Kwa siku tunaweza kujikuta tumesongwa na marafiki, ndugu, majirani, nk. Kama hujasongwa na hao utakuwa umesongwa na mitandao ya kijamii, unaweza kujikuta huna muda kabisa wa kutulia na kutafakari maisha yako.
Unaweza ukajikuta kwa siku usiwe na utulivu kabisa, maana wengine haipiti saa moja lazima achungulie kwenye mitandao ya kijamii kujua kinachoendelea. Hataki kupitwa kabisa na habari ya aina yeyote, tena zingine ni habari za ubuyu tu(umbea) msanii fulani amefanya nini, ametembea na nani, ameachana na nani… habari kama hizo.
Unakutana na mtu anakwambia siku hizi natingwa sana, nakosa kabisa muda wa kusoma Neno la Mungu, nakosa kabisa muda wa kuomba Mungu. Yaani huyu ndugu hana utulivu kabisa, na kweli anachosema sio uongo ila kutingwa kwenyewe anayosemea ni muda wote yupo kwenye magroup ya whatsApp, facebook, instagram, alafu analalamika hana muda.
Mtu yupo kitandani badala ya kulala, anakuwa na muda mwingine wa kuangalia simu yake nani katuma sms, kuna habari gani mpya usiku huo. Siku inaisha kwa huyu ndugu anakuwa hana muda wa kutulia peke yake na Mungu wake.
Wengine hawana simu zenye uwezo wa kuingia kwenye mitandao ya kijamii ila wanachoshwa na makundi ya marafiki, kutwa kukaa kuzungumza siasa, kubishana wenyewe kwa wenyewe. Wataongelea siasa watachoka, watahamia kwenye mpira napo watachoka, watahamia kuwasema watu na hapo napo watachoka na kuhamia lingine.
Watu wa namna hii ukiwagusa kwenye mambo ya msingi kwanini hawafanyi, watakuambia hawana muda, unaweza kuwashangaa ila ndio hivyo wanajua wao hawana muda. Na kweli muda mwingi wanaumaliza kwenye vitu ambavyo haviongezi uhusiano wowote na Mungu wao.
Vizuri kama mkristo kuwa na muda wa peke yako, sio vibaya kuwa na marafiki, wala sio vibaya kuwa kwenye makundi, bado tupo Duniani. Huwezi kukwepa hili, lakini kuwa na muda wa kujitenga nao, kuwa na muda wa faragha, muda ambao utautumia kusoma Neno la Mungu na kutafakari yale umejifunza.
Hata kama upo katikati ya kundi kubwa, hata kama mpo kambini, tafuta upenyo wa kuwa peke yako, sehemu ambayo haina fujo za watu. Sehemu ambayo unapata nafasi ya kuweka umakini kwenye Neno la Mungu, au unaweza kuwapa taarifa wale wanaokuzunguka wasikupunguzi wakati huo.
Ukiwa kama mkristo mwenye safari ya kwenda mbinguni, tabia zako na mwenendo wako unapaswa kufanana na wa Yesu Kristo. Hili ninalokueleza lipo kimaandiko, Yesu Kristo alikuwa na muda wa faragha, alikuwa na muda wa kuwa peke yake.
Rejea:Lakini mara kwa mara Yesu alijitenga nao ili kwenda mahali pa faragha kuomba. Luka 5:16 NEN.
Huwezi kupata utulivu wa kusoma Neno la Mungu wakati upo katikati ya watu wanaongea mambo yao, huwezi kuomba vizuri ukiwa na marafiki ambao hawana mpango wa kuomba. Lazima ujitenge nao pembeni ndipo utaweza kuzungumza na Mungu wako vizuri.
Ukishajitenga na makelele mengine ni rahisi kumsikia Mungu anasema nini na wewe kupitia Neno lake, unaweza kupata ujumbe uliokusudiwa kwako kupitia usomaji wako wa Neno la Mungu ukiwa kwenye utulivu.
Usishangae unasoma Neno la Mungu kila siku huoni mabadiliko yeyote juu ya usomaji wako, ukichunguza sana utajua mara nyingi huwa unasoma Neno la Mungu kwenye mazingira yasiyo rafiki kwako.
Usiendelee kuchati na marafiki zako huku unasoma Neno la Mungu, usiendelee kuongea na rafiki yako huku unaendelea kusoma Neno la Mungu. Wakati wa kusoma Neno la Mungu na wakati wa kuomba Mungu, ondoa kabisa mlio wa simu yako au zima kabisa simu yako.
Karibu kwenye kundi la whatsApp linalojifunza Neno la Mungu kila siku, njoo ujengewe nidhamu ya kusoma Neno la Mungu kila siku, tuma ujumbe wako kupitia whatsApp +255759808081. Hakikisha una nia ya kweli kujifunza Neno la Mungu.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
WhatsApp: +255759808081.