Kuna mambo mabaya tufanyiwa na marafiki zetu wa karibu, majirani zetu, wafanyakazi wenzetu, maboss zetu, ndugu zetu, wanafunzi wenzetu. Kama binadamu mwenye moyo wa nyama, huwa tunajikuta tunaumia mno na wakati mwingine kuwaza mambo mabaya juu ya wale waliotuumiza mioyo yetu.
Wakati mwingine tunaweza kujikuta tunatafuta namna gani tunaweza kulipiza kisasi kwa wale waliotutendea mabaya. Ndani ya mioyo yetu tunakuwa na mizigo mizito mno, mizigo hiyo haionekani kwa macho ya nyama ila inakuwa inatulemea sana.
Pamoja na kuokoka kwetu, pamoja na kuwa wakristo, bado kuna mambo hatuwezi kuachilia ndani ya mioyo yetu. Hii ni kutokana na uzito wa mambo yenyewe tuliyofanyiwa au tuliyowahi kufanyiwa huko nyuma na watu wenye visa vyao juu yetu.
Wakati mwingine tunajikuta tunateseka zaidi kutokana na uchungu mwingi tulionao mioyoni mwetu, kuliko hata wale waliotutendea mabaya hayo. Hii inatokana na kushindwa kuwaachilia ndani ya mioyo yetu, ambapo kuachilia inakuja pale mtu anaposamehe.
Kusamehe ni changamoto kubwa mno inayotukabili watu wengi, unaweza kumtamkia aliyekukosea, kuwa nimekusamehe ila bado ndani ya moyo wako unabaki na uchungu mwingi. Ndani yako unabaki na hasira ambayo inakuwa kama mimba inayosubiriwa mtu ajifungue mtoto.
Kushindwa kwetu kusamehe waliotufanyia mabaya, haijalishi ni mabaya ya namna gani, sio kana kwamba wote tunakuwa hatuwezi kusamehe. Kushindwa kwako kuachilia aliyekukosea/waliokukosea sio kana kwamba haiwezekani na kwa wengine, wengine wameweza na wanaishi vizuri kabisa.
Kwanini wengine wameweza Kuushinda ubaya waliofanyiwa? Ni kwa sababu wanalijua Neno la Mungu, sio kulijua tu Neno, hilo Neno lipo mioyoni mwao. Na wameliweka kwenye matendo, maana yake wanaliishi hilo Neno, wanachokizingatia wao ni hichi;
Rejea: Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana. RUM. 12:19 SUV.
Pamoja na kuzingatia hayo yaliyoandikwa kwenye hilo andiko hapo, bado ndani ya mioyo yao wanatambua sana. Wanajua dawa ya ubaya sio ubaya, watu wasiomjua Kristo, huwa wana msemo wao, wanasema hivi; ubaya ubaya. Maana yake mtu akimtendea baya naye atalipiza baya vile vile.
Nimewahi kusikia habari moja ya wanandoa wawili, yaani mume na mke, ni miaka mingi kidogo imepita tangu nisikie hichi kisa. Sasa mume alikuwa na tabia mbaya, ya kutembea na wanawake hovyo, mke wake alivyoona hivyo. Na yeye aliamua kulipiza kisasi kwa kutembea na mwanaume mwingine, ni kama kumkomoa mume wake, kumbe alikuwa hajui anajikomoa mwenyewe, yaani anajiangamiza nafsi yake mwenyewe.
Maana mume wake hana mbingu ya kumpeleka, anapofikiri kumkomoa mume wake, hamkomoi kwa chochote, bali anajiharibia uhusiano wake na Mungu wake. Anaamua kuvunja uhusiano wake na Mungu kwa sababu ya kutafuta kumkomoa mume wake.
Lakini walio na Neno la Kristo ndani ya mioyo yao, hawawezi kushindwa na ubaya, bali wao ndio wanaushinda ubaya huo. Haijalishi ni ubaya wa namna gani mtu anakuwa amefanyiwa, wao wanakuwa wanaushinda ubaya huo.
Rejea: Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema. RUM. 12:21 SUV.
Wanaoushinda ubaya, hawaushindi hivi hivi, utu wao wa ndani umepikwa vyema na una akiba ya kutosha ya Neno la Mungu. Kumbe kinachowasaidia ni Neno la Mungu, stamina waliyonayo ya kuweza kuushinda ubaya kwa wema, ni Neno la Mungu ndani yao.
Tumeshatambua sasa dawa ya ubaya sio tena ubaya, bali dawa ya ubaya ni wema, mtu akikutendea mabaya usimrudishie mabaya. Hiyo kazi mwachie Mungu mwenyewe, watapambana naye, maana wa kuweza kulipa kisasi ni Bwana mwenyewe.
Neno la Mungu ndio linaweza kukusaidia kujua haya, hakikisha unakuwa imara zaidi kwenye usomaji wako wa Biblia takatifu. Na kama ulikuwa bado hujaanza kusoma Neno la Mungu, hakikisha unaanza leo kusoma.
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
+255759808081