Mungu wetu anatutendea mengi, tusiyoyajua na tunayoyajua, tunayoyasikia kwa wengine aliowatendea, na tusiyoyasikia kabisa kwa wengine. Maana sio kila mtu utaweza kusikia kile Mungu amemtendea.
Anapotutendea Mungu muujiza mkubwa kwenye maisha yetu, wapo wengine hudhani ni siri yako na Mungu wako. Hupaswi kusema mahali popote, unabaki siri yako na Mungu wako, wengine wanaenda mbali zaidi na kusema haina haja kujipendekeza kwa watu.
Sio kana kwamba wanaongozwa na Roho Mtakatifu kufanya hivyo, wanakuwa wamejaa mitazamo yao ya kibinadamu. Wakati mwingine wamepingana na maagizo ya Mungu aliyowaagiza juu ya kile amewatendea katika maisha yao.
Ni kweli yapo mambo aliyokutendea Mungu kwenye maisha yako huwezi kuyasema kwa watu, hii ni kutokana na Yesu kukuzuia usiseme kile amekutendea. Na hili utaliona ukikosa amani ndani ya moyo wako pale unapotaka kusema kile ulichozuliwa usiseme, pamoja na kukosa amani ndani ya mioyo yao, bado wapo wamesema, na waliposema wamesababisha wakutane na shida kubwa sana kwenye maisha yao.
Yesu Kristo kupitia Roho Mtakatifu anapokuzuia usiseme jambo fulani, anajua ukisema kitatokea nini. Anapokuzuia unapaswa kutii hilo, na anapokuruhusu useme yale amekutendea kwenye maisha yako, hapo napo hupaswi kujizuia kusema. Ukijizuia na wakati uliambiwa useme, unakuwa umekiuka agizo la aliyekutendea muujiza huo mkubwa.
Tupo watu huwa tunafikiri kila kitu hakipaswi kujulikana kwa wengine, tunaona kila kitu kinapaswa kuwa maisha binafsi. Anapoonekana mwingine ameshuhudia mbele za watu yale Mungu amemtendea, mtu huyo huonekana hajasitarabika, huonekana haelewi kitu, huonekana anajikweza, huonekana anaumiza wengine, na mengine mengi.
Yote haya ni kwa sababu tumekosa Neno la Mungu mioyoni mwetu, tunapokuwa hatuna muda wa kusoma Neno la Mungu. Anapotokea mtu mwenye cheo fulani kikubwa akazungumza jambo, hata kama linapingana na Neno la Mungu, mtu huyo anaweza kuaminiwa zaidi. Na hayo aliyozungumza yanaweza kutumika kama nukuu kwenye mazungumzo ya wengi, ambapo haipaswi kuwa hivyo kwa mkristo.
Haijalishi umesoma kitabu cha mtu tajiri sana, mwenye elimu kubwa, kama alichoandika kinapingana na Neno la Mungu. Huyo mtu hapaswi kuaminiwa kutokana na umaarufu wake, wala kutokana na elimu yake, wala kutokana na cheo chake.
Mungu anapokutendea jambo, alafu ukasikia kibali moyoni mwako kueleza kile Mungu amekutendea, eleza watu wajue, eleza ulimwengu ujue vile Yesu Kristo amekutendea jambo kubwa kwenye maisha yako. Kupitia ushuhuda wako, wapo watapokea nguvu mpya, wapo imani zao zitajengeka kwa upya, wapo waliokata tamaa watainuliwa tena.
Sio hayo tu, jina la Bwana litatukuzwa kupitia yale Mungu amekutendea, hata wewe mwenyewe utasema au utahubiri kitu halisi kilichokutokea kwenye maisha yako. Kupitia ushuhuda wako, wapo watu watamwona Yesu Kristo kwa mtazamo wa tofauti kabisa, maana si wote tunafanana tunavyomwona Kristo mioyoni mwetu, japo tumeokoka.
Yesu Kristo baada ya kumponya yule mtu mwenye pepo wengi, mtu yule aliomba kufuatana na Yesu Kristo. Lakini Yesu Kristo alimpa kazi ya kufanya, kazi ya kwenda kuhubiri wengine yale mambo makuu aliyoyatenda Mungu juu ya maisha yake.
Rejea: Na mtu yule aliyetokwa na pepo alimwomba ruhusa afuatane naye; lakini yeye alimwaga akisema, Rudi nyumbani kwako, ukahubiri yalivyo makuu Mungu aliyokutendea. Akaenda zake, akihubiri katika mji wote, yalivyo makuu mambo aliyotendewa na Yesu. LK. 8:38-39 SUV.
Kama Yesu Kristo alitoa kibali cha kwenda kuwaeleza wengine yale mambo makuu aliyomtendea huyo mtu, kwanini wewe unaona ni vibaya kushuhudia wema wa Mungu juu ya maisha yako?
Unapaswa kuelewa kwamba, yapo mambo unayopaswa kusema mbele ya watu kwa kibali cha Yesu mwenyewe, na yapo mambo hupaswi kusema kwa kukosa kibali cha Yesu mwenyewe.
Rejea: Yesu akamwambia, Angalia, usimwambie mtu; ila enenda zako, ukajionyeshe kwa kuhani, ukaitoe sadaka kama alivyoamuru Musa, iwe ushuhuda kwao. Mathayo 8:4.
Unaona huo mstari, Yesu anamwambia aliyemponya, asimwambie mtu, pale pale anampa maagizo ya kwenda kujionyesha kwa kuhani. Na akishajionyesha kwa kuhani, atoe sadaka ya shukrani kama ilivyoamriwa na Musa. Tena anasema ili iwe ushuhuda kwao.
Kumbe kuponywa kwetu ni ushuhuda kwa wengine, kumbe kuinuliwa kwetu ni ushuhuda kwa wengine, kuwa Mungu anaweza kuinua vilivyoonekana vinyonge kwa wanadamu. Kama Yesu mwenyewe anaagiza hivi, kwanini wewe huwa unapata shida wengine wanaposhuhudia yale Mungu amewatendea?
Neno la Mungu ndio dira ya maisha ya mkristo, likubali Neno la Mungu, na kuwa na muda wa kulisoma na kulitafakari kila wakati. Chakula chako kikuu cha kiroho kiwe ni Neno la Mungu, alafu mafundisho mengine ndio yafuate nyuma.
Habari njema ni kwamba, nimekuandalia darasa zuri la kujifunza Neno la Mungu kila siku, ambapo nakufutilia kwa karibu sana kuhakikisha unasoma Neno la Mungu. Darasa hili linaendeshwa kwa njia ya whatsApp group, unatamani kuwa kwenye darasa hili zuri, tuma ujumbe wako kwenda +255759808081(tumia whatsApp tu)
Mungu akubariki sana.
Ndugu yako katika Kristo,
Samson Ernest.
www.chapeotz.com
WhatsApp: +255759808081