Nafasi nyingi tunazopata, wengi wetu huwa tunazitumikia hizo nafasi kwa mkono mlegevu sana, wengi wetu huwa hatuna moyo wa kulifanya hilo jambo. Tunakuwa tunafanya ilimradi tunafanya ila mioyoni mwetu hatuna ule msukumo kabisa wa kulifanya hilo jambo.

Unakubali mwenyewe kwenda kuomba kazi mahali fulani, kazi unaipata vizuri, lakini baada ya muda fulani unakuwa unaifanya kazi hiyo kama kuna mtu alikulazimisha kwenda kuiomba hiyo kazi. Hata ufanyaji wako wa kazi humshawishi mtu kabisa, maana yake unafanya kwa viwango vya chini sana.

Unapewa nafasi ya uongozi mahali, vile uliahidi, na vile watu walikuamini utawaongoza vizuri, inakuwa tofauti kabisa. Unafanya vizuri siku za mwanzo ila baada ya muda fulani kupita, ule moyo wa uongozi unatoweka, unakuwa hupatakani hata pale watu wanapokuhitaji uwasaidie jambo kwenye nafasi yako.

Unafungua biashara yako vizuri, siku za mwanzo ulikuwa unawakaribisha wateja vizuri, ulikuwa makini na kile unauza. Baada ya kuanza kupata wateja wengi kwenye huduma/bidhaa zako, ule moyo wa kujali wateja unaanza kupungua. Unaanza kuhudumia kama vile unalazimishwa na mtu kufanya hiyo biashara.

Mambo ni mengi sana inategemeana na wewe umekabidhiwa jambo gani ulifanye, inategemeana na nafasi gani umeipata. Pia unajua wewe mwenyewe hapo ulipo una nafasi gani katika jamii inayokuzunguka, inaweza ikawa ni nafasi ya eneo la kiroho au kimwili.

Wengi wetu huwa hatuna ule moyo wa kuzitumikia nafasi zetu tunazozipata, na wachache wanaojitoa kwa moyo wote kufanya yale majukumu yao waliyokabidhiwa au waliojitoa kufanya wanaoonekana ni watu wa kipekee sana.

Wengi hasa tunaofanya vibaya ni pale tunapoajiriwa au kuchaguliwa kuwatumikia watu, huwa tunaona sio jambo la kwetu. Ndio pale utasikia mtu akisema hivi, kazi hii sio ya baba yangu, maana yake hapo ameajiriwa tu kwa muda au amechaguliwa kukaa katika nafasi hiyo kwa muda tu.

Leo nataka ubadili mtazamo wako hasi, kama ulikuwa na mtazamo huo usiofaa, kuanzia sasa unapaswa kukataa hiyo hali kama utaona vyema kufanya hivyo. Hakuna atakayekulazimisha ila Neno la Mungu linatuelekeza hili ninalokueleza hapa, utabaki uamzi wako kuchukua hatua au kuacha.

Bora kuamua kufanya jambo au kukataa kabisa kufanya jambo hilo, kuliko kukubali kufanya jambo fulani alafu ukalifanya chini ya kiwango. Bora kukataa nafasi unayotaka kuchaguliwa, kuliko kukubali kuchaguliwa alafu ukaitumikia nafasi hiyo kwa uzembe mkubwa.

Rejea: Lo lote mfanyalo, lifanyeni kwa moyo, kama kwa Bwana, wala si kwa wanadamu, mkijua ya kuwa mtapokea kwa Bwana ujira wa urithi. Mnamtumikia Bwana Kristo. KOL. 3:23‭-‬24 SUV.

Hii ndio faida ya kujenga nidhamu ya kusoma Neno la Mungu kila siku, unaweza kupata nafasi ya kujua haya kupitia maandiko matakatifu. Wakati mwingine unaweza kufikiri kufanya jambo lolote kwa mkono mlegevu ni vizuri ila Neno la Mungu likawa linapingana na wewe.

Hili linaingia hata kwa msomaji wa Neno la Mungu, kama umeamua kusoma Neno la Mungu kila siku, fanya hivyo kwa moyo wote sio kwa sababu kuna mtu atakulipa. Fanya hivyo kwa ajili ya Bwana, fanya hivyo kwa faida yako mwenyewe, na kama unasoma ilimradi na wewe uonekane unasoma. Afadhali kuachana kabisa na hilo zoezi.

Umeamua kumtumikia Mungu, mtumikie haswa bila kuangalia mambo mengine, atakayekulipa kwenye utumishi wako ni Mungu mwenyewe. Fanya kwa Bwana, ukifanya kwa Bwana hutoangalia watu watakulipa shilingi ngapi, utafanya kwa sababu ni wito wako.

Narudia tena, lolote upatalo nafasi ya kulifanya, lifanye hilo jambo kwa moyo wote, sio kutafuta sifa, ni kwa sababu ni agizo la Mungu linakutaka ufanye hivyo. Kufanya kwako kwa moyo wote, unalifanya jina la Yesu Kristo litukuzwe kupitia wewe.

Amua Kufanya au Amua Kutofanya Kabisa, huwezi kufanya sema huwezi, unaweza kufanya sema naweza, na fanya kwa moyo wote, na fanya kwa bidii zote.

Mungu akubariki sana.

Samson Ernest.

Email: chapeo@chapeotz.com

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.