Utajiuliza swali gani hili nauliza kwako, nipo sawa kabisa kuuliza hili swali, ni ukweli usiopingika kuna mtu ukimwambia akupe sababu moja ya kwanini anampenda Mungu au kwanini ameokoka, anaweza akaikosa hiyo sababu.

Hii inatokana na wengi wetu tunatamani Mungu atutendee vitu fulani huku sisi wenyewe hatutaki kuwa na uhusiano mzuri wa kumpendeza yeye. Lakini zipo sababu nyingi sana kumpenda Mungu na kumrudishia sifa na utukufu.

Leo naenda kukupa sababu ya kwanini umpende Mungu wako, sio kwamba hukijui hicho kitu, unakijua vizuri sana sema huenda hujui kama ni kitu kikubwa sana cha kumrudishia sifa na utukufu Mungu.

Tunapaswa kuwa na tabia ya kumshukuru Mungu, kukuamsha tu mzima au ukiwa hai, ni muujiza mkubwa sana kwako. Wapo wenzako walivyolala jana hawakuweza kuamka tena.

Unaweza kusema kuamka tu nikiwa mzima ndio nimshukuru Mungu! Ndio unapaswa kumshukuru Mungu wako. Uzima wako ndio unakufanya uendelee kuweka alama nzuri ya kukumbukwa kwa matendo yako mazuri, uzima wako unakufanya uendelee kutimiza maono yako ukiwa hai.

Jambo lingine la msingi sana la kuendelea kumpenda Mungu wako ni kwa sababu anasikiliza sauti yako wakati unamwomba akusaidie jambo fulani, au akupe jambo fulani.

Jiulize ni watu wangapi Duniani wanaenda mbele za Mungu kumwomba kila dakika, ni watu wangapi Duniani wanamwomba Mungu alafu bado hawajajibiwa maombi yao. Lakini wewe anakusikia na kukujibu maombi yako.

Rejea: Haleluya. Nampenda BWANA kwa kuwa anaisikiliza Sauti yangu na dua zangu. ZAB. 116:1 SUV.

Ukishajua hili moyo wako utajaa shukrani nyingi za upendo mbele za Mungu, hutakosa jambo la kumshukuru Mungu wako kwa matendo yake makuu kwako. Hata kama kuna shida kubwa unaipitia, fikiri ni mambo mangapi Mungu amewahi kukujibu au kukusaidia?

Alafu jiulize hilo moja tu ambalo hajajibu ndio uondoe imani kwake? Hilo tu moja ambalo hajajibu ndio moyo wa kumpenda uishe kwake? Hapana, hatuwezi kuwa watu wa namna hiyo.

Muhimu sana kuwa na Neno la Mungu litatusaidia sana kutukumbusha mambo kama haya, kama unasoma Neno la Mungu kila siku usije ukaacha. Na kama huwa huna tabia ya kusoma Neno la Mungu, anza leo kusoma Neno la Mungu.

Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest,
WhatsApp +255759808081.