Unaweza ukawa kuna kitu kibaya katika maisha yako ya wokovu hukitamani kukifanya kabisa ukiwa kama mkristo, lakini unajikuta unakifanya hicho kitu. Hicho kitu kinaweza kukusumbua kwa muda mrefu, mwisho wake unaona ni kawaida kukifanya.

Pamoja na kukifanya, ndani ya dhamiri yako unasikia kushtakiwa, unaona unalolitenda sio sahihi kabisa kulifanya. Muda mwingine unaweza kufikiri labda ni kawaida ukiwa kama mkristo kufanya hivyo, baada ya kuona hakuna namna ya kuacha.

Unaweza ukawa unashindwa kuacha ile tabia mbaya uliyokuwa nayo kabla hujaokoka, ukiacha siku mbili tatu, unajikuta unairudia tena kwa siri. Ukijitahidi kuacha unajikuta unashindwa kabisa.

Labda unasumbuliwa na ulevi, watu hawajui kama bado unakunywa pombe ila wewe unaelewa huwa unakunywa kwa kificho kikubwa sana. Ambacho sio rahisi mtu kukubaini zaidi ya mtu wako wa karibu sana, anaweza akawa mke/mume wako.

Unaweza ukawa unashindwa kuacha uzinzi/uasherati, kila ukijaribu kujiepusha nao, unajikuta umeangukia kwenye hiyo dhambi. Hicho kitu kinaweza kuwa kinakusumbua sana moyo wako, inaweza kuwa hicho kitu ndicho kinakufanya ukose ujasiri mbele za Mungu.

Unaweza ukawa unasumbuliwa na shida ya kujichua, unajaribu kuacha kwa akili zako lakini unashindwa kuacha hiyo tabia, umeoa/umeolewa kabisa ila bado hiyo tabia unayo. Sio kwamba unaipenda hiyo tabia, huipendi kabisa ila unajikuta unaitenda.

Hupendi kabisa kuangalia picha mbaya za uchi ila unajikuta unasukumwa kuangalia hizo picha, na ukishaziangalia unabaki unajuta kwanini uliangalia. Hupendi ila unajikuta umeangalia usilichokipenda kukiangalia.

Hupendi kabisa tabia ya uwizi ila unajikuta unaiba kwa siri, kitu chochote kikikaa vibaya na una uhakika hakuna anayekuona unajikuta umekidokoa. Simu inaweza ikakaa vibaya ukaibeba, pochi ya mtu anaweza kuiweka vibaya ukaibeba.

Mtu mmoja alikuwa mvutaji wa sigara sana akawa anasema hivi, nimejaribu kutumia kila njia kuacha sigara nimeshindwa kabisa. Anasema, niliambiwa dawa fulani ya mswaki inaondoa hamu ya sigara, nikaitumia, lakini sikuona matokeo yeyote mazuri ya kunisaidia kuacha sigara.

Huyu ndugu anatamani sana kuacha sigara ila anajikuta anaendelea kuvuta kitu asichopenda kukifanya. Unaweza kumlaumu kwa uvutaji wake wa sigara bila kumpa njia ya kuacha hiyo tabia, ataona unamwonea tu bure kwa kumlaumu kwa kitu ambacho yeye mwenyewe anapambana kukiacha.

Mtume Paulo anatuthibitishia hili kwenye moja ya nyaraka zake, akasema hivi;

Rejea: Kwa maana lile jema nilipendalo, silitendi; bali lile baya nisilolipenda ndilo nilitendalo. RUM. 7:19 SUV.

Umeona hapo, kumbe mtu unaweza kufanya kitu ambacho hukipendi kabisa kukifanya, bila kujua shida ni nini inayokufanya uendelee kufanya kitu ambacho hukipendi wala Mungu mwenyewe hapendi. Utaendelea kukifanya hicho kitu ukifikiri hakuna njia nyingine ya kuweza kupata suluhisho.

Ipo sababu inayokufanya uendelee kufanya hilo usilolipenda, na kushindwa kufanya kile unakipenda kukifanya. Leo unaenda kujua ni kitu gani kinakusababisha ufanye kitu/jambo usilopenda kufanya, na lile unalopenda hulifanyi ipasavyo.

Unatamani kusoma Neno la Mungu kila siku, kila ukijaribu kuweka ratiba yako vizuri, ikifika muda huo unajikuta umeng’ang’ana kwenye mambo yasiyo na msingi wowote kwako. Unaweza ukawa unadhurura tu kwenye mitandao ya kijamii, tena vitu uvyoangalia huko havifai kabisa, unajikuta vinakumalizia muda wako wote.

Unatamani sana kupata hata nusu saa ya kuomba Mungu ila unajikuta muda wako unaumaliza kwa vitu visivyofaa, unaweza kujikuta unakesha kuangalia mpira ila maombi huwezi, unaweza kuwa unakesha kuangalia tamthilia hadi usiku wa manane ila kuomba unashindwa.

Unashindwa kwa sababu unakuwa umechoshwa na vitu visivyofaa kwako sana, vile vitu vya msingi sana kiroho unajikuta unashindwa kabisa kuvifanya.

Kitu gani sasa kinakuwa kinasababisha tufanye hivyo, kitu gani hasa kinatuzuia kufanya mazuri badala yake tunaishia kufanya yale mabaya tusiyopenda kuyafanya?

Hebu tuone maandiko matakatifu yanasemaje kuhusu hili, ndio Neno la Mungu lina majibu ya hili swali ambalo huenda umekuwa ukijiuliza sana ndani yako.

Rejea: Basi kama lile nisilolipenda ndilo nilitendalo, si mimi nafsi yangu nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu. RUM. 7:20 SUV.

Haleluya, kumbe kinachotusumbua ni ile dhambi ikaayo ndani yetu, dhambi inayoishi ndani yako ndio inakuwa inakusuma kufanya yasiyofaa. Na yale yanayofaa unakuwa unashindwa kufanya.

Sasa tumeshajua mbaya wetu ni yupi, mbaya wetu ni kuendelea kuelea dhambi ndani yetu bila kuitubia hiyo dhambi. Huenda hatuibii hiyo dhambi kutokana na kujiona tupo vizuri kiroho, tunajiona tupo vizuri kiroho ila kuna tabia chafu tunakuwa nazo.

Chukua hatua sasa ya kuomba toba au kutubu mbele za Mungu, baada ya hapo jiondoe kwenye mazingira yeyote yanayokuvutia kumtenda Mungu dhambi. Kutenda yale mbaya usiyopenda kufanya, ukishakaa mbali na hayo mazingira sasa jibidiishe kwenye Neno la Mungu.

Rejea: Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema. MIT. 28:13 SUV.

Neno la Mungu ndilo litaendelea kukutengeneza vizuri na kuwa katika viwango vizuri vya kiMungu. Ule uchanga wa kiroho wa kuanguka anguka hovyo kwenye dhambi utakutoka wenyewe ila lazima ukubali kuzaliwa mara ya pili.

Yaweke haya kwenye matendo ndipo utaona mabadiliko kwenye maisha yako, bila kuweka kwenye matendo, bila kuchukua hatua, utabaki kama ulivyo.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
WhatsApp: +255759808081.