Kuwa vizuri kiroho, alafu afya zetu zinakuwa mbovu kupita kiasi, biashara zetu zinakuwa mbovu kupita za wasiomjua Kristo, watoto wetu wanakuwa na tabia mbaya kuliko wasiomjua Kristo, hiyo inakuwa sio sawa kabisa.

Vile tunavyozidi kufanikiwa kiroho, tunaona tulikuwa kwenye hatua fulani ya uchanga wa kiroho, baada ya muda fulani tunaona tumesogea hatua fulani. Ndivyo tunavyopaswa kuzidi kufanikiwa katika mambo yetu mingine.

Mafanikio ya kiroho na kimwili, hayapaswi kupishana, bila kuwa na afya njema huwezi kumtumikia Mungu wako vizuri. Kama umefanikiwa kiroho, unapaswa kuidai afya yako urejeshewe na anayetoa afya njema, ambaye ndiye aliyekufanikisha kiroho, ambaye ndiye unayemtumikia.

Ndivyo maandiko matakatifu yanavyotuambia hivyo, kufanikiwa kwetu rohoni, kunapaswa kuambatana na mambo yetu yote, yaani yote kweli unayoyajua na usiyoyajua.

Rejea: Mpenzi naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako, kama vile roho yako ifanikiwavyo. 3 YOH. 1:2 SUV.

Unapoona hali fulani sio nzuri, zinaenda kinyume na mafanikio yako kiroho, unapaswa kwenda mbele za Mungu kudai haki yako sawasawa na Neno lake.

Usikae kimya unaona mambo yako yanazidi kuhabirika, unaona biashara yako haifanikiwi, unaona kazini kwako hukui, unaona kwenye masomo yako kiwango chako kipo chini, unaona kwenye ndoa yako ni mgogoro kila siku, mwambie Yesu Kristo niliondolee haya na kunipa kufanikiwa.

Usiseme ni mambo ya kawaida, je umeenda mbele za Mungu amekuambia ni mambo ya kawaida? Maana huwezi kuwa vizuri kiroho alafu Yesu Kristo ashindwe kuzungumza na wewe, na akizungumza na wewe utamsikia na kumwelewa vizuri.

Wengine wamejitungia misemo yao, eti kama umeandikiwa sio wa kufanikiwa ni sio wa kufanikiwa tu, hata kama utajituma sana. Huo ni upotofu, ni kukosa Neno la Mungu moyoni, wewe hujazaliwa uwe mtu wa kuumwa tu, hujaletwa Duniani uje uwe unaugua tu, na uje uwe maskini tu.

Kama rohoni unaona mafanikio makubwa, na mambo yako mengine unapaswa kuyaona hayo mafanikio, kwenye afya yako unapaswa kuona ukiwa na afya njema. Unaona una afya mgogoro idai mbele za Mungu, unaona mambo yako hayaendi vizuri, mweleze Yesu ayaweke vizuri.

Tena Mungu mwenyewe anakupa ruhusa ya kueleza mambo yako, ili apate kukupa haki yako, kumbe una haki zako, na hizo haki zako anayeweza kukupa ni Mungu mwenyewe.

Rejea:Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako. ISA. 43:26 SUV.

Unaweza kuwa unasema nimeomba sana juu ya mambo yangu, lakini bado sijaona kufanikiwa, usichoke kumkumbusha Mungu wako. Hojiane naye, mweleze mambo yako, naye atakupa sawasawa na Neno lake.

Kama ni hali ya uchumi wako unapaswa kumwambia Mungu arejeshe afya ya uchumi wako, kama ni magonjwa kila siku wewe ni mtu wa kuingia hospital na kutoka, kila siku unatembea na madawa kama unauza kumbe ni ya kunywa mwenyewe. Mwambie Yesu Kristo akuondolee magonjwa kwenye mwili wako.

Ndugu msomaji wangu, sikuelezi haya kama maneno ya kawaida, hapana, Neno la Mungu ni amina na kweli, hakikisha kufanikiwa kwako rohoni, na kwenye afya yako napo unafanikiwa, maana yake inakuwa njema.

Usitishwe na mazingira ya nje, angalia Neno la Mungu linasemaje juu ya afya yako, juu ya mambo yako mengine, kama umefanikiwa kiroho ni lazima ufanikiwe na kimwili pia. Haina kujadiliana sana, unapaswa ufanikiwe haswa.

Haya ni matunda ya kusoma Neno la Mungu kila siku, unazijua haki zako za msingi. Karibu kwenye darasa letu la kusoma Neno la Mungu kila siku, hili darasa letu lipo whatsApp group, ukiwa na simu yako yenye uwezo wa whatsApp tunaweza kuungana pamoja. Unajisikia moyoni mwako kuungana na wapendwa wenzako wanaojifunza Neno la Mungu, tuma ujumbe wako kwenda +255759808081(tumia whatsApp tu)

Mungu akubariki sana.

Ndugu yako katika Kristo,

Samson Ernest.

www.chapeotz.com