Inaweza kukuwia vigumu kuwa na furaha pale unapokuwa unapita kwenye jaribu nzito, ugumu unaletwa kutokana na maumivu makali unayokutana nayo wakati huo.

Wote tunajua hakuna jaribu rahisi, majaribu mengi ni magumu sana kuvuka, majaribu mengi ni magumu sana kustahimili. Kuzungumza inaweza ikawa rahisi ila likikukuta hilo jaribu, unaweza kutamani ardhi ipasuke uingie mzima mzima.

Wengine huwa wanafika wakati wanataka kujidhuru kwa sumu, kujinyoga, kujipiga na risasi. Lakini mtu aliyeokoka, ana utofauti wake, tena ipo neema inayomfunika wakati huo.

Tunapojaribiwa juu ya imani yetu, tunapaswa kufurahi, maana katika kujaribiwa kwetu pale tunapohimili hayo majaribu. Wale wanaotutazama humtukuza Yesu Kristo, wengine hutamani kuokoka kutokana na kuona tumetoka salama pasipo kumkosea Mungu.

Tunapaswa kufurahi wakati tunajaribiwa, maana katika kujaribiwa kwetu, tunakuwa imara zaidi kwenye imani yetu katika Kristo kuliko tulivyokuwa kabla ya kujaribiwa. Na majaribu yanathibitisha ukomavu wa imani yetu, pale tunaposhinda.

Rejea: Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. YAK. 1:2‭-‬3 SUV.

Ndugu yangu, wakati wa kujaribiwa kwako unapaswa kuhesabu kuwa ni furaha, wakati wa kujaribiwa sio wakati wa kujitenga na mambo ya Mungu. Sio wakati wa kuacha kusoma Neno la Mungu, sio wakati wa kuacha kuhudhuria ibada za kanisani, sio wakati wa kuacha maombi, sio wakati wa kujitenga na wapendwa wenzako.

Wakati wa kujaribiwa kwako, ndio wakati wa kuweka bidii zaidi kwa mambo ya Mungu, na ndani yako unapaswa kufurahi. Hata kama kwa nje unaonekana kuumizwa na jaribu, tunapaswa kuwa na furaha yenye matumaini makubwa.

Furaha ambayo inaambatana na matumaini makubwa, mtu anapoongea na wewe atoke akiwa anashangaa jinsi unamwamini Yesu Kristo. Aone shida uliyonayo bado haijakutoa kwenye imani yako, badala ya kubaki kukutia moyo wewe, wewe ugeuke kuwa faraja kwake.

Tena Neno la Mungu linasema ana heri yule mtu astahimiliye majaribu, maana akiisha kukubaliwa na Bwana ataipokea taji ya uzima. Kumbe ipo taji ya uzima kwa wale wote wanaostahimili majaribu, ambao wakati wa kujaribiwa kwao hawamkosei Mungu wao.

Rejea: Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, Bwana aliyowaahidia wampendao. YAK. 1:12 SUV.

Kama ulikuwa unafikiri majaribu yatakoma kwako, utakuwa unajidanganya ndugu yangu, hasa ukiwa umeokoka, kila wakati utakutana na jaribu. Lengo likiwa kukuondoa kabisa kwenye imani yako, kama hutokuwa mwangalifu utaangushwa na jaribu hilo.

Ukishavuka jaribu moja, ni kama maandalizi ya jaribu lingine kubwa zaidi mbele yako. Usipojua nini kinatafutwa kwako, utachokea njiani na mwisho wa siku utaona bora kuachana na mambo ya wokovu.

Mfano, kwa vijana wengi wakishaumizwa na mahusiano kadhaa, anaacha na wokovu, wengine wanajiingiza kwenye mahusiano na watu wasio wa imani zao. Kama ni dada, anaona wakaka wa kanisani hamwoni, wanaoa wanawake wengine wanamwacha yeye.

Ukishakutana na jaribu lolote kwenye maisha yako, unapaswa kuelewa ni kitu gani inatafutwa kwako, uwe unafahamu imani yako inawindwa. Kwahiyo unapaswa kufurahi kwa sababu kiwango chako cha imani kinaenda kuongezeka na kuimarishwa zaidi, pale utakapovuka kwenye jaribu hilo.

Zaidi unapaswa kufurahi kwa sababu unaye Yesu Kristo, unaye aliyeshinda jaribu la kifo na mauti, unaye aliyeshinda majaribu makubwa zaidi ya hayo unayopitia. Furahi kwa sababu hilo jaribu utalishinda, halitakuweza kamwe, maana unaye Yesu moyoni mwako.

Hii ndio faida ya kujua Neno la Mungu, bila Neno la Mungu huwezi kushinda majaribu mengi, unapaswa kujifunza Neno la Mungu kila siku. Nikualike katika darasa la kusoma Neno la Mungu kila siku, darasa hili lipo whatsApp, ili uunganishwe kwenye group hili, tuma ujumbe wako kwenye +255759808081(tumia whatsApp tu)

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

www.chapeotz.com

+255759808081