Utofauti wetu tukiwa tumeokoka huonekana pale tunapoanza kufanya mambo tofauti na yale waliyoyazoea watu wasiomjua Kristo, ndio maana unapofanya jambo fulani ukiwa kama mkristo, alafu likawa linaendana na wao wasiokoka, lazima watakutoa kwenye kundi la waliokoka na kukuweka kwenye kundi lao.

Maneno yetu mazuri hayawezi kuwa kitambulisho chetu sana cha watu kutufahamu vizuri na kutuweka kwenye kundi la watu fulani, isipokuwa matendo yetu ya kila siku ndio yanatutambulisha zaidi kuliko maneno.

Mtu anaweza kukuambia ameokoka ila ukiangalia matendo yake yalivyo, na ukijiangalia na wewe matendo yako yalivyo. Unaona kabisa matendo yake na yako yatofautiana kabisa, utofauti wake ni pale anapofanya mambo kinyume na Neno la Mungu.

Mtu akishaanza kubadilika katika matendo yake, alafu alikuwa mtu wa imani moja, huyo hawezi kuwa ndugu yako kiroho. Maana tayari amehamia upande mwingine wa giza, na unajua giza na nuru havikai pamoja, kimoja kikiingia kingine kinatoka.

Mtu akishakuwa mkristo, akawa anaishi maisha ya kumpendeza Bwana, na wewe ukawa mkristo unayeishi maisha ya kumpendeza Bwana Yesu. Huyo ni ndugu yako kabisa kiroho na kimwili, anaweza akakufaa zaidi kuliko ndugu yako wa damu.

Haijalishi mnasali madhehebu tofauti, kama mahali anaposali wanalitaja jina la Kristo, na wanaenda sawasawa na Mungu alivyoamuru kupitia Neno lake. Huyo ni ndugu yako, tena unapomwona unapaswa kumfurahia na kujisikia vizuri, maana wote ni watoto wa Baba mmoja, ambaye ni Yesu Kristo.

Haijalishi ni mzazi wako, kama imani zenu zinatofautiana, hamuwezi kuwa pamoja, lazima mtakuwa kinyume tu. Maana imani zenu zinatofautiana, imani yako inaweza ikawa kwa Yesu Kristo, mwenzako imani yake ikawa kwenye miungu mingine ya mababu.

Vile vile katika huduma, unapoona mtu anamtumikia Mungu na analitaja jina la Kristo, anaombea wagonjwa kupitia jina la Yesu Kristo, na wanapokea uponyaji kupitia jina la Yesu Kristo. Huyu ni ndugu yako katika Kristo, huyo ni mtendaji mwenzako katika shamba la Bwana, unapomwona mfurahie sana na sio umchukie maana anakusaidia kazi.

Sasa wengine wanapoona Mungu anamtumia sana mtu fulani katika utumishi wake, wanaanza chuki dhidi yake, wanaanza kumsema vibaya kisa amewazidi uwezo. Wanashindwa kuelewa aliyempa uwezo ndiye yule yule waliyempokea kama Bwana na mwokozi wa maisha yao.

Unapoona mtu anatumiwa na Mungu katika kuitenda kazi yake, na wewe unatumika shambani mwa Bwana ila bado huoni Mungu akikutumia kama anavyomtumia mtumishi mwenzako. Hupaswi kuanzisha chuki dhiki yake, bali unapaswa kwenda kumuuliza Mungu, na unapaswa kujifunza kwa aliyekuzidi.

Yesu Kristo alitupa dira nzuri kabisa, alituweka wazi kabisa watu walio kinyume na sisi wapoje, na walio pamoja na sisi wapoje. Baada ya kuona wanafunzi wake wanapata tabu juu ya mtu aliyekuwa anatoa pepo kwa jina la Yesu Kristo, na wakati hawakuwa miongoni mwa wale wanafunzi kumi na mbili.

Rejea: Yohana akajibu akamwambia; Bwana mkubwa, tuliona mtu anatoa pepo kwa jina lako; tukamkataza, kwa sababu hafuatani na sisi. Yesu akamwambia, Msimkataze, kwa kuwa yeye ambaye si kinyume chenu yu upande wenu. LK. 9:49‭-‬50 SUV.

Mtu yeyote asiye kinyume na wewe atakuwa upande wako, hata kama hampo naye kanisa/dhehebu moja, huyo yupo upande wako. Maana hayupo kinyume na kazi aliyotuagiza Yesu Kristo tuitende, umeona mtumishi wa Mungu anahubiri injili ya Yesu Kristo, tena ile injili yenyewe. Muunge mkono, mtie moyo, unga mkono huduma yake kwa kutoa mali zako, maana ni mtu aliye upande wako.

Kama umeshachunguza vizuri, watu wote wanaoanza kuwa kinyume na wewe unayefanya kazi ya Mungu. Watu hao mara nyingi wanakuwa ni wale watu waliokuwa wameokoka, alafu wakarudi nyuma, na wale watu wasiotaka kumkubali Yesu Kristo kama mwokozi wa ulimwengu huu.

Mzinzi/mwasherati yeyote hawezi kuwa rafiki yako na wakati unakemea huo uchafu wake, lazima utageuka kuwa adui kwake, vile vile mlevi, mwizi, muongo, mla rushwa, mla madawa ya kulevya, ukishagusa eneo lake. Lazima chuki kubwa iinuke ndani yake juu yako.

Na Yesu akasema yule mtu ambaye hataki kuwa pamoja naye, yaani asiyetaka kumpokea Yesu Kristo, asiyetaka kuishi maisha matakatifu, asiyetaka kuacha sigara, asiyetaka kuacha pombe, asiyetaka kuacha uzinzi, huyo yupo kinyume naye.

Rejea: Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutawanya. LK. 11:23 SUV.

Ukimkuta mtu ambaye hajaokoka, huyo mtu atakuwa na tabia chafu zisizompendeza Mungu, haijalishi ni mtu wa namna gani. Bado hawezi kuwa mtu salama kwako.

Mtu ambaye ana chuki na watumishi wa Mungu wanaoeneza habari njema, na wewe ukawa unatumika. Hata kama hajakufikia uone chuki yake ya wazi, hata kama ni rafiki yako. Huyo ni mtu hatari kwenu wote, lazima na wewe ipo siku atapanga kitu kibaya dhidi yako.

Aliye pamoja na wewe hawezi kukupinga, ukiona upo kwenye huduma na mtu anayekushambulia sana kwa maneno mabaya. Na huyo mtu mpo pamoja naye katika kikundi fulani au kanisa moja, jua huyo si ndugu yako, kuwa naye makini anaweza kukutenda jambo baya. Ikiwezekana kaa naye mbali.

Hii ndio faida ya kusoma Neno la Mungu, kama ulikuwa bado hujajiunga na darasa la kusoma Neno la Mungu kila siku kwa njia ya whatsApp group. Tuma ujumbe wako sasa kwenda +255759808081, utaunganishwa kwenye group la CHAPEO YA WOKOVU.

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

www.chapeotz.com

WhatsApp: +255759808081