana nao, hawapo tayari kubadilika, maswali yao hayana lengo la kujifunza na kubadilika.

Hata kama unajua kweli sawa sawa, kuwa makini, na epuka maswali yasiyofaa, yaani maswali yanayoibua magomvi. Kama unajibu hayo maswali uwe unafahamu hayo, ili usije ukajiingiza kwenye magomvi na watu wasiomjua Kristo sawasawa.

Utasema sisi kama wakristo tuliojua kweli hatupaswi kuogopa hayo, wala kujiepusha na hayo, ni kweli maana sio mara zote utamjua haraka muuliza swali. Pale unapojua muulize swali nia yake sio kuelewa bali ni kutaka mabishano tu ambayo mwisho wake ni magomvi, achana na huo mjadala.

Kama hutoachana na mjadala huo, eleza yale ya msingi, alafu jitoe kwenye mjadala huo. Usijiweka kwenye mjadala huo muda mrefu kwa kusudi la kutoonekana umeshindwa, wengi huwa hawataki kuachana na mabishano fulani makali kwa lengo la kutoonekana ameshindwa. Ukijiona upo hivyo fahamu hiyo ni hali ya uchanga wa kiroho, au hali ya mtu asiye na Neno la Mungu la kutosha moyoni mwake.

Haya ninayokueleza hapa, Neno la Mungu linatuelekeza hivyo, tuyakatae maswali ya upumbuvu, maswali yanayoibua magomvi katikati yetu. Maana tuliokoka hatupaswi kuwa watu wa magomvi.

Rejea: Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi. Tena haimpasi mtumwa wa Bwana kuwa mgomvi; bali kuwa mwanana kwa watu wote, awezaye kufundisha, mvumilivu; akiwaonya kwa upole wao washindanao naye, ili kama ikiwezekana, Mungu awape kutubu na kuijua kweli; wapate tena fahamu zao, na kutoka katika mtego wa Ibilisi, ambao hao wametegwa naye, hata kuyafanya mapenzi yake. 2 TIM. 2:23‭-‬26 SUV.

Waambie watu ukweli, usijiweke kwenye nafasi ya kumlazimisha/kuwalazimisha wakuelewe au wakubaliane na wewe na kile unawaeleza. Unapojiweka kwenye nafasi ya kulazimisha wakuelewe, alafu na hao unaotaka wakuelewe hawana mpango huo. Uwe na uhakika unatafuta magomvi.

Mwelimishe mtu, pale unapopata nafasi ya kufanya hivyo au unapopata kibali moyoni mwako, abaki yeye sasa afuate kile umemwambia au aachane kabisa na kile umemwambia. Cha msingi wewe umetimiza wajibu wako, mengine unamwachia Mungu mwenyewe.

Narudia tena, usijiingize kwenye mijadala/maswali ya kipumbavu, utagombana sana na watu bila kuzaa matunda yeyote. Tumia akili sawasawa, usiwe kama mtoto mchanga asiyejua kitu, uwe mtu mzima kwenye akili zako.

Mungu akubariki sana.

Chapeo Ya Wokovu

chapeo@chapeotz.com

www.chapeotz.com

+255759808081.