Ongezeko la mafundisho yasiyofaa kwa kanisa, watumishi kujikita zaidi kwenye mafundisho yasiyolifaa kanisa. Mafundisho ambayo hayawafanyi watu wamrudie Kristo, mafundisho yanayowafundisha watu wafanikiwe zaidi kimwili huku Rohoni wakizidi kuwa maskini wakutupwa.

Mafundisho ambayo yanakwepa kukemea dhambi, mafundisho yanayowafanya watu waone matendo mabaya wanayofanya. Waone ni matendo ya kawaida ambayo hayawezi kumzuia mtu kuingia mbinguni, na washirika wao wakitaka kupandikizwa kweli ya Mungu. Wanakuwa wapo nao makini kuwalisha mafundisho yasiyofaa.

Mafundisho ambayo yanayowafanya washirika waone kila mavazi yanafaa kuvaliwa, hawana mipaka yeyote kwenye mavazi. Wamewalea washirika wao hivyo na hawataki mtu mwingine awafundishe nje na wao wanavyowafundisha.

Washirika wao ukiwakuta mahali wanasikiliza mafundisho tofauti na waliyolishwa, sikiliza yao ipo tofauti kabisa na mtu mwingine. Sio ajabu kumkuta mshirika anaduwaa tu, na akishapata fundisho tofauti na alivyomezeshwa. Ametengenezewa mazingira ya kwenda kuuliza kwa kiongozi wake.

Sio vibaya kuuliza ikiwa upo sehemu sahihi unapokutana na mafundisho ya kukupotosha, inakuwa vibaya kama upo sehemu isiyo sahihi. Alafu ukapata mafundisho sahihi, mafundisho hayo sahihi ukayatilia mashaka makubwa.

Lengo la mtumishi au mwalimu huyu kufundisha yasiyofaa ni nini? Lengo linakuwa kupata fedha. Fedha ndio zinamfanya mtu huyo afundishe vitu visivyofaa, maana anajua akifundisha yanayofaa, atakuwa na washirika wachache. Anaona atachelewa kupata idadi kubwa ya watu ambao watamfanya apate fedha nyingi za haraka.

Hata hawa watu wanaoinuka na kuadhisha huduma, wengi wao sio kana kwamba wameitwa na Mungu, wengi wao sio kana kwamba wana wito wa kiMungu ndani yao. Wengi wao wanaadhisha huduma kwa sababu ya maslahi yao binafsi ya kuingiza kipato na sio kuwaleta watu kwa Yesu Kristo.

Kuongezeka kwa manabii kwa kasi kubwa, kila mtu anayeinuka kwa huduma anajiita nabii, wengine wanajipachika majina ya nabii mkuu. Wapo wengine wanajipachika vyeo vya mtume mkuu. Anawaona manabii wengine wote ni wadogo, yeye mkubwa, na mwingine anawaona mitume wengine wote ni wadogo, yeye ni mkubwa.

Yote hii ya kujipachika majina makubwa ni kwa sababu gani? Yote hii tamaa za pesa kutaka kuonekana wapo juu ili wawapate watu vizuri. Kuinuka kwa manabii wengi wa kubashiria watu mambo ya uongo, kufanya miujiza ya ajabu ajabu, mafuta ya upako, vitambaa vya upako, maji ya upako, na mengine mengi ya kufanana na hayo. Hii yote ni kutafuta pesa, yaani ni biashara kwao. Ndio maana hivi vitu havifanyiki bure, vinafanyika kwa fedha.

Utasema haya mambo umeyatoa wapi Samson, yapo ndani ya biblia, Neno la Mungu linatufunulia haya yote. Hizi mbinu chafu za manabii wa uongo wanaoibuka kila siku, ni mawakala wa shetani sawa ila kazi yao kubwa ni kutafuta pesa bana kuwafanya wasijue kweli ya Kristo.

Rejea: Wakuu wake huhukumu ili wapate rushwa, na makuhani wake hufundisha ili wapate ijara, na manabii wake hubashiri ili wapate fedha; ila hata hivyo watamtegemea BWANA, na kusema, Je! Hayupo BWANA katikati yetu? Hapana neno baya lo lote litakalotufikia. MIK. 3:11 SUV.

Tumepata ujumbe mwingine hapo wa viongozi, wapo viongozi wanatumia nafasi zao vibaya, kuwababikia watu kesi kwa lengo la kutaka kupewa rushwa. Wakijua mtu mwenye fedha hawezi kukubali kufungwa kwa kosa lisiloeleweka.

Nimekuambia tamaa ya fedha imewafanya manabii wengi wanaoibuka kila siku, huwezi kukosa hivi vitu, mafuta ya upako, maji ya upako, vitambaa vya upako, na mengine mengi ya kufanana na hayo. Haya yote huwezi kuyapewa bure, lazima utoe fedha watakayokuambia wao.

Usishangae watu kuambiwa kunywa pombe kwa mkristo sio tatizo, usishangae watu wakifundishwa kuvaa mavazi yeyote hata yasiyofaa hayawezi kumzuia mtu kuingia mbinguni. Maana lengo lao ni kuendelea kuwashikilia watu wengi zaidi, ili mapato yao yawe juu zaidi.

Rejea: Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu. TIT. 1 :11 SUV.

Kuyajua haya ni mpaka uwe na Neno la Mungu moyoni mwako, huwezi kujua mahali ulipo unapotoshwa kama huna Neno la Mungu moyoni mwako. Muhimu sana kuwa na Roho Mtakatifu, Roho Mtakatifu atakusaidia kuelewa vizuri yale unasoma, ataendelea kukufundisha zaidi kadri unavyozidi kutafakari yale umejifunza ndani ya biblia.

Jambo lingine la msingi, hakikisha unamwomba Mungu akufungue ufahamu wako, hili ni la msingi sana. Ndio maana nakusisitiza usome Neno la Mungu, na Neno la Mungu linakutaka ufahamu wako uwe umefunguka. Zaidi ya hapo utakuwa unasoma Neno la Mungu kama gazeti.

Nimalize kwa kusema hivi, soma Neno la Mungu kila siku, na pata muda wa kutafakari yale uliyojifunza kwa kusoma Neno la Mungu. Taratibu utaanza kuona mambo yanayofanyika mahali ulipo yapo kinyume na Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

Blog: www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081.