Katika maisha unaweza kufika mahali ukavunjika moyo au ukavunjwa moyo na jambo fulani ambalo ulikuwa unalifanya likafeli. Au kuna kitu ulikuwa unakitegemea kikaharibika/kikaharibiwa.

Unaweza ukawa ulikuwa na matumaini makubwa kwa jambo fulani ila ikafika mahali matumaini yale makubwa yakaanza kufifia, kutokana na vile siku zinavyozidi kwenda mbele ukawa huoni matokeo yeyote mazuri kwenye hilo jambo.

Inaweza ikawa juu ya afya yako, mwanzoni ulikuwa na matumaini makubwa ya kupona ugonjwa uliokuwa unakusumbua. Lakini kadri siku zilivyozidi kwenda mbele na ukawa huoni mabadiliko yeyote ya kupona, ndani yako yale matumaini uliyokuwa nayo yanaweza yakapungua au kuisha kabisa.

Kama ni mwanamke unaweza ukawa ndani ya ndoa mwaka wa pili au wa tatu sasa au zaidi ya hiyo, huoni dalili ya kupata mtoto hadi umefika mahali ile imani au matumaini uliyokuwa nayo yameanza kufifia. Lakini mwanzoni ulikuwa na ujasiri mkubwa wa kuona Mungu atakupatia mtoto.

Kama umefika mahali fulani umeanza kuona kama imani yako inapungua, umeanza kuchoka, umeanza kuzimia moyo wako. Huoni tena matumaini ya kupokea kile ulitarajia kukipokea kutoka kwa Mungu wako, Mungu yule yule anao uwezo wa kukupa nguvu mpya za kuendelea mbele.

Rejea: Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. ISA. 40:29 SUV.

Neno la Mungu ni pumzi ya Mungu mwenyewe, akisema amesema, hakuna jambo litakalopindishwa. Kama umefika mahali umechoka, huoni tena matumaini ya kupokea kile ulikitarajia kutoka kwa Mungu, Neno la Mungu linatuambia Mungu huwapa nguvu wazimiao.

Sijui umezimia na nini, lakini amini Neno la Mungu lisemavyo, amini unaenda kuinuliwa tena, na lichukue hili Neno na uliamini kuwa ni lako. Utaona nguvu mpya ikianza kukuhuisha ndani yako.

Ule uwezo wako uliopaswa kuwa nao, alafu ukawa huna au ukawa umepotea, Neno la Mungu linasema hivi; …humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. ISA. 40:29 SUV.

Amini sasa tayari imekuwa kwako, usiangalie hali uliyokuwa nayo dakika au siku chache zilizopita, wala usijiulize itakuwaje, wewe litazame na liamini Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.